Na Khamis Amani
VIONGOZI wakuu watatu wa Jumuiya ya Uamsho wakiwa na wafuasi wao watano walioshitakiwa kwa matukio mbali mbali ya uharibifu wa mali, uchochezi, kumficha Sheikh Faridi pamoja na kumtukana Kamishna wa Polisi Zanzibar, wamerudishwa tena rumande.
Washitakiwa hao, wamerudishwa rumande jana baada ya Mrajis wa Mahakama Kuu ya Zanzibar, George Joseph Kazi kumaliza kusikiliza kesi hiyo.
Kurudishwa kwao rumande, kumekuja baada ya Mkurugenzi wa Mashitaka (DPP) Ibrahim Mzee Ibrahim kuwafungia dhamana washitakiwa hao kwa maslahi ya umma, chini ya kifungu cha 19 (1) (2) cha sheria za Usalama wa Taifa sura ya 47 sheria ya mwaka 2002.
Washitakiwa hao walifikishwa mahakamani hapo jana kuendelea na kesi yao hiyo, wakitokea rumande ya chuo cha mafunzo Kilimani, wakiwa chini ya ulinzi mkali wa askari polisi wa kikosi cha kutuliza ghasia (FFU).
Washitakiwa hao ni Farid Had Ahmed (41) mkaazi wa Mbuyuni, Mselem Ali Mselem (52) wa Kwamtipura, Mussa Juma Issa (37) anayeishi Makadara, pamoja na Azan Khalid Hamdani (48) mkaazi wa Mfenesini.
Wengine ni Suleiman Juma Suleiman (66) wa Makadara, Khamis Ali Suleiman (59) mkaazi wa Mwanakwerekwe, Hassan Bakari Suleiman (39) wa Tomondo pamoja na Ghalib Ahmada Omar (39) mkaazi wa Mwanakwerekwe.
Wakiwa mahakamani hapo, wakati shauri hilo lilipofikishwa kwa ajili ya kutajwa, jopo la Wanasheria wa serikali kutoka Ofisi ya Mkurugenzi wa Mashitaka (DPP), lililoongozwa na Rashid Fadhil, Raya Issa Mselem pamoja na Ramadhan Nassib, wameiamba mahakama kwamba, upelelezi wake bado haujakamilika.
Hivyo, Wanasheria hao wa serikali waliiomba mahakama hiyo kuliahirisha shauri hilo, na kulipangia tarehe nyengine kwa ajili ya kutajwa, ili uweze kupatikana muda wa ziada wa kuendelea na upelelezi huo.
Mara baada ya hoja hizo, upande wa utetezi ulioongozwa na Mawakili wa kujitegemea Salum Taufiq, Abdallah Juma na Suleiman Salum, waliwasilisha mahakamani hapo vitendo vya ukiukwaji wa katiba wanavyofanyiwa wateja wao na maofisa wa vyuo vya mafunzo.
Walidai kuwa, wateja wao wamekuwa wakikosa fursa muhimu wanazostahiki kuzipata wakiwa mahabusu hali ambayo ni ukiukwaji wa sheria pamoja na katiba.
Wakinukuu baadhi ya vifungu vya katiba ya Zanzibar ya mwaka 1988 inayotoa fursa ya watu wote kuwa sawa mbele ya sheria, haki ya kulindwa na kupata haki sawa mbele ya sheria, mawakili hao walidai kuwa wateja wao wamekuwa wakikosa haki hizo na kutendewa tafauti na rumande wengine.
Haki hizo ni kukosa kuonana na jamaa zao, kuletewa chakula kutoka uraiani, kufungiwa ndani ya chumba chake kila mshitakiwa bila ya kupata fursa ya kuonana na washitakiwa wengine zaidi ya asubuhi wanapokwenda haja na mchana kwa muda wa chakula.
Sambamba na hilo, suala la ibada kwa washitakiwa hao limedaiwa kuwa ni gumu kwao, kwani maofisa wa vyuo vya mafunzo hawawapi fursa ya kuabudu ipasavyo hasa kuchanganyika na wengine katika sala ya Ijumaa, suala ambalo linaendana kinyume na katiba katika suala zima uhuru wa kuabudu.
"Haki za washitakiwa hawa zinavunjwa wazi wazi na maofisa wa vyuo vya mafunzo na serikali kwa ujumla, hawa raia kama raia wengine wanapaswa kupatiwa haki zao zote za msingi wanazostahiki," alidai wakili Salum Taufiq.
"Hawana fursa ya kusali sala ya Ijumaa na wenzao, hawana vitabu vya dini, hata ndevu wamenyolewa ili kuwadhalilisha na wamefanyiwa kwa makusudi ili kuwavunjia heshima zao," aliongeza.
Hivyo wakili huyo ameiomba mahakama hiyo kuzingatia hoja hizo na kuzitolea maamuzi yanayofaa.
