Habari za Punde

PBZ yatoa mabati 150 skuli ya maandalizi Gombani

Na Haji Nassor, Pemba
JUMLA ya wanafunzi 125 wa skuli ya maandalizi ya kiislamu iliopo kijiji cha Gombani shehia ya Ng’ambwa Wilaya ya Chake Chake, wanatarajia kuhamia katika skuli yao mpya wakati wowote kuanzia sasa, baada ya Benki ya Watu wa Zanzibar (PBZ) tawi la Pemba, kukabidhi mabati 150 kwa ajili ya kuezekea skuli yao.

Hayo yalifahamika jana kwenye hafla ya kukabidhi msaada huo kutoka PBZ, ambapo ulishuhudiwa na waalimu, wanafunzi, wazazi na walezi pamoja na wajumbe wa kamati ya skuli hiyo.

Akizungumza kabla ya kukabidhiwa msaada huo wenye thamani ya zaidi shilingi milioni mbili, Mwenyekiti wa Kamati ya skuli hiyo Abeid Nassor Juma, alisema msaada huo unaweza kuwaondoshea usumbufu wa makaazi vijana wao.

Alisema kwa sasa wanatumia eneo la msikiti wa Ijumaa wa Gombani, jambo ambalo huwakosesha wanafunzi hao mtiririko mzuri wa masomo yao kwa kuwa panapokuwa na shughuli husitisha masomo.

Akizungumza katika hafla hiyo, Meneja wa Benki ya Watu wa Zanzibar (PBZ) tawi la Pemba, Haji Machano, alisema PBZ inafahamu na kuelewa vyema umuhimu wa elimu na ndio maana imeamua kutoa misaada yake.

Alisema elimu ni kitu cha mwanzo alichopewa amri kiongozi wa umma wa kiislamu, hivyo inaonesha umuhimu wake kwa jamii.

Hata hivyo ameiomba Kamati ya ujenzi wa skuli hiyo, kuhakikisha msaada huo unatumika kama ulivyokusudiwa ili kuona jengo hilo linamazika na wanafunzi wanalitumia.

Nae Mwenyekiti wa ujenzi wa skuli hiyo, Hafidh Mohamed Salim aliipongeza PBZ kutokana na misaada yake ya mara kwa mara katika ujenzi huo.

Alisema PBZ imekuwa mdau mkuu wa ujenzi huo, ambapo wakati wa ujenzi katika hatua za awali, walitoa msaada wa saruji paketi 200.

Skuli hiyo ambayo ina vyumba sita vya kusomea, afisi za walimu, vyoo vinne, sehemu ya duka na jiko, hadi sasa jumla shilingi milioni 20 zimeshatumika na kwa makisio ya awali walihitaji shilingi milioni 125 hadi kumalizika.

Mwalimu Mkuu wa skuli hiyo, Fatma Hamad Seif alielezea kufurahishwa kwake na PBZ jinsi ilivyoamua kupiga jeki ujenzi wa skuli hiyo.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.