Na Rajab Mkasaba, Vietnam
MKE wa Rais wa Zanzibar Mama Mwanamwema Shein ameeleza haja ya kuanzishwa uhusiano na ushirikiano kati ya sekta ya afya ya Zanzibar na hospitali ya Taifa ya Watoto ya Vietnam katika maeneo ya mafunzo na ziara za Madaktari bingwa ili kuimarisha huduma za tiba kwa watoto wanaozaliwa na matatizo ya kiafya.
Mama Mwanamwema Shein aliyasema hayo wakati alipotembelea hospitali hiyo ya wagonjwa maalum ya watoto hasa katika maeneo ya upasuaji wa kichwa, moyo, pamoja na wale wanaozaliwa kabla ya muda.
Katika maelezo yake, Mama Mwanamwema Shein alieleza kuwa kuwepo kwa uhusiano na ushirikiano kati ya pande mbili hizo kutasaidia kwa kiasi kikubwa kuimarisha sekta ya afya na kutoa huduma kwa watoto wenye matatizo maalum.
Akiwa katika ziara yake hiyo fupi hospitalini hapo, Mama Mwanamwema Shein alitoa shukurani kwa fursa aliyoipata ya kuweza kujionea kazi kubwa wanayofanya Madaktari na Wauguzi hospitalni hapo katika kuokoa maisha ya watoto na kuweza kuwaletea matumaini ya maisha yao.
Alisema kuwa huduma za hospitali hiyo kwa watoto wenye matatizo mbali mbali zinamkumbusha enzi zake za utumishi wa zadi ya miaka 30 aliyofanya kazi katika sekta ya afya kweye hospitali mbali mbali za Zanzibar.
Madaktari na Wauguzi hospitalini hapo, walimueleza Mama Mwanamwema Shein kuwa tangu kujengwa kwa hospitali hiyo mnamo mwaka 1969 kumekuwa na maendeleo makubwa ambapo hospitali hiyo ilianza na vitanda 123 tu na sasa wana uwezo wa kulaza wagonjwa 1165.
Walimueleza kuwa hospitali hiyo imepiga hatua kubwa katika utaalamu na teknolojia ambapo sasa ina uwezo mkubwa wa kushughulikia upasuaji wa kichwa, moyo pamoja na kuokoa maisha ya watoto wanaozaliwa kabla ya kutimiza muda wa miezi tisa wakiwa tumboni.
Aidha, Madaktari na Wauguzi hao walimueleza Mama Shein kuwa hospitali hiyo hivi sasa ina uwezo wa kujitengenezea wenyewe vifaa mbali mbali vinavyotumika katika wodi za watoto wanaozaliwa kabla ya muda jambao ambalo linasaidia sana katika kupunguza matumizi makubwa ya fedha kwa kuagiza vifaa kutoka nje ya nchi.
Mama Mwanamwema pia, alitembelea Makumbusho ya Taifa ya Wanawake yaliopo mjini Hanoi ambayo shughuli zake zote zinaonyeshwa na kufanywa na akina mama.
Akitoa shukurani kutokana na mapokezi mazuri aliyoyapata kutoka kwa akina mama hao, Mama Mwanamwema alisema kuwa mwanamke ana mchango wa pekee kwa ujenzi wa Taifa hivyo anathamini na kuzipongeza juhudi zao.
Alisema kuwa mwanamke ana nafasi muhimu katika kuleta maendeleo na maisha bora kwa familia hivyo kuna haja ya kuenziwa na kutunzwa vizuri sanjari na kutambuliwa mchango wake mkubwa katika jamii.
Makumbusho hayo yameganywa katika sehemu tatu ambazo zinaeleza hatua mbali mbali muhimu walizopita wanawake wa nchi hiyo tangu kipindi ambacho Vietnam ikipambana na wakoloni.
Sehemu hizo tatu ni pamoja na maisha ya ndoa na mchango wa mwanamke katika kuimarisha familia,umuhimu wa uzazi na nafasi ya mwanamke katika kuongeza ukoo wa jamii iliyomuoa pamoja na mchango mkubwa wa kijeshi wa mashujaa wanawake wa Taifa hilo waliojitolea maisha yao wakati wa vita vya kupigania huru.
Pia, makumbusho hayo yamehifadhi picha za wanawake ambao Taifa hilo linaona wameonesha mfano wa kuigwa katika maeneo hayo matatu, vifaa mbali mbali vilivyotumika katika hatua hizo za maendeleo kama vile nguo za makabila, vyombo vya kupikia, kutwangia nafaka, mapambo ya mwili na nyumbani, vyakula, dawa za kienyeji, sialaha za moto, za kijeshi na vitu vyenginevyo.
Wakati huo huo, Mama Mwanamwema Shein alivitembelea vikundi vya akina mama vinavyojishughulsha na kazi mbali mbali za sanaa za mikono na utengenezaji wa nguo za hariri vilivyopo mjini Haoi, Vietnam.
Mama Mwanamwema alitoa pongezi kwa akina mama hao kwa kuweza kujumuika pamoja na kufanya shughuli hizo za kuwaongezea kipato katika familia na hivyo kuendeleza heshima ya mwanamke katika jamii jambo ambalo ni muhimu sana kulirithisha kwa vizazi vyao.
No comments:
Post a Comment