Habari za Punde

Balozi Seif akutana na Balozi mpya wa Tanzania nchini Nigeria

 Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi  akimpongeza  Balozi Mpya wa Tanzania Nchini Nigeria pamoja na Nchi nyengine 9 za Afrika Magharibi Balozi Daniel Ole Njoolay  alipozungumza naye Ofisini kwake Vuga Mjini Zanzibar.
Balozi Mpya wa Tanzania Nchini Nigeria Balozi Daniel Ole Njoolay akimuhakikishia Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif kwamba atajihidi kuiwakilisha vyema Tanzania katika utumishi wake wa Kidiplomasia.

Picha na Hassan Issa wa – OMPR – ZNZ.
 
Na Othman Khamis Ame
 
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar  Balozi Seif Ali Iddi alisema Mataifa ya Bara la Afrika yanaweza kupiga hatua kubwa na ya haraka ya maendeleo iwapo Viongozi na Wananchi wake wataamua  kushirikiana kwa dhati katika kuendeleza miradi ya pamoja ya kiuchumi.
 
Akizungumza na Balozi Mpya wa Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania Nchini Nigeria Balozi Daniel Ole Njoolay  hapo Ofisini kwake Vuga Mjini Zanzibar, Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar alisema si vyema kwa wakati huu Afrika ikaendelea kutajwa kuwa Bara linalokumbwa na  Migogoro, njaa pamoja na vita visivyokwisha.
 
Balozi Seif alisema kuaminiana pamoja na mipango bora itakayoendelezwa na Viongozi na Wataalamu wa Mataifa ya Afrika katika   kuzitumia  Mali na rasilmali zilizomo kwenye Mataifa hayo inaweza kuzipiku kimaendeleo hata baadhi ya Nchi za Ulaya zilizotangulia kiuchumi.
 
Alifahamisha kwamba Taasisi na jumuiya za Kimataifa zinaelewa mchango mkubwa uliokuwa ukitolewa na baadhi ya Viongozi wa mataifa ya Afrika. Hivyo fursa hiyo ni vyema itazingatiwa na kupewa nafasi na viongozi waliopo madarakani Barani humu katika muelekeo la kuliongezea nguvu zaidi za Kiuchumi na Kisiasa Bara hili.


“ Tulikuwa tukishuhudia Viongozi wa Tanzania na Nigeria wakihusishwa katika kusaidia utatuzi wa migogoro Barani Afrika na hata  katika baadhi ya Mataifa mengine Duniani . Rais Mstaafu wa Tanzania Mh. Benjamin Mkapa wa Tanzania na Msaafu mwenzake wa Nigeria Bw. Obasanjo walikuwa vinara wa kusimamia amani. Kwa nini tusiwatumie wengine wastaafu katika kusaidia kuimarisha ushirikiano kwenye uchumi ? “. Alisisitiza Balozi Seif.
 
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar alimpongeza Balozi huyo mpya wa Tanzania Nchini Nigeria Balozi Daniel Ole Njoolay kwa kuteuliwa kwake kushika wadhifa huo ambapo  pia ataiwakilisha Tanzania katika Mataifa Tisa ya Magharibi mwa Bara la Afrika.
 
Alimuomba Balozi huyo kuiwakilisha vyema Tanzania katika Mataifa hayo akikumbuka  kwamba Tanzania na Nigeria pamoja na Nchi nyengine za Afrika Magharibi zina uhusiano wa muda mrefu tokea mataifa ya Afrika yalipokuwa yakidai uhuru wao.
 
Balozi Seif aliitolea mfano Nigeria jinsi inavyoshirikiana na Tanzania  katika masuala ya elimu ikijitolewa kutoa walimu kadhaa wanaosaidia kufundisha katika baadhi ya vyuo vikuu pamoja na skuli za Sekondari  Nchini Tanzania.
 
“ Tunalazimika kuishukuru Serikali  ya Nigeria kwa jitihada zake za kutupatia walimu wa Skuli za Sekondari ambao wamesaidia kwa kiwango kikubwa kupunguza pengo la walimu wa fani hiyo katika skuli zetu nyingi hapa Nchini “. Alisema Balozi Seif.
 
Alimtaka Balozi wa Tanzania Nchini Nigeria  kuhakikisha kwamba uwakilishi wake kwenye Mataifa hayo ya Afrika Magharibi unaihusu vyema Jamuhuri Nzima ya Muungano wa Tanzania Bara na Zanzibar.
 
 Alisema zipo fursa nyingi za uwekezaji katika Visiwa vya  Unguja na Pemba ambazo zinaweza kutumiwa na wawekezaji wa Mataifa ya Afrika Magharibi  licha ya ardhi ndogo iliyopo lakini akitolea mfano wa  sekta za Viwanda vidogo vidogo pamoja na Hoteli za Kitalii.
 
“ Licha ya maeneo madogo ya ardhi tuliyonayo katika visiwa vyetu vya Unguja na Pemba lakini bado fursa ya uwekezaji katika maeneo ya  Hoteli na Viwanda vidogo vidogo  yanapatikana “. Alifafanua Balozi Seif.
 
Naye Balozi wa Tanzania Nchini Nigeria Balozi Daniel Ole Njoolay alimuhakikishia Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif kwamba uwakilishi wake kwenye Mataifa hayo ya Afrika ya Magharibi utazingatia pande zote mbili za Jamuhuri  ya Muungano wa Tanzania.
 
Balozi Njoolay  alimuomba Balozi Seif ambaye ni mzoefu katika masuala ya Kidiplomasia kumsaidia katika kutekeleza utumishi wake huo mpya wakati wowote atakapohitajia msaada wake .
 
 

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.