Habari za Punde

Taarifa ya Dk Shein alipozungumza na waandishi wa habari



TAARIFA YA RAIS WA ZANZIBAR NA MWENYEKITI WA

BARAZA LA MAPINDUZI, MHE. DK. ALI MOHAMED SHEIN, KWA

WAANDISHI WA HABARI, 12 NOVEMBA, 2013 IKULU, ZANZIBAR

Ndugu Waandishi wa Habari na Ndugu Wananchi,

Assalam Alaikum,

Kwa mara nyingine tena nina furaha kukukaribisheni Ikulu kwa mazungumzo ya pamoja. Nimewahi kukutana nanyi katika utaratibu wetu wa kawaida mara mbili hapa Ikulu na katika sehemu nyengine. Ingawa hatujakutana katika utaratibu wa aina hii kwa muda sasa hapa Ikulu, kutokana na kuwepo shughuli nyengine za kitaifa zilizopelekea kuzungumza na wananchi kwa jumla.  Kwa mfano sikukuu za Iddi, mkutano wa hadhara na taarifa muhimu kwa wananchi na kadhalika. Lakini leo nimeitisha mkutano huu kwa madhumuni ya kuzungumza nanyi na wananchi wote kwa jumla juu ya hali ya nchi yetu katika miaka mitatu ya Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar, Awamu ya Saba yenye muundo wa Umoja wa Kitaifa, ninayoiongoza.

Kama mnavyoelewa, niliingia madarakani kuwa Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi tarehe 3 Novemba 2010 baada ya kuapishwa rasmi kufuatia kuchaguliwa na wananchi waliowengi katika uchaguzi Mkuu uliofanyika tarehe 31 Oktoba, 2010 kwa mujibu wa Katiba ya Zanzibar ya mwaka 1984.

Mara tu baada ya kuingia madarakani nilitekeleza wajibu wa Kikatiba kwa kuwateua viongozi mbali mbali wa Serikali na kuwaapisha katika nyakati mbali mbali.


Tarehe 10 Novemba 2010 nililizindua Baraza la Wawakilishi la saba (7) ambapo niliuelezea mwelekeo wa Serikali na Mipango yake kwa kuzingatia Ilani ya Uchaguzi Mkuu wa Mwaka 2010/2015 ya CCM, MKUZA II  na Malengo ya Milenia.


Ndugu Waandishi wa Habari na Ndugu Wananchi,

Napenda nikumbushe kwamba shughuli ya Uchaguzi Mkuu na uundaji wa Serikali yenye Muundo wa Umoja wa Kitaifa zilifanyika wakati hali ya nchi ikiwa tulivu, shwari na salama na wananchi wakiwa katika hali ya mshikamano, umoja na kufahamiana. Hali hiyo iliipa sifa kubwa nchi yetu na ikaiwezesha Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar ya Awamu ya Saba kuanza kutekeleza vyema kazi zake.

Nachukua fursa hii kuwashukuru sana Makamu wangu wawili, Mheshimiwa Maalim Seif Sharif Hamad na  Mheshimiwa Balozi Seif Ali Iddi kwa jitihada na kazi zao kubwa walizozichukua  katika kipindi hiki cha miaka mitatu kwa kunisaidia katika kuiongoza Zanzibar.  Umahiri wao na uadilifu wao umesaidia sana katika kuwatumikia wananchi. Vile vile natoa shukurani kwa  Mawaziri, Naibu Mawaziri, Katibu Mkuu Kiongozi na Katibu wa Baraza la Mapindzi, Makatibu Wakuu, Naibu Makatibu Wakuu na Watendaji Wakuu wengine wote wa Idara na taasisi mbali mbali za Serikali yetu kwa kufanya kazi kwa bidii katika kuyatekeleza malengo ya Serikali. Lakini lazima niseme Juhudi za watendaji hao zimefanikiwa kutokana na kazi nzuri inayofanywa na wafanyakazi wote wa Serikali na Taasisi zote pamoja na ushirikiano mkubwa wa wananchi. Natoa pongezi na shukurani kwa wote.

MISINGI YA KIUTAWALA, AMANI NA UTULIVU

Ndugu Waandishi na Ndugu Wananchi,
Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar ya Awamu ya Saba imekuwa ikitekeleza kazi zake vizuri kwa kuzingatia Katiba na Sheria katika kuwatumikia wananchi, kama ilivyofafanua Katiba ya Zanzibar ya 1984 kifungu cha 9(2)(a) kinachoeleza nanukuu: “mamlaka ya kuendesha nchi ni ya wananchi wenyewe ambapo nguvu na uwezo wote wa Serikali kufuatana na Katiba unatoka kwa wananchi wenyewe”. Kwa hivyo, tumeingia madarakani tukiufahamu wajibu wetu wa kuwaletea maendeleo wananchi wote bila ya ubaguzi na kwamba Serikali hii inawajibika kwao.

Aidha, Kifungu cha 9(b) cha Katiba hiyo kinasema;
“Usalama na hali nzuri kwa wananchi itakuwa ndiyo lengo kubwa la Serikali” na kwa hivyo wakati wote Serikali yetu inachukua hatua madhubuti ya kuhakikisha kwamba usalama na utulivu wa nchi inakuwepo wakati wote na mshikamano na mapenzi baina ya wananchi yanaendelezwa.  Amani na utulivu ndio nguzo kubwa ya maendeleo yetu ndio maana tunapobaini kuwa usalama na utulivu, amani na mshikamano inatishiwa kuvunjwa, huwa tunachukua hatua kali kwa wanaohusika. Kwa hivyo, jambo kubwa na la msingi tunalopaswa kulienzi na kuliendeleza ni kwa bidii zetu zote ni suala zima la umoja na mshikamano wenu,

ambao ndio siri kubwa ya kuendelea na kuwepo kwa hali ya amani na utulivu yenye kuimarisha maendeleo yetu.  Katika kipindi chote cha miaka mitatu Zanzibar iko salama na wananchi tunaishi kwa salama, amani na mshikamano.  Hata hivyo, katika kipindi cha mwaka 2012 kwa nyakati tafauti tulishuhudia vitendo vya vurugu na fujo; ambavyo vilidhibitiwa na vyombo vyetu vya ulinzi na usalama.  Tutaendelea kuchuka hatua hizi wakati wote, bila ya kuwa na khofu wala woga lakini kwa kuzingatia misingi ya utawala bora.  Wito wangu kwa wananchi wote ni kuzidi kuimarisha umoja, amani na utulivu na mafanikio tuliyoyapata. 

Ndugu Waandishi na Ndugu Wananchi,
Kwa sababu tumeweza kudumisha na kuiendeleza amani na utulivu katika kipindi cha miaka mitatu, Serikali imefanikiwa kupata maendeleo makubwa katika utekelezaji wa mipango ya Serikali inayotokana na Dira ya 2020 na MKUZA  II na Ilani ya CCM ya Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2010/2015 ambayo imezingatia Katiba ya nchi yetu. Kwa mara nyengine nainukuu Katiba kifungu cha 10 kinachosema;-

“ Kwa madhumuni ya kuendeleza umoja na maendeleo ya watu na ustawi wa jamii katika nchi itakuwa ni wajibu wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar:-

a)    Kutoa huduma za kutosha kwa ajili ya kuendeleza watu katika njia za mtu kuwa huru kwenda atakapo na utoaji huduma kwa watu na kutoa haki zote za kuishi kwa Mzanzibari sehemu zote za Zanzibar.

b)   Kuondosha kabisa vitendo vya rushwa na utumiaji mbaya wa cheo dhidi ya umma kwa wale wote walio na madaraka.

c)    Kusimamia Maendeleo ya Uchumi wa Nchi kufuatana na misingi na madhumuni yaliyowekwa na Katiba na kuhakikisha upatikanaji wa huduma bora, kuwatibu na kusimamia uendeshaji wa rasilimali muhimu za nchi.

d)    Kutoa mwongozo wa kuhakikisha Maendeleo ya Uchumi yenye urari na yaliyopangika na kwamba mfano wa kiuchumi  hautafanyika katika utaratibu utakaopelekea kulimbikiza kwa utajiri na  njia za kuzalisha mali kwa watu wachache au kikundi fulani. ’’

Vifungu vyengine (e)-(i) ambavyo sikuvinukuu hapa ni sehemu ya kifungu cha 10.

