Habari za Punde

Sekta binafsi iungwe mkono - Dk Shein

Na Rajab Mkasaba, Ikulu
 
RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Ali Mohamed Shein amefunga mkutano wa saba wa Baraza la Biashara Zanzibar (ZBC) na kusisitiza kuwa ipo haja ya kuungwa mkono kwa sekta binafsi ili iweze kuimarika na hatimae kuisaidia serikali pamoja na wafanyabiashara wadogo wadogo.
Mkutano huo wa siku moja ambao ulikuwa chini ya Mwenyekiti wake, Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, ulifanyika katika ukumbi wa Salama, Hoteli ya Bwawani mjini Zanzibar.
Mkutano huo ulikuwa na mada tatu zilizowasilishwa ambapo washiriki nao walipata nafasi ya kuzichangia mada hizo ikiwemo ‘Nadharia ya Viwanda na Maendeleo ya Kiuchumi’, ‘Historia ya Sekta ya Uzalishaji wa Viwanda Zanzibar’, na ‘Fursa za Maendeleo ya Viwanda kwa Zanzibar’.
Akifunga mkutano huo uliokuwa na maudhui yasemayo ‘Ubia na Uwekezaji kwa Maendeleo ya Viwanda Zanzibar’,, Dk. Shein alisema kuwa serikali ina wajibu wa kuisadia sekta binafsi ili ifanye vizuri kwa lengo la kupata uwezo na kuweza kuisaidia serikali pamoja na wafanyabiashara wadogo wadogo ili nao waweze kujimudu.
Alieleza kuwa sekta binafsi bado haina uwezo mkubwa hivyo pale wanapohitajia msada kutoka serikalini hakuna budi kusaidiwa ili kuweza kufanya kazi zao vizuri na kuisaidia serikali.
Dk. Shein alisema kuwa wawezekezaji wazalendo wapo hapa nchini na baadhi yao wameshaanza kuonesha njia ya kuimarisha sekta hiyo hivyo serikali nayo haina budi kushirikiana nao pamoja na sekta binasfi ili iweze kufanya kazi vizuri.
“Mcheza kwao hutunzwa hapigwi, hivyo nasi serikali tunawajibu wa kuwaunga mkono na kuwasaidia wenzetu wa sekta binafsi kwa lengo la kupata mafanikio zaidi katika kuimarisha uchumi wetu na kukuza maendeleo”.;alisisitiza Dk. Shein.
Aidha, Dk. Shein alisema kuwa kazi kubwa iliyopo hivi sasa ni kuanzishwa viwanda kwa vitendo sambamba na kushirikiana na kuiunga mkono sekta binafsi ili iweze kufanya kazi zake kwa ufanisi zaidi.
Alisema kuwa sekta binafsi kwa upande wa nchi jirani imeweza kufanya vizuri ikilinganishwa na Zanzibar hivyo ipo haja ya kushirikiana na kusaidiana ili na hapa Zanzibar iweze kuimarika zaidi na kuleta mafanikio makubwa.
Alitoa shukurani kwa kufanywa vizuri na mafanikio makubwa mkutano huo huku akitoa shukurani kwa watoa mada wote pamoja na sekritarieti na wajumbe na viongozi mbali mbali waliohudhuria mkutano huo kwa kutoa ufafanuzi na hatimae wajumbe kutoa michango yao.
Pamoja na hayo, Dk. Shein alieleza kuwa Serikali iko tayari kuendeleza ushirikiano na sekta binafsi kwa kutambua umuhimu wake katika kuimarisha uchumi na kukuza maendeleo ikiwa ni pamoja na kuongeza soko la ajira.
Michango mbali mbali ilitolewa na wajumbe walioshiriki mkutano huo ikiwa ni pamoja na kuiomba serikali kuendeleza wajibu wake wa kuisaidia sekta binafsi ili iweze kurejesha sekta ya viwanda nchini kwa kuzidisha ushirikiano, mawasiliano na uratibu.
Nalo Jeshi la Polisi lilieleza umuhimu wa suala la usalama katika kuendeleza viwanda nchini kama ilivyo umhimu katika kuendeleza sekta ya utalii hapa nchini
Kutokana na uwasilishwaji wa mada zilizotolewa katika mkutano huo na hatimae kutolewa michango mbali mbali kutoka kwa washiriki wa mkutano huo, ulifikia maazimio kadhaa.
Miongoni mwa maazimio hayo ni pamoja na Sekta binafsi na Sekta ya Umma zikutane katika ngazi za kisekta na baadae ziwasilishe makubaliano yao kwenye Baraza la Biasahara Zanzibar katika kutafuta ufumbuzi wa matatizo yanayokabili sekta mbali mbali.
Azimio jengine ni pamoja na kuanzisha na kuimarisha viwanda vidogo vidogo na vya kati kwa maendeleo ya Zanzibar. Pamoja na kuanzisha fursa zitakazopelekea wafanyabiashara kupata mikopo ya uwekezaji na kuanzisha Benki ya Uwekezaji Zanzibar kwa mfumo wa PPP.
Sambamba na hayo, azimio juu ya kuimarisha mfumo wa ukusanyaji wa mapato ya utalii nalo lilitolewa ikiwa ni pamoja na Wawekezaji wazalendo kupatiwa kiwango maalum (prefential rate) kitakachowasaidia katika biasahara zao.
Pia, kupatiwa nyenzo kwa vyombo vya ulinzi mfano magari, mapikipiki kwa ajili ya kufanyia kazi ili kuimarisha usalama katika sekta ya utalii.
Sheria za Manispaa na Halmashauri za Miji pamoja na sheria ya Afya ya Jamii (2012) zitekelezwe na zisimamiwe kwa mashirikiano na sekta binafsi ili miji iwe katika hali ya usafi zaidi.
Mapema Dk. Shein alitembelea mabanda ya maonyeso ya Wajasiriamali yaliokuwa yamejengwa katika viwanja vya ukumbi wa Salama, Bwawani mjini Zanzibar na kuangalia bidhaa mbali mbali zinazotengenezwa na Wajasiriamali hao na kupongeza juhudi wanazozichukua katika shughuli zao hizo.

1 comment:

  1. Hebu msituzinguwe, Baraza la biashara halina kazi hata moja linaloifanya kila kukicha mzanzibari mlalahoi anazidi kuteketea kwa kulipa kodi mara mbili (ZRB na TRA) na hilo baraza limenyamaza kimya.

    Nawakae hapo wale riziki zao wajitayarishe na majibu mbele ya ALLAH juu ya dhulna zinazofanywa hapa zanzibar.

    ReplyDelete

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.