Habari za Punde

Ridhwan Kikwete: Klabu zibadilike

Ataka waandishi waepuke unazi wa Simba, Yanga
 
Na Mwajuma Juma, Bagamoyo
 
 
MWENYEKITI wa Kamati ya Kusaidia Timu za Vijana za Taifa Ridhwan Jakaya Kikwete, amesema mfumo wa uendeshaji soka Tanzania unahitaji mabadiliko makubwa.
 
Akifungua mkutano mkuu wa Chama cha Waandishi wa Habari za Michezo Tanzania (TASWA) uliofanyika jana mjini Bagamoyo, Kikwete alisema wakati umefika kwa viongozi wa klabu za soka kubadilisha mfumo wa uendeshaji.
 
Alisema mfumo wa kujiendesha kwa kutegemea mfuko wa mtu mmoja, haufai kuendelezwa, na kutaka klabu zitegemee michango ya wanachama ili kuzijengea msingi madhubuti.


  Ametoa mfano kwa kuukosoa mfumo wa klabu ya Yanga, ambayo alisema ili iishi imekuwa tegemezi wa fedha za kujiendesha kutoka kwa mtu mmoja, tafauti na Simba inayotegemea michango ya wanachama wake. ”Huu si utaratibu mzuri na haukubaliki katika kuendesha shughuli za soka kwamba timu ikihitaji fedha basi zitolewe katika mfuko wa mtu, ni lazima tubadilike”, alisema.
 
Kwa upande mwengine, mtoto huyo wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, aliwaasa waandishi kuacha kuandika habari kwa utashi na mapenzi yao kwa timu fulani, akisema kufanya hivyo ni kuwanyima haki wasomaji wa habari hizo. “Magazeti sio yenu bali ni ya wasomaji, tafadhali msiyatumie vibaya kwa maslahi yenu, na wala msiingize unazi wa Simba na Yanga katika kazi”, alisisitiza Kikwete.
 
Aidha, aliwataka waandishi hao kuandika habari zenye mwelekeo wa kujenga na kuelimisha jamii zaidi, ili waweze kuifikisha pazuri taaluma yao ambayo lengo lake ni kuielimisha jamii.
 
Mkutano huo ulihudhuriwa na zaidi ya wanachama wa 100 wa TASWA, ambapo ajenda mbalimbali zilijadiliwa, ikiwemo dhamira ya chama hicho kuanzisha Chama cha kuweka na kukopa (Saccos), ambayo iliridhiwa na wanachama hao.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.