Ndugu Waandishi wa Habari  na Ndugu Wananchi,
Napenda nichukue fursa hii kuelezea baadhi ya mafanikio tuliyoyapata katika sekta za uchumi, huduma za jamii, miundombinu, utawala bora na  nyinginezo kwa maendeleo  ya nchi yetu.

                                                            UCHUMI
Wakati tunaadhimisha miaka mitatu ya Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar, Awamu ya Saba, ni faraja na  fahari kwetu kuona kuwa  utekelezaji wa Ilani ya CCM ya Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2010/2015 na mipango mikuu ya Serikali katika kukuza uchumi unakwenda kwa mujibu wa matarajio na mipango yetu. Juhudi kubwa zinazochukuliwa na Serikali katika kuimarisha ukusanyaji wa mapato, uwezeshaji, na ushirikishaji wa wananchi katika harakati za kujenga uchumi wetu zimekuwa zikizaa matunda mazuri.

Ukusanyaji wa mapato ya ndani umekuwa ukiongezeka mwaka hadi mwaka. Katika mwaka 2010/2011 tulikusanya Tsh. 181.4 bilioni, mwaka 2011/2012 tulikusanya Tsh. 212 bilioni na katika mwaka 2012/103 ukusanyaji ulikuwa Tsh. 266.2 bilioni.  Juhudi za kuimarisha Bodi ya Mapato ya Zanzibar (ZRB) zinaendelezwa pamoja na kuimarisha mashirikiano na Mamlaka ya  Mapato Tanzania (TRA).

Uchumi wetu umekuwa ukikua kila mwaka. Ulikua kwa asilimia 6.4 katika mwaka 2010 ulifikia asilimia 6.7 katika mwaka 2011 na ulifikia asilimia 7.0 katika mwaka 2012 na tunatarajia kwa mwaka 2013 utafikia asilimia 7.5.

Ndugu Waandishi wa Habari na Ndugu Wananchi,
Itakumbukwa kuwa wakati tunaingia madarakani, pato la Mtu Binafsi lilikuwa ni Tsh. 726,000 na maelekezo ya Ilani ya CCM ya Uchaguzi Mkuu wa Mwaka 2010 yalilenga Pato la Mtu Binafsi lifikie Tsh. 884,000 ifikapo mwaka 2015.

Jitihada za Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar zimefanikiwa kuliongeza Pato la Mtu Binafsi  kutoka Tsh. 726,000 mwaka 2010 hadi kufikia Tsh. 960,000 mwaka 2011 ambazo ni sawa na Dola za Kimarekani 611 kutoka Dola 560, mwaka 2010. Katika mwaka 2012, Pato la Mtu Binafsi liliongezeka na kufikia Tsh. 1,003,000 sawa na dola za Kimarekani 638.

Huduma za benki zimeendelea  kuimarishwa ili  kutoa huduma nzuri kwa sekta binafsi ili nazo zitoe mchango mkubwa katika kukuza uchumi na soko la ajira nchini. Mikopo ya Benki kwa sekta binafsi iliongezeka kutoka Tsh.147.5 bilioni mwezi Septemba 2011 hadi kufikia Tsh. 150.9 bilioni mwezi wa Septemba 2012. Taasisi za kifedha zinaendelea kuimarika kutoka asilimia 4.0 mwaka 2011 hadi kufikia asilimia 10.2 mwaka 2012.

Licha ya mafanikio hayo tuliyoyapata hata hivyo, bado mfumko wa bei umekuwa ukitupa changamoto kadhaa na mwaka 2011, ambapo ulifika asilimia 14.7. Jitihada mbali mbali zimechukuliwa katika kukabiliana na hali hiyo ikiwa ni pamoja na kuimarisha shughuli za kilimo, kuwapunguzia wananchi ushuru katika baadhi ya bidhaa muhimu na kushajihisha uwekezaji. Mwaka 2012 mfumko wa bei ulishuka na kufikia asilimia 9.4 na hivi sasa umefikia asilimia 4.4.
  

BIASHARA NA VIWANDA
Ndugu Waandishi wa Habari na Ndugu Wananchi,
Kutokana na kuwepo kwa mazingira mazuri ya biashara nchini, biashara ya usafirishaji na uingizaji wa bidhaa umeweza kuimarika ambapo usafirishaji  hasa wa karafuu na mwani umeongezeka kutoka Tsh. 17,907.0 milioni mwaka 2010 hadi Tsh. 67,390.5 milioni mwaka 2012, ongezeko la  asilimia 276.3. Bidhaa zenye thamani ya Tsh. 271,273.1 milioni zimeagiziwa, mwaka 2012 kutoka Tsh. 129,137 milioni mwaka 2010.

Serikali imeweza kusimamia upandaji wa bei holela kwa bidhaa muhimu kama Mchele, Sukari na Unga wa ngano kwa kuunda  kanuni maalum za uagiziaji na kusimamia mwenendo wa biashara ambapo hivi sasa bei zinapangwa kwa mashirikiano ya pamoja baina ya serikali na wafanyabiashara wa ngazi zote.  Serikali imetoa ruhusa kwa wanaotaka kuagizia bidhaa hizo muhimu hapa Zanzibar, waagizie kwa mujibu wa taratibu zilizowekwa. Wananchi wanaombwa kuondokana na dhana kuwa kuna wafanyabiashara wachache ndio waliopewa vibali vya kuagizia bidhaa za namna hiyo.

Tarehe 21 Agosti, 2011 Serikali imelifanyia mageuzi makubwa ya shirika la ZSTC na tayari imeshapitisha sheria mpya ya ZSTC yenye lengo la kuweka muundo mpya wa shirika hilo kwa lengo la kupunguza gharama za uendeshaji, na kuweka majukumu mapya. Kwa upande wa biashara ya karafuu, Serikali inatekeleza mpango wa kuweka Utambulisho wa Karafuu ya Zanzibar (Branding) ili iweze kutambulika kimataifa na kupata hadhi na bei zaidi katika masoko ya dunia.

Ndugu Waandishi wa Habari na Ndugu Wananchi,
Katika kuimarisha mazingira ya biashara na viwanda nchini, Serikali imeamua kuifanya Zanzibar kuwa Eneo Tengefu la Kiuchumi (SEZ) ndani ya Jumuiya ya Afrika Mashariki.  Taasisi ya Viwango Zanzibar (ZBS) imeanzishwa, ili kusimamia ubora na kuweka viwango vya bidhaa zinazozalishwa na zinazoingizwa nchini.

Jitihada za kuvifufua na kuvikuza  viwanda hapa nchini zinaendelezwa, na katika kipindi cha 2011/12 jumla ya miradi tisa ya viwanda yenye jumla ya mitaji ya dola za Kimarekani 7.5 milioni iliidhinishwa na Mamlaka ya Vitega uchumi ( ZIPA). Mchango wa sekta hii bado ni mdogo katika Pato la Taifa, hata hivyo ukuaji wake umekuwa  ukiongezeka mwaka hadi mwaka.

