Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar Maalim Seif Sharif Hamad akiagana na balozi mdogo wa Oman aliyepo Zanzibar Sheikh Mansoor Al-Busaid baada ya mazungumzo yao yaliyofanyika ofisini kwake Migombani.
Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar Maalim Seif Sharif Hamad akizungumza na Balozi mdogo wa Oman aliyepo Zanzibar Sheikh Mansoor Al-Busaid ofisini kwake Migombani.
Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar Maalim Seif Sharif Hamad akimshindikiza balozi mdogo wa Oman aliyepo Zanzibar Sheikh Mansoor Al-Busaid baada ya mazungumzo yao yaliyofanyika ofisini kwake Migombani
(Picha na Salmin Said, OMKR)Na Hassan Hamad OMKR
Oman imeahidi kuendeleza mashirikiano yake na Zanzibar katika sekta mbali mbali zikiwemo elimu, habari, utunzaji wa kumbukumbu na majengo ya asili.
Balozi mdogo wa Oman aliyepo Zanzibar Sheikh Mansoor Al-Busaid ameeleza hayo wakati akizungumza na Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar Maalim Seif Sharif Hamad ofisini kwake Migombani.
Balozi Al-Busaid ambaye alionana na Makamu wa Kwanza wa Rais kwa ajili ya kumuaga baada ya kumaliza muda wake wa utumishi hapa nchini, amesema mashirikiano hayo yataendelezwa kwa maslahi ya pande zote mbili.
“Hivi sasa waandishi wawili wa gazeti la Zanzibar Leo wako nchini Oman, tumewapeleka kwa ajili ya kuripoti uchaguzi wa mabaraza ya miji ‘municipality election’ na pia tunatarajia kuchukua waandishi wengine wawili wa magazeti kwenda Oman”,alieleza balozi Al-Busaid.
Ameishukuru Serikali pamoja na wananchi wa Zanzibar kwa kumpa ushirikiano mzuri katika kipindi chote cha utumishi wake, na kuahidi kuwa balozi mzuri wa kuzidi kuitangaza Zanzibar nje ya nchi.
Amefahamisha kuwa Zanzibar ni nchi ya amani na pahala pazuri pa kuwekeza, na kuelezea umuhimu wa kuwaalika wawekezaji wengi zaidi kuja kuwekeza.
Nae Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar Maalim Seif Sharif Hamad ameishukuru Serikali ya Oman kutokana na misaada yake kwa Zanzibar ambayo inasaidia harakati za serikali za kukuza uchumi
wake.
Ameelezea kufarajika kwake kutokana na uamuzi wa Sultan Qaboos wa Oman kuanzisha Mfuko wa Elimu Zanzibar ambao utawasaidia wanataaluma wa Zanzibar kukuza ujuzi wao na kuinua kiwango cha elimu nchini.
“Nimepata moyo sana kwa Sultan Qaboos kuanzisha mfuko wa elimu Zanzibar ambao naamini utawasaidia sana wanataaluma wetu, na hii inathibitisha kuwa Sultan Qaboos anaipenda na kuithamini sana Zanzibar”, alifahamisha Maalim Seif.
Maeneo mengine ambayo Oman iko mstari wa mbele katika kushirikiana na Zanzibar ni pamoja na masuala ya utamaduni, afya na utunzaji wa kumbukumbu.
Kwa mujibu wa maelezo ya viongozi hao tayari Sultan Qaboos amekialika kikundi cha taarab cha wanawake cha Zanzibar kwenda nchini Oman kwa ajili ya kuonyesha umahiri wao wa kuimba na kucharaza ala za muziki wa Taarab.
Wamefahamisha kuwa Oman na Zanzibar zina uhusiano wa muda mrefu wa kindugu, na kwamba hata tamaduni zake zinashabihiyana kwa kiasi kikubwa.
No comments:
Post a Comment