Habari za Punde

Lema akwaa kisiki

 
Na Kunze Mswanyama, Dar
MAHAKAMA ya Rufaa ya Tanzania, imemwamuru aliyekuwa Mbunge wa Arusha mjini kupitia Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), Godbless Lema, kufanya marekebisho katika hati yake ya kukaza hukumu ya mahakama kuu iliyomvua wadhifa huo, aliyokuwa ameiambatanisha katika rufaa yake.
Mahakama hiyo imempa siku 14 Lema kufanya marekebisho hayo, kuanzia jana, na kisha kuwasilisha upya rufaa yake mahakamani hapo.
Uamuzi huo wa mahakama ya rufaa ulitokana na kukubaliana na hoja moja ya pingamizi lililowekwa na makada watatu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), dhidi ya rufaa hiyo aliyoikata Lema.
Mahakama hiyo ilikubali hoja ya wajibu rufaa kuwa rufaa hiyo ilikuwa na dosari kutokana na tofauti ya vifungu vya sheria vilivyotumika katika hukumu iliyomvua ubunge, na vilivyotumika katika hati ya kukaza hukumu, iliyowasilishwa mahakamani sambamba na rufaa hiyo.

Hata hivyo kilichomwokoa Lema ni kifungu cha 111 cha kanuni za mahakama, ambapo mahakama hiyo ilisema kuwa chini ya kanuni hiyo dosari hizo zinaweza kurekebishwa.
Chini ya kanuni hiyo, mahakama ya rufaa ilimwamuru Lema kupitia kwa Mawakili wake, Tundu Lisu na Method Kimomogoro,kufanya marekebisho ya dosari hizo zilizobainika na kisha kuwasilisha upya rufaa yake ndani ya siku 14 kutoka jana.
Lema alivuliwa wadhifa huo na mahakama kuu kanda ya Arusha, Aprili 5, 2012 kufuatia kesi iliyofunguliwa na wanachama watatu wa Chama cha Mapinduzi (CCM), Mussa Mkanga, Happy Kivuyo na Agnes Mollel, wakipinga ushindi wake katika uchaguzi mkuu mwaka 2010.
Lakini baadaye, alikata rufaa mahakama ya rufaa, kupitia kwa wakili wake Method Kimomogoro kupinga hukumu ya mahakama kuu, huku akitoa hoja 18 za kupinga hukumu hiyo.
Tarehe ambayo rufaa hiyo ilipangwa kusikilizwa na jopo la Majaji watatu Mahakama ya Rufaa; Salum Massati, Natalia Kimaro na Jaji Mkuu, Mohamed Othman Chande (kiongozi wa jopo), wakili wa wajibu rufaa, Alute Mughwai, aliweka pingamizi la awali.
Katika pingamizi hilo, wakili Mghwai aliiomba mahakama hiyo iitupilie mbali rufaa hiyo, akidai kuwa ina kasoro za kisheria na za kikanuni, huku akibainisha hoja tatu za kuunga mkono pingamizi hilo.
Hoja hizo za pingamizi la awali zilikuwa ni pamoja na kuchanganywa au kutofautiana kwa vifungu vya sheria ya uchaguzi ya mwaka 2010, kati ya hukumu iliyomvua ubunge na hati ya kukaza hukumu hiyo.
Hoja nyingine ni kwamba hati ya kukaza hukumu hiyo haikuwa na mhuri wa Jaji aliyeitoa wala tarehe ambayo hati hiyo ya kukaza hukumu ilitolewa.
Hoja ya tatu ilikuwa ni mtindo wa kuandika hati ya kukaza hukumu, kwa kutokuandika maneno, “imetolewa kwa mkono wangu na mhuri wa mahakama”.
Hata hivyo, katika uamuzi wake jana, mahakama ya rufaa ilikubaliana na hoja moja ya pingamizi hilo, kuwa tofauti au kuchanganywa kwa vifungu hivyo vya sheria ni dosaria mbayo inaifanya hati hiyo isiwe halali, na ikatupilia mbali hoja nyingine mbili kuwa hazina msingi.