Hivi karibuni ujenzi wa kiwanda kikubwa cha maziwa cha Azam Diary factory katika eneo la Fumba, Unguja umeanza kiwanda hicho kitasarifu bidhaa za maziwa na kinatarajiwa kuajiri zaidi ya wafanyakazi 200. Aidha, kiwanda cha Sukari cha Mahonda kinaendelea kufufuliwa na wafanyakazi 350 wamepatiwa ajira.

Serikali imekuwa ikishajihisha ushiriki wa Sekta binafsi kuekeza katika viwanda kwa njia mbali mbali ikiwemo kupitia mikutano ya Baraza la Biashara la Zanzibar.
UWEZESHAJI KIUCHUMI.
Ndugu Waandishi wa Habari na Ndugu Wananchi,
Katika azma ya kuendelea kuwawezesha wananchi kiuchumi na kuyashughulikia kwa ufanisi mkubwa masuali ya kazi na ajira hivi karibuni nilianzisha Wizara ya Uwezeshaji, Ustawi wa Jamii, Vijana, Wanawake na Watoto na Wizara ya Nchi (OR) Kazi na Utumishi wa Umma.

Serikali ya Awamu ya Saba imekuwa ikitekeleza vizuri  mikakati mbali mbali inayohakikisha vijana na kinamama wanajengewa uwezo wa kujiajiri kwa kwa kujiimarisha kwenye vikundi vya ushirika na SACCOS. Serikali imekuwa ikitoa mikopo yenye jumla ya Tsh. 156 milioni

zilikopeshwa kwa wananchi wapatao 212 kupitia Mfuko wa Kujitegemea Unguja na Pemba. Kutokana na Mfuko wa JK/AK jumla ya Tsh. Bilioni 1.5 zimekopeshwa kwa wananchi mbali mbali.  Vikundi 11 vyenye wanachama 1,526 vimeanzishwa Unguja na Pemba. Jumla ya vikundi 789 wamepatiwa mafunzo ya kitaalamu kwa kupitia program ya ASSP katika Wilaya zote.  Aidha, vikundi vya vijana 58  vimepewa Tsh. 192.4 milioni kupitia mfuko wa vijana wenye thamani ya Tsh. 300 milioni.  Vile vile, Serikali imeanzisha mfuko wa Zaka ambapo vikundi 142 kutoka Unguja vilipatiwa jumla ya Tsh. 196.3 milioni na vikundi 57 kutoka Pemba vilipatiwa jumla ya Tsh. 104.2 milioni. Jitihada zipo katika hatua za mwisho za kuuzindua mfuko wa uwezeshaji nchini, uliowekewa lengo la kuwasaidia vijana na watu wengine kwenye jamii.

Kwa upande wa ajira za Serikalini, katika kipindi cha mwaka wa fedha 2012/2013 Serikali iliidhinisha fursa za ajira mpya 2,552 na  hadi kufikia mwezi Juni, 2013 Serikali imeweza kutoa ajira zipatazo 2,934 na kwa mwaka wa fedha 2013/2014 Serikali imelenga kutoa ajira 2,464.  Kadhalika, ajira kadhaa zimeweza kupatikana kutoka kwenye sekta binfasi.


U T A L I I

Ndugu Waandishi wa Habari na Ndugu Wananchi,
Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar, Awamu ya Saba, iliingia madarakani ikiwa na dhamira ya kubwa ya kuiimarisha sekta ya Utalii. Katika hotuba niliyoitoa   kwenye uzinduzi wa Baraza la Nane la Wawakilishi nililezea juu ya lengo letu la kuibadilisha sura ya sekta ya utalii ili iwe na mchango mkubwa zaidi katika uchumi wetu ikiwa ni sekta kiongozi kwa kuzingatia MKUZA II.  Nilibainisha nia yetu ya kuufanya utalii kuwa ni kichocheo cha sekta nyengine ikiwemo kilimo, ufugaji, uvuvi, usafiri wa anga na baharini pamoja na shughuli za ujasiriamali.  Katika kutekeleza dhamira hiyo tarehe 16 Oktoba, 2011 niliitangaza dhana ya ‘Utalii kwa Wote’ katika Mkutano wa Sita wa Baraza la Biashara la Zanzibar katika Hoteli ya Bwawani. Kamati za Utalii kwa wote za Wilaya za Unguja na Pemba tayari zimeundwa ili kuziimarisha huduma za utalii kwenye Wilaya, na kuwahamasisha wananchi kuendeleza miradi ya uzalishaji mali, hususan kilimo cha mboga mboga, matunda, biashara ndogo ndogo na kadhalika.

Chuo cha Maendeleo ya Utalii kilichoko Maruhubi  kinaimarishwa ili kitekeleze kwa ufanisi zaidi lengo la kujenga rasilmali watu wenye ujuzi, utaalamu na stadi  zinazohitajika. Lengo letu ni kukifanya chuo hicho kiendelee kutoa mafunzo ya utalii unaotilia maanani, mila, utamaduni na desturi zetu pamoja na hifadhi ya mazingira. Hivi sasa Serikali ishachukua hatua ya kuibua maeneo mapya ya vivutio vya utalii yakiwemo mapango, michezo ya asili, matamasha, maeneo ya hifadhi ya wanyama.  Hatua zinachukuliwa za kuimarisha utalii wa kumbukumbu za kihistoria kwa maeneo mbali mbali ya Unguja na Pemba, kuimarisha utalii wa kiutamaduni na kuuendeleza utalii wa ndani wenye kuyatunza mazingira.  Serikali imeamua kukiunganisha chuo hichi kwenye uongozi wa SUZA hapo baadae ili kitoe elimu ya juu kwenye fani ya Utalii.

Ndugu Waandishi wa Habari na Ndugu Wananchi,
Vile vile, Serikali inaendelea kushirikiana na taasisi binafsi ikiwemo Jumuiya ya ZATI na ZATO katika kuuimarisha utalii na kuitangaza Zanzibar kiutalii nje ya nchi kwa njia mbali mbali.  Hoteli za kisasa zinaendelea kujengwa na wawekezaji mbali mbali wa ndani na nje ya nchi.  Jitihada za kuchukua hatua za kuzipanga hoteli katika madaraja yake zimeanza kuchukuliwa kwa lengo la kuimarisha huduma, gharama na mapato ya Serikali.

Juhudi  za pamoja zinazochukuliwa na Serikali na Sekta Binafsi zimepelekea kuongezeka kwa idadi ya watalii wanaokuja kututembelea. Katika mwaka 2011 tulipokea watalii wapatao 175,067 na watalii 169,223 walifika nchini katika mwaka 2012. Idadi ya wageni tulipokea kila mwaka kwa miaka miwili iliyopita ni kubwa zaidi ikilinganishwa na idadi ya kila mwaka kwa miaka kabla ya 2011. Matarajio yetu ni kupata idadi kubwa zaidi ya wageni katika mwaka huu na hapo baadae kwa kuwashajiisha wawekezaji wa Turkey, nchi za Falme za Kiarabu, China na kadhalika.

MIUNDOMBINU NA MAWASILIANO

Ndugu Waandishi wa Habari na Ndugu Wananchi,
Serikali imeweza kutekeleza vyema Ilani ya CCM ya mwaka 2010/2015, Dira 2020 na MKUZA II katika sekta ya miundombinu kwa kuzijenga barabara mpya tulizoziahidi na kuzifanyia matengenezo makubwa barabara mbali mbali za mijini na mashamba, Unguja na Pemba.

