Na Hafsa Golo
CHAMA cha CUF kimelishauri Shirika la Magazeti ya
Serikali wachapishaji wa magazeti ya Zanzibar Leo, Zanzibar Leo Jumapili na
Zaspoti kufanya kazi zake kwa kuzingatia
kuimarisha serikali ya Zanzibar iliyo katika mfumo wa umoja wa kitaifa (GNU).
Chama hicho kimelitaka gazeti hilo kuendelea kuandika
habari zinazoingatia maadili, silka, mila na desturi za Wazanzibari.
Kimesema ni fahari kwa mwananchi Zanzibar kulisoma gazeti
la Zanzibar Leo hata mbele ya watoto lakini inakuwa aibu kuyasoma magazeti
mengine mbele ya watoto hivyo kulazimu msomaji kulisomea chumbani.
Mkurugenzi wa Haki
za Binaadamu, Habari na Uenezi wa chama hicho, Salim Dimani aliyasema hayo
wakati ujumbe wa chama hicho ulipofanya ziara katika ofisi za shirika hilo,
Rahaleo mjini hapa.
Aidha alisema magazeti yanayochapishwa na shirika hilo
hasa Zanzibar Leo ndio chombo cha habari pekee kinachotegemewa na wananchi kwa
kupata habari sahihi.
Alisema gazeti hilo limekuwa likitekeleza majukumu yake
ipasavyo, hali iliyosaidia kuongeza wigo wa wasomaji wake.
Dimani alisema Wazanzibari wengi popote walipo wamekuwa
wakilitegemea gazeti hilo kupata taaluma na matukio muhimu yanayotokea Zanzibar
na duniani, hivyo aliahidi kwamba kwa kuwa CUF ina wajumbe wengi katika Baraza
la Wawakilishi, kitatumia fursa hiyo kuhakikisha shirika linapatiwa bajeti ya
kutosha pamoja na mtambo wa kuchapia.
Alisema CUF kitaendelea kulitumia gazeti la Zanzibar Leo
kutoa taarifa zao za utekelezaji wa majukumu yake kwa faida za wananchi na
kulitaka gazeti hilo kufanya haki kwa vyama vyote vya siasa nchini.
Naye Mwakilishi wa zamani, Najma Khalifan alisema CUF kipo tayari kutoa ushirikiano kwa lengo la
kujenga taswira za utendaji katika kuifikishia ujumbe jamii kwa kuwa gazeti
ndio chombo pekee ambacho kinahifadhi kumbukumbu kwa muda mrefu.
Alisema amekuwa akifahamu ugumu wa utayarishaji gazeti
hasa iwapo upatikanaji wa rasilimali zikiwemo fedha utakapokuwa haupatikani kwa
wakati.
Hata hivyo,
alilishauri gazeti hilo kuendelea kutoa taarifa za vyama vya siasa bila
ya ubaguzi.
Akizungumzia
changamoto zilizokuwepo katika shirika hilo, Mhariri Mtendaji wa Shirika
hilo, Abdulla Mohammed alisema tatizo kubwa linalowakabili ni ukosefu wa ofisi,
mtambo wa kuchapishia magazeti na uhaba wa fedha.
Alisema ukosefu wa mtambo unasababisha kuzorotesha
majukumu ipasavyo kwani hata zile fedha kidogo zinazokusanywa zimekuwa
zikitumika kulipia gharama za uchapaji Tanzania Bara.
"Suala la mtambo ni muhimu kwani ndio nyenzo mojawapo ya kurahisisha
shughuli zetu, iwapo tutapata mtambo wetu tuko tayari kuchapisha hata kurasa 40
za rangi," alisema.
No comments:
Post a Comment