Uamuzi huo uliondikwa na Jaji Nathalie Kimaro kwa niaba ya jopo hilo, ulisomwa na Naibu Msajili wa Mahakama ya Rufaa, Zahra Maruma.
Katika uamuzi huo, mahakama hiyo ilisema kisheria, hati ya kukaza hukumu lazima ikidhi masharti ya amri ya xx, kanuni ya 6 na 7, sura ya 33, inayotaka hati ya kukaza hukumu ikubaliane na hukumu, iwe na tarehe iliyotolewa na isainiwe na jaji aliyeitoa.
“Katika shauri hili, hati ya kukaza hukumu haikubaliani na hukumu. Hukumu inarejea kifungu cha 114 (1)-(7), (sheria ya uchaguzi), lakini hati ya kukaza hukumu inarejea kifungu cha 113 (1)- (7),” ilisema mahakama hiyo na kuongeza,“Hati ya kukaza hukumu (katika shauri hilo) inakiuka amri ya xx kanuni ya 6 na 7 za mwenendo wa mashauri ya madai.”
Hata hivyo, mahakama ilisema kuwa inakubaliana na mawakili wa wajibu pingamizi hilo kuwa kosa hilo linaweza limetokana na kuteleza kwa kalamu ama kutokana na kosa la uchapaji.
Ilisema mbali na kosa hilo la kuchanganya vifungu, hati hiyo ya kukaza hukumu inakidhi matakwa yote ya kwa kuwa imesainiwa na jaji (Rwakibalia aliyeitoa), na kuandikwa tarehe iliyotolewa ambayo ni Aprili 5, 2012.
“Katika mazingira haya tumebaini kuwa hoja ya kwanza ina nguvu katika kiwango cha kuchanganya vifungu vya sheria. Lakini pia tunadhani lilitokana na kuteleza kwa kalamu au kosa la uchapaji,” lilisema jopo hilo na kuiongeza: “Kwa sababu hii linaweza kurekebishwa chini ya kanuni ya 111 ya kanuni za mahakama.”
Kuhusu hoja ya pili, kutokuwa na mhuri wa jaji na saini yake, mahakama ilisema kuwa kutokutekeleza masharti ya kanuni za masjala ya mahakama kuu hakuwezi kuifanya hati ya kukaza hukumu isiwe halali.
Kuhusu hoja ya tatu, pia mahakama hiyo ilisema kuwa chini ya sheria ya mwenendo wa mashauri ya madai, kifungu cha 101 (1) na (3) hakuna mfumo maalumu wa kuandika hati ya kukaza hukumu.
Hivyo mahakama hiyo ilisema kuwa kukosekana kwa maneno,” imetolewa chini ya mkono wangu na mhuri wa mahakama, hakuathiri hati hiyo ya kukaza hukumu na kwamba hoja hiyo haina nguvu.
Hata hivyo mahakama hiyo ilisema kuwa hati hiyo ya kukaza hukumu inaonesha wazi kuwa imesainiwa na Jaji na jina lake liko wazi na kwamba kukosemana kwa maneno hayo hakuweza kuathiri mamlaka yake .
“Kwa mazingira haya, kwa hoja ya kwanza ya pingamizi, ni mtizamo wetu kwamba hati ya kukaza hukumu ina dosari na tunakubaliana na pingamizi,” ilisema mahakama ya rufaa na kuongeza:“Hata hivyo, kama tulivyokwisha kubainisha awali, kosa hilo linaweza kurekebishika. Hoja nyingine (za pingamizi) tumeona kwamba hazina mashiko na tunazitupilia mbali.”
“Tunamruhusu mkata rufaa kuwasilisha hati ya kukaza hukumu iliyofanyiwa marekebisho, chini ya Kanuni ya 111 ya Kanuni za Mahakama ya Rufani za mwaka 2009. Mrufani anapewa siku 14 kutoka siku ya kutoa uamuzi huu, kuwasilisha hati ya kukaza hukumu iluyofanyiwa marekebisho.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.