Ujenzi wa barabara ya Gando-Wete, Konde-Wete bado unaendelea na tunatarajia utakamilika baadae mwaka huu au mapema mwakani.  Barabara za Kaskazini Pemba zinazojengwa kwa msaada wa MCC ambazo ni Bahanasa-Mtambwe, Mzambarautakao-Pandani-Finya, Mzambarau Karima-Mapofu, Chwale-Kojani na Kipangani-Kangagani, zenye urefu wa km. 35; nazo tunarajia kukamilika mwaka huu.  Ujenzi wa barabara mpya ya Jendele-Cheju hadi Unguja Ukuu Kae Bona, tayari umeanza na ile ya Jumbi-Koani karibu itaanza.
Vile vile, serikali imefanya jitihada za kuziimarisha huduma za bandari nchini na kwa kushirikiana na Kampuni ya Azam Marine imejenga upya majengo ya kuwahudumia abiria katika bandari ya Malindi. Upembuzi yakinifu umeshafanyika kwa ajili ya ujenzi wa bandari mpya ya Mpigaduri na bandari ya Mkokotoni Unguja.
Serikali imeshughulikia vizuri ujenzi wa jengo jipya la abiria katika uwanja ndege wa Kimataifa wa Abeid Amani Karume ambao umefikia hatua nzuri licha ya kujitokeza matatizo ya kiufundi ambayo tayari yamesawazishwa. Ujenzi huo unatarajiwa kukamilika mwishoni mwa 2014.  Ujenzi wa eneo la kuegesha ndege (apron) na ujenzi wa barabara mpya ya kupitia ndege (taxiway) nao unatarajiwa kukamilika hivi karibuni.
Ndani ya kipindi hiki cha miaka mitatu, Mamlaka ya Viwanja vya Ndege ilianzishwa na imefanya marekebisho mbali mbali katika jengo la abiria na eneo la Uwanja wa Ndege wa Abeid Amani Karume.  Utoaji  wa huduma katika viwanja vya Unguja na Pemba umeimarishwa na vifaa mbali mbali vya kuimarisha ulinzi na usalama zikiwemo mashine za uchunguzi na vifaa vya zimamoto vimewekwa.
Ndugu Waandishi wa Habari na Ndugu Wananchi,
Serikali imezingatia umuhimu wa kuziimarisha huduma za usafiri wa baharini kwa kulifanyia mabadiliko makubwa ili liweze kujiendesha kwa faida na kuwahudumia wananchi kwa ufanisi zaidi. Katika kutekeleza azma hii, Serikali ilifanya uamuzi wa kununua meli mpya.  Hivi sasa, Serikali imeshafunga mkataba na Kampuni ya Korea ya Kusini na tayari ujenzi wa meli hio umenza ambayo itakuwa na uwezo wa kuchukuwa abiria 1,200 na mizigo tani 200. Meli hiyo inategemewa kufika nchini mwezi Juni, 2015 na kusafirisha abiria na mizigo katika bandari za Unguja Pemba, Tanga na Da es Salaam.
Vile vile, matayarisho ya kutaka kununua  meli mpya ya mafuta yenye uwezo wa kuchukua tani 3,500 tayari yameanza.  Mkataba wa makubaliano unategemewa kufungwa kabla ya kumalizika mwaka huu na meli hio inategemewa kujengwa kwa muda wa miezi 18 baada ya kufungwa mkataba na inatarajiwa kufika nchini mwezi wa Juni hadi Agosti 2015.
Serikali inaendelea na hatua ya kusimamia taasisi zote zinazotoa huduma za mawasiliano ya simu kwa kupunguza idadi ya minara ya mawasiliano kwa Unguja na Pemba.  Aidha, Serikali inasimamia mradi mkubwa wa mawasiliano ya “e- government” ambao unatekelezwa kwa awamu mbili.
Tayari taasisi nne zinatumia mtandao huo zikiwemo Bodi ya Mapato, Wizara ya Fedha, Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Amali na kituo maalum cha mawasiliano hayo.
UMEME
Ndugu waandishi wa Habari na Ndugu Wananchi,
Ilani ya Uchaguzi ya Chama cha Mapinduzi, imeitaka Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar kuimarisha upatikanaji wa huduma za nishati ya umeme. Mradi  wa  ujenzi  wa  njia  ya  pili  ya  umeme  kwa ajili ya Kisiwa cha Unguja  wenye Megawati 100 uliojengwa kwa msaada wa Serikali ya Marekani kupitia Shirika la MCC, umekamilika kwa  wakati   na ulizinduliwa  rasmi  tarehe  10 Aprili 2013.  Kadhalika, mradi wa usambazaji wa umeme ulizinduliwa tarehe 11 Juni, 2013 ambao ulifadhiliwa na Serikali ya Japan. Mradi huo wa uimarishaji wa  njia  na  miundombinu  ya  umeme umejumuisha  ujenzi  wa  njia  za  kusambaza  umeme kuanzia  Mtoni hadi Tunguu, Mtoni  hadi Fumba  na  Mtoni hadi  Mahonda pamoja na Ujenzi  wa  Vituo  vya  kusambaza  umeme  huko  Mtoni, Welezo  na  Mwanyanya.
 
