Habari za Punde

Moroko amvutia Poulsen kifaa kutoka Zanzibar

 
Ni mchezaji bora ligi kuu Zanzibar 2012/13
Haruna Moshi ‘Boban’ naye arejea Tanga
Na Mwandishi Wetu, Tanga
TIMU ya Coastal Union ya Tanga, imekamilisha usajili wa wachezaji wanne wapya, akiwemo mchezaji bora wa ligi kuu ya Zanzibar msimu huu, Abdallah Othman Ally.

Ally anayecheza pembeni juu kushoto mwenye kasi na uwezo mkubwa wa kumiliki mpira, amesaini mkataba wa miaka miwili na Coastal Union ambayo tangu ipande tena ligi kuu mwaka juzi, imepania kurejesha makali yake
.

Mbali na Ally anayechezea pia timu ya taifa ya Zanzibar, Zanzibar Heroes, wagosi wa kaya pia wamemrejesha kiungo waliyemuibua mwaka 2000 kabla ya kufuata maslahi Moro United, baadaye Simba SC na Geffle FF ya Sweden, Haruna Moshi Shaaban ‘Boban’.

Boban amerejea Tanga alipoanzia kucheza soka ya ushindani mwaka 2000 chini ya kocha maarufu wa zamani, Mansour Magram (sasa marehemu), akitokea sekondari ya Makongo, Dar es Salaam.

Coastal pia imesajili wachezaji wawili kutoka JKT Oljoro ya Arusha, kipa Said Lubawa na sentahafu Marcus Ndehele na Mkurugenzi wa Ufundi wa Coastal Union, Nassor Ahmed Hussein Bin Slum amesema bado wanasaka wachezaji watano zaidi kulingana na mapendekezo ya benchi la ufundi.
“Huu si usajili wa kukurupuka, ni usajili unaotokana na mapendekezo ya benchi la ufundi la timu chini ya kocha mkuu, Hemed Suleiman ‘Morocco’. Alitaka wachezaji tisa, ambao aliwapendekeza kwa majina yeye mwenyewe. Na sisi tumekuwa tukimfuata mmoja baada ya mwingine na kumalizana naye”.

“Sasa bado tupo kwenye harakati za kumalizana na wengine watano. Lengo letu ni kuhakikisha kocha anakuwa na timu atakayoridhika nayo kulingana na mapendekezo yake, hatutaki kuingilia kusajili hata mchezaji mmoja,”alisema Bin Slum.  
Mkurugenzi huyo alisema mazoezi ya Coastal Union yataanza wiki ya kwanza ya mwezi Julai mwaka huu, nje kidogo ya mji ambako kikosi kitapiga kambi kujiandaa kikamilifu kwa ajili ya msimu mpya.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.