Habari za Punde

JK: Mgao wa umeme kukoma 2015

 
Na Kunze Mswanyama, Dar
RAIS wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dk. Jakaya Kikwete amewatangazia rasmi watanzania kwamba mgao wa umeme utamaliza ifikapo 2015.
Tanzania imekuwa ikitumia kiasi cha shilingi zaidi bilioni moja kila mwaka kugharamia umeme wa mafuta kuepuka mgao wa umeme.
Rais aliyasema hayo jana wakati akizindua rasmi mradi wa ujenzi wa mitambo ya kusafishia na kusafirisha gesi uliopo Kinyerezi, Manispaa ya Ilala jijini Dar es Salaam, ambapo gesi hiyo itatumika kuzalisha umeme wa megawati 3600 hadi utakapomalizika mwaka 2014.
Alisema kutokana na kumalizika kwa mgao ajira zitaongezeka huku watanzania wakitarajiwa kuishi maisha kama wanayotakiwa kuishi watu waliopo kwenye karne ya 21.

Mradi huo wenye thamani ya shilingi trilioni moja (dola bilioni 1.225) ni mkopo wenye masharti nafuu kutoka China.
“Sasa nimeamini msemo usemao akufaae kwa dhiki ndiyo rafiki.Tumehangaika na matatizo ya umeme kwa muda mrefu ambapo tulikosa majawabu lakini sasa tumeyapata,” alisema Rais Kikwete.
Huku mvua kubwa ikinyesha, Rais alikiri kuwa akiwa Waziri wa Nishati na Madini mwaka 1988-1994, alianzisha mchakato wa kupatikana umeme wa gesi lakini alikabiliwa na vikwazo vingi vilitoka Benki ya Dunia ambapo benki hiyo ilisema haiwezekani kwa Tanzania kutumia gesi kuzalisha umeme bali iendelee na umeme wa kutegemea maji.
“Wengi tuliamini kuwa umeme wa maji ndiyo mwisho na mimi ni mmoja wa walioamini hivyo. Lakini leo hii tuna matatizo ya umeme kutokana na kutegemea maji ambayo yameathiriwa na matatizo ya tabianchi hivyo kutokuwa na umeme wa uhakika.Mradi huu ni moja ya njia za kutafuta mbadala wa umeme wa maji,” alisema.
Alisema ifikapo 2015 Tanzania itakuwa ikihitaji megawati 2780 ambapo kama zikikosekana itabidi kutumia vibatari kupata mwanga na pia kuendesha viwanda kwa kutumia mkaa jambo ambalo haliwezekani daima.
Alioneshwa kushangazwa kusikia kuwa mkoa wa Dar es Salaam pekee kwa siku hutumia magunia ya mkaa 40,000 ambapo kama gesi hiyo ikipatikana kwa wingi itaweza kuokoa mazingira kwani itatumiwa majumbani na viwandani ili kuongeza uzalishaji.
Aliwaahidi wananchi kuwa,umeme huo utatosha nchi nzima na mwengine utauzwa nchi za jirani ambazo zina upungufu wa nishati hiyo.
Pia alisema makaa ya mawe kutoka Ngaka, Mchuchuma na Liganga itaweza kuzalisha umeme mara baada ya kukamilika michakato inayoendelea sasa.
“Naamini tutatumia gesi majumbani, viwandani na kwenye magari yetu tutaachana na matumizi ya petrol na dizeli ambazo ni kikwazo kikubwa kwa maendeleo yetu. Nimesikia kuwa gesi hii itatufaa kwa miaka 90 zaidi. Kama nikijaaliwa uzima baada ya miaka hiyo 90 nitakuwa na miaka 150”, alisema Rais Kikwete.
Kwa upande wake Waziri wa Niashati na Madini, Prof. Sospeter Mhongo, alisema hadi sasa Tanzania inatumia asilimia 54.8 ya umeme wa maji na asilimia 29.8 ya umeme wa mafuta.
Alisema, serikali imeamua kutafuta njia mbadala za kuzalisha umeme ambapo sasa umeme utazalishwa kutokana na makaa ya mawe, gesi, maji, upepo, joto ardhi na bayogesi ili kuondoa upungufu wa nishati hiyo unaolikumba taifa kila mwaka.
Aliongeza kuwa,umeme huo utaongeza pato la taifa kutoka dola bilioni 24 za sasa hadi dola bilioni 33 ifikapo 2015 baada ya kuanza kuzalishwa kwa megawati 2780 kutoka megawati 1438 zinazozalishwa sasa ambazo hazitoshelezi.
Naye Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Maendeleo ya Petroli (TPDC), Yona Kilaghane, alisema mradi huo ambao ni mkubwa kufuatia ule wa Algeria wenye urefu wa kilomita 2475.
Alisema mradi huo utakuwa na urefu wa kilomita 532 kutoka Mtwara hadi Dar es salaam.
Naye Balozi wa China nchini, Lu Youqing alisema anajivunia mradi huo kutekelezwa kipindi cha uongozi wake kwani ni mradi mkubwa ambao ni wa kwanza kwa Afrika kutokana na thamani ya fedha kubwa itakayotumika.
Alisema hadi sasa China imewekeza makampuni zaidi ya 300 yanayojishughulisha na miradi mbalimbali kwenye kilimo, miundombinu na miradi ya kiuchumi nchini Tanzania.
Huo ni mradi wa kwanza mkubwa kwa China kutoa kwa nchi marafiki.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.