Katika juhudi za Serikali za kusambaza huduma za umeme kwa wananchi,  jumla  ya  Vijiji 110  vimefanikiwa  kusambaziwa  umeme  katika  miaka  mitatu,  kuanzia 2011 hadi 2013. Kati  ya  vijiji  hivyo, vijiji  65 vipo Unguja na vijiji 45 Pemba.  Mradi  wa  Usambazaji Umeme  Vijijini   hadi  sasa  umefikia  asilimia 87.5  ya vijiji vyote vya Unguja  na  Pemba.
Serikali  imechukua  juhudi  kubwa  za  kufanikisha  mpango  wa  upatikanaji  wa umeme  mbadala na inaendelea kupata mashirikiano mazuri na Jumuiya ya nchi za Ulaya katika  kutafuta  njia  mbadala  itakayofaa  ya  kuzalisha  umeme  kwa  njia  ya  Upepo  au  Jua.  Mtaalamu  tayari  ameteuliwa  na  yupo  hapa  nchini kwa maandalizi ya kufanyika  uchambuzi yakinifu.
ARDHI
Ndugu waandishi wa Habari na Ndugu Wananchi,
Kuhusu suala zima la matumizi endelevu ya ardhi,Serikali imeanzisha Idara ya Mipango Miji na Vijiji na kazi yake kubwa ni kufanya mabadilko makubwa katika sekta ya ardhi (Land Reform).
Idara imeshapitia Mpango Mkuu wa matumizi ya ardhi wa mwaka 1995 na imeandaa Mpango Mkuu wa Taifa wa Matumizi ya Ardhi (National Land Use, 2013) ambao utawasilishwa Serikalini kabla ya mwezi wa Disemba 2013.  Vile vile, mipango ya matumzi ya ardhi kimikoa imetayarishwa.
Kazi ya kutengeneza “Zanzibar Town Master Plan” imeanza rasmi tarehe 2/5/2013 na itamalizika Julai 2014 na  kazi za Mikoa ya Unguja na Pemba nazo zimeanza na ile mipango midogo midogo ya vijiji inaendelezwa. Matumizi ya ardhi ya kijiji cha Nungwi tayari umefikia hatua za mwisho na utakuwa tayari mwisho wa mwaka huu wa 2013.
Ndugu Wananchi na Ndugu Waandishi wa Habari,
Serikali inaendelea na juhudi za  kuweka mkakati wa matumizi ya Ardhi (National Spatial Developement Strategy) kwa kutambua  kuwa udogo wa ardhi ya Zanzibar, ifikapo 2014 na migongano ya kisekta katika kutumia ardhi.  Maeneo yote muhimu na matumizi yake yatapangwa katika mkakati huu.
Ndugu Wananchi na Ndugu Waandishi wa Habari,
Serikali itatoa kipaumbele katika kufanya tafiti kwa ajili ya kuandaa makaazi bora na kuhimiza ujenzi wa nyumba za ghorofa. Utafiti wa ujenzi mpya wa eneo la N’gambo na ujenzi wa nyumba za ghorofa Ng’ambo utaanza mwezi wa Novemba (Novemba 2013).  Lengo ni kufikia azma ya Serikali ya awamu ya Saba kuhakisha kuwa Wazanzibari wanapata makaazi bora.
Kuhusu viwanja kwa ajili ya ujenzi, jumla ya viwanja 1393 vimegaiwa  kutoka 2010 hadi Septemba 2013 kwa ajili ya ujenzi wa aina mbali mbali.
MAJI
Ndugu Waandishi wa Habari na ndugu Wananchi,
Kwa miaka mitatu Serikali imezingatia umuhimu wa huduma ya uhakika ya maji. katika Vijiji mbali mbali unguja na Pemba. Usambazaji wa maji safi na usafi wa Mazingira unafanywa kwa kupitia Mradi wa Maji na Mazingira unaofadhiliwa kwa pamoja kati ya Benki ya Maendeleo ya Afrika (AfDB), Shirika la Kimataifa la Makaazi (UN-Habitat), Serikali na Jamii. Mradi huu utahusisha kuchimba visima, kujenga matangi, kulaza mabomba, kujenga vyoo maskulini pamoja na kuimarisha vianzio vya maji.
Katika kutekeleza mradi huo Serikali inaendeleza kazi za ujenzi wa miundo mbinu ya maji katika Miji mitatu ya Pemba na Vijijini Unguja na Pemba, sambamba na ujenzi wa matangi ya majaribio ya uvunaji wa maji ya mvua.
Kupitia Programu hii, Serikali imekamilisha Mradi wa maji Mkoa wa Mjini Magharibi awamu ya pili chini kwa ufadhili wa Serikali ya Japan kwa kujenga matangi makubwa mawili, uchimbaji wa visima vitano pamoja na ulazaji wa mabomba yenye urefu wa kilomita 21.
Kuhusu Mradi wa Upatikanaji wa Maji na Usafi unaoendeshwa kwa mkopo wa Benki ya Maendeleo ya Afrika, kwa upande wa Unguja vijijini ujenzi wa  matangi ya Matemwe na Nungwi na unaendelea yamekamilika na kazi bado inaendelea na kwa upande wa Pemba vijijini kazi za Mradi zimekamika kwa asilimia 87.64 na utekelezaji halisi umefikia asilimia 66.80.
Kwa upande wa Pemba Mijini ujenzi umefikia asilimia 54.17 na utekelezaji halisi umefikia 20.12 na visima vyote 10 tayari vimechimbwa na uchunguzi wa maji umeanza kufanyika kwa miji yote mitatu ya Pemba. Kadhalika, kazi za uchimbaji msingi na ufungaji mabomba kwa maeneo yote
ya Miji ya Wete, Chake Chake na Mkoani tayari zimefanyika kwa masafa ya km 12 kati ya 62.50 za mabomba kwa maeneo yote.
Katika kuimarisha huduma za maji, Serikali ya Ras Al Khaimah inaisaidia Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar kwa kuchimba visima vya maji 50 kwenye maeneo mbali mbali ya Unguja na Pemba.  Visima hivi tayari vimeanza kuchimbwa kwenye maeneo mbali mbali. Jumla ya visima 21 kati ya 50 vilikuwa vimeshachimbwa katika maeneo 14 ya Mkoa wa Mjini Magharibi na maeneo 5 ya Mkoa wa Kusini Unguja.
Pamoja na juhudi kubwa ambazo Serikali tunazichukua ili kuziimarisha huduma za kupatikana maji safi na salama lakini sekta ya maji inakabiliwa na changamoto ya upungufu wa maji chini ya ardhi na kwenye chemchem zetu. Nimeshuhudia mwenyewe kwenye ziara yangu niliyoifanya kwenye vianzio vya maji Welezo, Saateni na Mwanyanya na maeneo mengine.
Hali ya uzalishaji wa chemchem karibu zote ikiwemo Mwanyanya na Mtopepo katika Mkoa wa Mjini Magharibi siyo nzuri sana. Mkoa wa Mjini Magharibi wanahudumiwa na visima 60 na chemchem 2. Kati ya visima hivyo, jumla ya visima 26 vipo wilaya ya Mjini na visima 34 vipo wilaya ya Magharibi. Upatikanaji wa maji kutoka katika chemchem za Mtoni na Mwanyanya zinazopeleka maji Mji Mkongwe, ambayo ilikuwa ni zaidi ya 30% ya mahitaji ya Mkoa. Lakini kiwango cha kupatikana maji kimepungua kwa asilimia chini ya 15.  Tatizo kubwa lililopelekea kupungua kiwango cha maji ni uharibifu wa mazingira, ukataji wa miti kwenye maeneo hayo, wananchi kuyavamia maeneo hayo na kujenga kwenye  vyanzo vya maji au kwenye uoto wa asili.  Vile vile, kutokuwepo vivuli vya asili na mabadiliko ya tabia nchi, kunapelekea maji kukauka.  Nawanasihi wananchi wasiyaharibu mazingira na wasiyavamie maeneo ya vyanzo vya maji, seuze kujenga kwenye maeneo hayo.
KILIMO
Ndugu Waandishi wa Habari na ndugu Wanachi,
Dhamira ya kuleta Mapinduzi ya Kilimo imeelezwa  wazi wazi katika Ilani ya Uchaguzi ya Chama cha Mapinduzi  ya 2010-2015, MKUZA II na inasimamiwa na Mipango mingine ya Serikali, Wizara za Kilimo na Maliasili. Dhamira  hiyo imeanza kutafsiriwa kwa vitendo katika  utekelezaji wa kazi za Wizara hizo tangu mwaka wa kwanza wa Awamu ya Saba ya uongozi wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar, ambapo matumizi ya teknolojia na zana za kisasa za kilimo yalianza kuonekana tangu msimu wa kilimo wa mwaka 2011/2012.