Akitetea hoja hizo, Mwanasheria wa serikali Ramadhan Nassib alisema kuwa, Ofisi ya Mkurugenzi wa Mashitaka (DPP), haipendelei kuona haki haitendeki pamoja na utumiaji mbaya wa ukiukwaji wa sheria kwa vyombo vya dola.
Pamoja na hilo, ameiomba mahakama hiyo kutoa maelekezo kwa upande huo wa utetezi kuwasilisha hoja zao hizo katika mahakama husika kwa vile hoja zao hizo zimegusia ukiukwaji wa katiba.
Alidai kuwa, Mahakama Kuu pekee ndiyo yenye kusimamia na kusikiliza mashauri yote ya ukiukwaji wa katiba yanayowasilishwa mbele yake kwa ajili ya kutolewa maamuzi.
Kwa upande wake Mwanasheria wa serikali Raya Issa Mselem aliiambia mahakama hiyo isitilie maanani hoja hizo za upande wa utetezi kwa madai kuwa hapo si pahala pake.
"Mheshimiwa maombi yao yatupiliwe mbali, wapewe maelekezo maalumu ya kuona wapi haki za washitakiwa zitapatikana," aliongeza Raya Mselem.
Baada ya kumaliza kusikiliza hoja za pande mbili hizo, George Kazi ambaye pia ni hakimu wa mahakama ya mkoa Vuga, aliiahirisha kesi hiyo hadi Novemba 20 mwaka huu.
Mara baada ya ahirisho hilo, washitakiwa hao waliingizwa katika gari ya polisi yenye nambari za usajili PT 1891 ya OCD Mjini, ikiambatana na gari yenye nambari PT 0873 ya FFU Mjini (M), PT 1449 Polisi ZPA 0001, PT 1407 ya Ufundi/Ujenzi na PT 2086 ya FFU Kaskazini (U) kwa ajili ya safari ya makaazi yao ya muda ndani ya chuo cha mafunzo.
Washitakiwa wote hao wanakabiliwa na mashitaka ya uvunjifu wa amani, ushawishi wa kuchochea na kurubuni watu, kula njama pamoja na shitaka la kufanya kitendo kinachoweza kuleta uvunjifu wa amani, linalomkabili Azan Khalid Hamdani pekee.
Mapema washitakiwa hao walisomewa mashitaka ya uvunjifu wa amani chini ya kifungu cha 3 (d) cha sheria za Usalama wa Taifa sura ya 47 sheria ya mwaka 2002, kwa kuhusishwa na matukio yaliyotokea Oktoba 17 na 18 mwaka huu kuanzia saa 12:00 za asubuhi hadi usiku wa manane.
Katika shitaka hilo, kupitia barabara tofauti zilizomo ndani ya mkoa wa Mjini Magharibi Unguja walidaiwa kuharibu barabara, majengo, vyombo vya moto na piki piki, na walifanya hivyo bila ya kuwepo sababu za msingi za kuharibu na kuteketeza kinyume cha maslahi ya umma na kusababisha hasara ya zaidi ya shilingi 5,000,000.
Shitaka la pili lililokuwa likiwakabili ni la ushawishi na uchochezi, ambapo ilidaiwa kuwa baina ya Mei 26 hadi Oktoba 19, 2010 walifanya mikutano katika maeneo tofauti yakiwemo Lumumba, Msumbiji, Fuoni meli sita na Mbuyuni, ambayo kwa nyakati tofauti walishawisi na kuchochea watu kufanya makosa.
Makosa waliyodaiwa kufanywa ni kuweka vizuizi barabarani kwa kutumia mawe, makontena ya kuhifadhia taka, matawi ya miti, mapipa ya mafuta, kuchoma maringi ya magari, kuharibu majengo tofauti, magari na kusababisha huduma muhimu za jamii za serikali kuweza kuharibwa.
Shitaka la mwisho kwa washitakiwa wote hao lilikuwa la kula njama, ambapo sehemu tofauti zisizojulikana pamoja na muda wake ndani ya wilaya ya Mjini Unguja, kwa pamoja walidaiwa kula njama ya kusababisha Farid Had Ahmed kujificha katika sehemu ambazo hazijulikani na kupelekea uvunjifu wa amani katika jamii.
Ama shitaka la nne la kufanya kitendo kinachoweza kuleta uvunjifu wa amani, lilikuwa likimuhusu Azan Khalid Hamdani pekee, ambalo katika shitaka hilo alidaiwa kumtolea maneno ya kashfa na matusi Kamishna wa Polisi wa Zanzibar.
Sambamba na matusi hayo Azan alidaiwa kumwambia Kamishna huyo kuwa mjinga, jambo ambalo mahakama ilidaiwa kuwa lingeliweza kusababisha uvunjifu wa amani.
Mashitaka yote hayo hawakutakiwa kujibu mara baada ya kusomewa mahakamani hapo na badala yake watajibu mahakama kuu mara baada ya upelelezi wake kukamilika, kutokana na kwamba mahakama hiyo haina uwezo wa kusikiliza kesi za aina hiyo.
No comments:
Post a Comment