Kuanzia  msimu wa kilimo wa mwaka 2011, Serikali iliongeza idadi ya matrekta kutoka 27 yaliyokuwepo kabla, hadi kufikia matrekta 37.  Matrekta mengine 20 yatanunuliwa katika msimu wa kilimo wa 2013/14.  Kadhalika, Serikali ilinunua mashine 14 mpya za kisasa za kuvunia mpunga ambazo awali hazikuwepo. Vile vile, Serikali imekusudia kuagiza zana za kupandia mpunga (Planters) 30 mwanzoni mwa msimu huu wa kilimo ili kuwarahisishia wakulima kazi za kupanda mpunga na kuondokana na upandaji wa kizamani unaopelekea mavuno kuwa kidogo.
Katika kuziendeleza juhudi zetu za kutoa taaluma bora ya kilimo cha kisasa kwa wakulima nchini,  Serikali imeanzisha Skuli za Wakulima mashambani zipatazo 1,200 Unguja na Pemba zenye kuhudumia takriban kaya 24,000. Matokeo ya skuli hizi za wakulima ni ongezeko la tija na uzalishaji wa kupiga mfano katika mazao mbali mbali ya kilimo.
Katika kuyatekeleza malengo ya Mapinduzi ya Kilimo, Serikali imekiimarisha chuo cha kilimo cha Kizimbani kwa kuanzisha masomo katika kiwango cha Diploma badala ya kuishia na masomo ya kiwango cha cheti yaliyokuwa yakitolewa kabla ya 2010. Dakhalia mpya yenye uwezo wa kuchukua wananfunzi 500 imejengwa na Serikali imeamua kukiunganisha chuo hiki katika orodha ya vyuo vya SUZA hapo baadae, ili kutoa taaluma ya kilimo iliyobora zaidi nchini. Kiasi ya wanafuzi 354 wameshahitimu masomo yao kuanzia mwaka 2010 hadi sasa.  Katika kipindi cha miaka mitatu 2011/2013, Wizara ya Kilimo imeajiri mabibi na mabwanashamba 139 wenye kiwango cha cheti cha Kilimo na Mifugo kinachotolewa na Chuo cha Kilimo Kizimbani.
Ndugu Waandishi wa Habari na Ndugu Wananchi,
Katika kukiendeleza kilimo kinachozingatia miongozo ya tafiti mbali mbali, Serikali inaendelea na juhudi za  kuiimarisha Taasisi ya Utafiti ya Kizimbani  imeimarishwa ili kiweze kufanya tafiti za  kilimo na mbegu bora za mazao mbali mbali.  Idadi ya wataalamu wa utafiti nayo imeongezeka kwa kusomesha wafanyakazi 15. Kati ya hao wataalamu 10 wamepata mafunzo ya  shahada ya pili na 5 shahada ya kwanza. Vile vile, maabara mpya ya utafiti wa mazao imejengwa kwa kushirikiana na COSTECH kwa lengo la  kufanya utafiti kwa njia za kisasa.
Juhudi za kutoa mafunzo kwa wakulima zimewasaidia sana wakulima wengi na takwimu za Wizara ya Kilimo na Maliasili zinaonesha ongezeko kubwa la matumizi ya pembejeo za kilimo kuanzia mwaka 2010 hadi mwaka 2013. Kadhalika,  uagiziaji wa mbegu za aina mbali mbali umeongezeka kutoka tani 55 mwaka 2010 hadi tani 620 mwaka 2013. Mbolea kutoka tani 130 hadi tani 1,500  na dawa za kuulia magugu kutoka lita 12,000 hadi kufikia lita 30,000.
Ndugu Waandishi wa Habari na Ndugu Wananchi,
Katika kipindi cha miaka mitatu, Serikali kwa mafanikio makubwa  imetekeleza sera na program mbali mbali za kilimo  zikiwemo kukamilisha Sheria ya uhakika wa chakula na lishe, na  Sera ya Masoko. Juhudi  zinaendelea kuchukuliwa kwa kuhakikisha kuwa hekta 8,521 kwa ajili ya kilimo cha umwagiliaji maji zinatumika kama ilivyopangwa. Kati ya hekta 750 tayari zishatayarishwa na Serikali ya Jamhuri ya Korea itaziendeleza hekta 2,200 katika mabonde ya Cheju, Kibokwa na Kilombero kwa Unguja na Makwararani na Mlemela kwa upande wa Pemba.
UVUVI NA MIFUGO
Ndugu Waandishi wa Habari na Ndugu Wananchi,
Katika kipindi cha miaka mitatu (3) iliyopita, juhudi mbali mbali zimechukuliwa katika kuiendeleza sekta ya uvuvi, ambayo mchango wake katika Pato la Taifa umepanda kutoka asilimia 6.1 mwaka 2011 hadi asilimia 6.7 mwaka 2012.  Kadhalika, kiwango cha samaki kilichovuliwa kimeongezeka kutoka wastani wa tani 26,600 mwaka 2010/2011 hadi wastani wa tani 30,500 mwaka 2012/2013.  Uzalishaji wa mwani nao uliongezeka kutoka tani 12,500 mwaka 2010/2011 hadi kufikia tani 13,844 mwaka 2012/2013. Serikali ilifanya juhudi maalum yan kuwawezesha wavuvu kwa kuwapa mafunzo ya uvuvi bora unaozingatia uhifadhi wa mazingira pamoja na matumizi bora ya vifaa vya kisasa kupitia Mradi wa MACEMP, ambapo jumla ya Tsh. 4.86 bilioni zilitumika.
Kuhusu sekta ya ufugaji, Serikali imeandaa sera ya ufugaji katika kipindi hiki cha miaka mitatu na imeendeleza juhudi za kuwaendeleza wafugaji kupitia program mbali mbali na program ya kuimarisha huduma za mifugo (ASDP-L).  Jumla ya vikundi 335 vya Unguja na Pemba vilipewa mafunzo.  Wafugaji 3,200 walitembelwa na kupewa ushauri.  Vile vile, huduma za utafiti na utibabu wa wanyama ziliimarisha na matengenezo ya Maabara ya Maruhubi na Chake Chake yalifanyika.
Kwa upande wa  Mapinduzi ya Uvuvi tumefanya jitihada maalum kwenda kujifunza kutokana na uzoefu wa wenzetu nchi za nje kama vile China na Vietnam. Wavuvi na wakulima wa mwani 59 wamepelekwa nchini China kujifunza. Viongozi mbali mbali walifanya ziara ya kujifunza mambo ya uvuvi nchini China na Vietnam.
Katika kutekeleza dhamira yetu ya kuimarisha taaluma ya ufugaji wa samaki, tumeanzisha bwawa la mfano la kujifunza kufuga samaki Jozani na jengine litaanzishwa Donge hivi karibuni. Hivi sasa, shughuli za ufugaji wa samaki zinaendelea katika maeneo mbali mbali Pemba na zimeonesha mafanikio makubwa katika vijiji vya Muambe, Chambani, Pujini Kibaridi, Jadida, Kiungoni Wete, Makombeni, Chokocho na maeneo mengine.
Katika juhudi za  kuimarisha uvuvi wa bahari kuu, Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar imetia saini Maelewano ya Awali (MoU) na Serikali ya Jamhuri ya Watu wa China katika masuali ya kuendeleza uvuvi.
 ELIMU
Ndugu Waandishi wa Habari na Ndugu Wananchi,
Ni dhahiri kuwa maendeleo ya nchi yoyote yanategemea kuwepo kwa fursa na elimu bora wanayoipata wananchi wake. Kwa mantiki hiyo Serikali ya Mapinduzi ya Awamu ya Saba imechukua jitihada kubwa kuimarisha sekta ya elimu kwa maendeleo ya nchi yetu na mafanikio ya kuridhisha yamepatikana katika elimu ya maandalizi, msingi, sekondari pamoja na utoaji wa elimu mbadala, mafunzo ya ualimu, elimu ya ufundi na mafunzo ya amali pamoja na fursa za elimu ya juu kwa wanafunzi wa Zanzibar.
Idadi ya skuli za Maandalizi zimeongezeka kutoka 238 zenye wanafunzi 1641 mwaka 2010 hadi skuli 278 zenye wanafunzi 30,912 mwaka 2013. Fursa ya Elimu ya msingi imeimarika kutoka skuli 299 zenye wanafunzi 226,746 mwaka 2010 hadi skuli 342 zenye wanafunzi 247,353. Wanafunzi walioandikishwa kuanza darasa la kwanza mwaka 2010 walikuwa 31,092. Mwaka huu wa 2013 walikuwa ni 35,703 ambao wote wamepatiwa nafasi ya kusoma watoto wote
waliofikia umri wa kuanza skuli.  Hali hii imeifanya nchi yetu kupiga hatua kubwa ya utekelezaji wa malengo ya Milenia na yale ya Elimu kwa Wote. Aidha, kwa kuzingatia umuhimu wa Sayansi na Teknolojia kwa watoto, Serikali imetekeleza mradi wa teknolojia ya habari na mawasiliano uitwao T.21 kwa skuli za msingi 74 hapa nchini.
Elimu ya sekondari imezidi kuimarishwa kwa kuongezeka kwa idadi ya skuli zinazotoa elimu hiyo kutoka kidato cha kwanza hadi cha sita na hivi sasa zipo skuli za sekondari 252 zenye wanafunzi 84,099 kutoka skuli 227 zilizokuwa na wanafunzi 78,794 mwaka 2010. Serikali imekamilisha ujenzi wa skuli mpya za sekondari 13 kati ya 16 ambazo zimeshapatiwa samani na vifaa vya maabara na kuanza kutumika.  Skuli 3 ambazo ni Paje- Mtule, Dimani na Tunguu ujenzi wake umefikia asilimia 94. Skuli hizi zilikuwa zikamilike mwaka 2015 kwa mujibu wa maelekezo ya Ilani na mipango ya awali, lakini Serikali imezikamilisha kabla ya wakati wake.
Katika uimarishaji wa elimu ya Sekondari, Serikali imekamilisha ujenzi wa skuli tatu za ghorofa katika maeneo ya Mpendae, Kwamtipura na Mazizini zinazotarajiwa kufunguliwa katika sherehe za maadhimisho ya miaka 50 ya Mapinduzi. Aidha, ujenzi wa skuli nyengine mbili za ghorofa unaendelea vyema katika vijiji vya Kibuteni Mkoa wa Kusini Unguja na Mkanyageni katika Mkoa wa Kusini Pemba. Serikali vile vile, imekamilisha matengenezo makubwa katika skuli za sekondari za Forodhani na Tumekuja Unguja na Utaani na Fidel Castro kwa Pemba. Matengenezo katika skuli za sekondari za Hamamni kwa Unguja na Uweleni Pemba yako katika hatua za mwisho kumalizika.
Aidha, kwa lengo la kuwaendeleza watoto wa kike katika masomo ya Sayansi, serikali imeamua kuzifanya skuli za sekondari ya Benbella Unguja na Utaani Pemba zitumike kwa azma hio.
Ndugu Waandishi wa Habari na Ndugu Wananchi
Fursa ya elimu ya juu nayo imezidi kuimarika kwa kuongeza idadi ya vijana wanaojiunga na elimu ya chuo kikuu hapa Zanzibar ambapo ndani ya kipindi hiki cha miaka mitatu vijana waliojiunga katika vyuo vikuu vya SUZA, chuo cha Elimu Chukwani na  Chuo Kikuu cha Zanzibar wameongezeka kutoka vijana 3,624 mwaka 2010 hadi vijana 4,485 mwaka 2013. Idadi hii haijumuishi vijana wanaoendelea kujisajli katika vyuo hivyo kwa mwaka wa masomo 2013 /2014.
Katika kipindi hiki Chuo Kikuu cha Taifa SUZA kimeongeza idadi ya skuli za masomo kutoka skuli moja mwaka 2010 hadi skuli tano. Skuli hizo ni skuli ya Elimu Endelezi, skuli ya Elimu ya Lugha ya Kiswahili na Lugha za Kigeni na skuli ya Sayansi ya Asili na Jamii na katika mwezi wa Oktoba, 2013 Skuli ya Tiba (Medical School) ilizinduliwa. Vile vile, Chuo kimeanzisha shahada ya uzamifu (PhD) ya lugha ya Kiswahili. Sambamba na hatua hiyo, Chuo hiki kimeongeza idadi ya kampasi zake na kufikia tatu badala ya mbili ambapo sasa chuo kimepata haiba nzuri kwa kuanza kutumia kampasi yake mpya ya Tunguu iliyoanza kutumika mwaka 2012.
Kadhalika, ndani ya kipindi hiki Chuo Kikuu cha Zanzibar nacho kimeongeza masomo yanayofundishwa katika chuo hicho, masomo yaliyoongezwa ni shahada ya Uzamili katika Utawala wa Umma na Sayansi ya Uchumi na Fedha.  Masomo mengine ni ya Shahada ya Benki ya Kiislamu na Fedha, Shahada ya Teknolojia ya Habari na Uchumi, Shahada ya Lugha na Ualimu pamoja na Shahada ya Uuguzi. Chuo Kikuu cha Elimu Chukwani nacho kimeimarisha masomo yake ikiwa ni pamoja na kuanza kusomeshwa kwa somo la lugha ya Kiswahili kwa wananchuo wa maandalizi (pre- university) na wa Shahada ya ualimu.
Ndugu Waandishi wa Habari na Ndugu Wananchi,
Ili kuwawezesha vijana wengi zaidi wanaopata sifa ya kuendelea na masomo yao vyuoni, Serikali imeongeza fedha kwa ajili ya mikopo ya wanafunzi kutoka Tsh. 2.3 bilioni mwaka 2010 hadi Tsh. 9.1 bilioni mwaka 2013. Serikali iliwapa mikopo waombaji wapya 1000 katika mwaka huu wa fedha wa 2013/2014. Serikali imechukua juhudi za makusudi ili kuongeza fedha kwa matumizi ya sekta ya elimu kwa ulinganisho wa matumizi ya serikali na Pato la Taifa kutoka asilimia 15.6 mwaka 2010 hadi asilimia 21.4 mwaka wa fedha uliomalizika wa 2012/2013.
Kadhalika, kwa upande wa madarasa ya kisomo kwa ajili ya  wasojua kusoma na kuandika, mafanikio yamepatikana kwa kupungua watu wenye tatizo hilo na kuwa na wanakisomo 463 katika mwaka huu wa 2013 kutoka wanakisomo 6,980 mwaka 2010.
Sambamba na jitihada hizo, Serikali pia imeendelea  kuimarisha mafunzo ya ualimu yanayotolewa katika chuo cha Kiislamu Mazizini, Chuo cha Kiislam Micheweni na Chuo cha Benjamin William Mkapa Kisiwani Pemba pamoja na mafunzo ya Ualimu na Daraja la 3A  yanatolewa na utaratibu wa Elimu masafa kwenye vituo 9 vya walimu Unguja na Pemba.  Katika mwezi wa Aprili, 2013 jumla ya walimu 675 walimaliza mafunzo yao ya cheti cha ualimu Daraja hilo.
Ndugu Waandishi wa Habari na Ndugu Wananchi,
Katika kuimarisha elimu ya ufundi na mafunzo ya amali, serikali imefanikiwa katika kuimarisha mazingira  na taaluma inayotolewa katika Taasisi ya Karume ya Sayansi na Teknolojia pamoja na vituo vya mafunzo ya Amali vya Mwanakwerekwe na Mkokotoni kwa Unguja na Vitongoji huko Pemba. Idadi ya wanafunzi katika taasisi ya Karume imeongezeka kutoka 237 mwaka 2010 hadi 1,215 mwaka 2012/2013. Kwa upande wa masomo ya kujiendeleza ya ufundi stadi, stashahada ya ICT, mafunzo ya Sayansi na Hisabati kwa elimu ya msingi na kidato cha nne, Taasisi ina jumla ya wanafunzi 996. Aidha, idadi ya wanafunzi wanaochukua masomo mbali mbali ya ufundi  na amali katika vituo vya mafunzo vya Mwanakwereke, Mkokotoni na Vitongoji imeongezeka kutoka wanafunzi 449 mwaka  2010 hadi wanafunzi 784 maka 2012/2013.
Kwa jumla nimeridhishwa sana na mafanikio ya sekta ya elimu licha ya changamoto zinazoikabili sekta hii ikiwemo uhaba wa walimu hasa wa sayansi, matokeo yasioridhisha ya mitihani ya Taifa, ukosefu wa samani na kuwepo kwa idadi kubwa ya wanafunzi katika baadhi ya madarasa ya skuli za mijini, uhaba wa fedha katika Bodi ya mikopo ya wanafunzi na nyenginezo. Hata hivyo, ninamatumaini kuwa changamoto hizi tutaweza kuzitatua hatua kwa hatua kwa ushirikiano na wananchi wakiwemo sekta ya binafsi kwa kuwekeza zaidi katika sekta ya huduma za jamii ikiwemo sekta ya elimu.
 AFYA
Ndugu Waandishi wa Habari na Ndugu Wananchi,
Ni wajibu tufurahie mafanikio makubwa tuliyoyapata katika Sekta ya Afya. Ukiacha mambo ya jumla ambayo tumeendelea nayo tangu awamu zilizopita kama vile ujenzi wa vituo 134 vya afya, ambavyo vimepelekea kupunguza masafa ya kupata huduma kwamba mwananchi wa Zanzibar hendi masafa ya kilomita 5, bila ya kupata huduma za afya.  Huduma zimeimarishwa kwenye hospitali  4 za koteji kila moja ikiwa na vitanda 40, na  huduma muhimu zikiwemo za uchunguzi wa maradhi wa Maabara, huduma za meno, upasuaji mdogo na kadhalika. Lengo letu la kuziimarisha hospitali hizi ili ziwe hospitali za Wilaya, limefikia hatua nzuri; hasa kwa hospitali ya Koteji ya Makunduchi na Kivunge.  Yapo mambo mengine ya msingi ambayo  Serikali imeyafanya katika kipindi cha miaka mitatu iliyopita katika kutekeleza Ilani ya CCM ya 2010 - 2015.
Kwa mfano katika kusimamia utekelezaji wa sera ya afya na ushirikishwaji wa wananchi na sekta binafsi katika kuchangia maendeleo ya afya kwa kuzingatia malengo ya Milenia, Dira ya 2020 na MKUZA, Serikali imezifanyia mapitio sera kadhaa pamoja na kushughulikia uanzishwaji wa Bima ya afya.
Ndugu waandishi wa  Habari na Ndugu Wananchi,
Katika kuendelea kuimarisha huduma za Hospitali ya Mnazi Mmoja, ili ifikie hadhi na kiwango cha Hospitali ya Rufaa, Serikali imeweza kuyafanya mambo yafuatayo:- kuweka  Mtambo wa Oxygen kwenye chumba cha upasuaji (theatre), wodi ya wagonjwa mahututi (ICU), wodi ya wazazi (maternity ) na chumba cha dharura na mashine ya kisasa ya kufanyia operesheni (minimal access surgery) kwenye chumba cha upasuaji.
Serikali imefungua “kituo cha meno cha tabasamu” (smiling center) kwa mashirikiano na wataalamu kutoka China na madaktari wazalendo wa Zanzibar kwa kufanya marekebisho kwa midomo yenye kasoro, Mfumo wa kuweka kumbukumbu za wagonjwa kwa kutumia kompyuta (Electronic medical Record System) umeanzishwa, vifaa vya kisasa vikiwemo kompyuta kwa ajili ya kazi hiyo vimewekwa sehemu ya mapokezi na umeanza kurikodi kumbukumbu za wagonjwa wa nje (OPD).
Mafunzo ya utafiti wa afya (clinical research) yametolewa kwa wafanyakazi 30 ili waweze kufanya tafiti mbali mbali na kusaidia kuimarisha huduma za afya, pamoja na kuifanyia ukarabati mdogo wodi ya wazazi na chumba cha wagonjwa wa dharura.  Mashirikiano na Hospitali ya Haukeland University ya Norway yameendelezwa kwa kubadilishana wataalamu. Kwa mwaka 2013 wataalamu wetu watano (madaktari wawili na wauguzi watatu 3) wamerejea kutoka Norway ambako walipata mafunzo kwa miezi sita wakati wafanyakazi watano (madaktari 2 na wauguzi 3) wa hospitali hiyo hivi sasa wapo katika Hospitali ya Mnazi Mmoja wakisaidiana na madaktari na wauguzi wetu wazalendo katika kutoa huduma bora za afya. Kurudi kwao kumeongeza ujuzi zaidi wa kukabiliana na kesi za maradhi mbali mbali.
Kadhalika, ipo miradi iliyobuniwa ambayo tayari imeanza kutekelezwa.  Miradi hio ni:- Mradi wa kuimarisha huduma za mama na mtoto, Mradi wa ujenzi wa jengo la wodi ya watoto, Mradi wa upasuaji wa maradhi ya kichwa na uti wa mgongo (Neurosurgical unit), Mradi wa kitengo cha “Gastro-Enterology”, Mradi wa kuimarisha kitengo cha kisasa cha wodi ya wagonjwa mahututi (ICU) na Mradi wa elimu ya utafiti.  Vile vile, maandalizi ya utibabu wa matatizo ya maradhi ya haja ndogo na figo yameanza.
Hospitali ya Wete imefanyiwa matengenezo katika wodi ya wanaume pamoja na vyoo vyake, kliniki ya watoto pamoja na kupatiwa vifaa vya kisasa. Aidha, imejengwa Maabara mpya kubwa na ya kisasa kwa kushirikiana na “International Center for Aids care and treatment Programme” ( ICAP) katika hospitali ya Micheweni.
Kwa kupitia mashirikiano yaliyoanzishwa baina ya hospitali ya  Kivunge na mradi wa HIPZ, hospitali imefanikiwa  kuanzisha kitengo cha huduma za dharura (Emergency Unit) kitakachotoa huduma za haraka kwa wagonjwa wanaofikishwa hospitalini hapo pamoja na kufanyiwa matengenezo kwa kituo cha elimu ya kujiendeleza (Resource Centre) iliyopo hospitalini hapo.
Katika kutekeleza mpango wa kuifanya Hospitali ya Abdalla Mzee kuwa hospitali ya Mkoa, mchakato umeanza ambapo Hospitali hii itajengwa kwa msaada mkubwa kutoka Jamhuri ya Watu wa China na itakuwa ni ya kisasa yenye uwezo wa kutoa huduma za wagonjwa wa maradhi mbali mbali na wagonjwa mahututi (ICU), huduma za dharura (accident and emergency) na huduma za uchunguzi wa CT Scan.
Katika kipindi hiki huduma za matibabu ya macho zimefanyika na uchunguzi na utibabu wa macho kwa wafanyakazi na wanafunzi 69 wa Jeshi la Polisi umefanyika. Askari  51 walipatiwa miwani na 18 walipewa dawa za macho. Huduma za uchunguzi na utibabu wa macho zimetolewa kwa wananchi katika maeneo mbali mbali Unguja na Pemba.
Kwa kushirikiana na Kitengo cha Elimu Mjumuisho na Stadi za Maisha cha Wizara ya Elimu, na Timu za Afya za Wilaya, kitengo cha maradhi ya macho kimeweza kufanya uchunguzi na utibabu wa macho kwa jumla ya wanafunzi 2,665 wa skuli mbali mbali ambao  kati yao, 587 walipatiwa matibabu ikiwemo dawa za macho, ushauri wa kiafya na utoaji wa miwani.
Serikali iliahidi kukiimarisha Chuo cha Taaluma za Sayansi ya Afya pamoja na watumishi wa sekta ya afya kwa kuwapatia mafunzo ya ndani na nje ya nchi. Utekelezaji wa ahadi hii umekwenda vizuri ambapo wafanyakazi  226  wamepelekwa mafunzo ya muda mrefu na ya muda mfupi katika vyuo mbali mbali.
Chuo cha Taaluma za Sayansi za Afya sasa kitaunganishwa na SUZA katika kukiendeleza, uamuzi huu hivi sasa unafanyiwa kazi na Serikali.
Katika kuziimarisha afya za wanawake, Serikali imeondoa ada ya Tsh. 40,000 kwa akinamama wanaokwenda kujifungua kwa operesheni. Kadhalika, huduma za bohari kuu ya dawa zimeimarishwa ili kurahisisha upatikanaji wa dawa nchini.  Bohari Kuu mpya ya dawa ilifunguliwa rasmi huko Maruhubi katika shamrashamra ya Sherehe  za Maadhimisho ya miaka 49 ya Mapinduzi mwezi Januari, 2013.
UTAWALA  BORA
Ndugu Waandishi wa Habari na ndugu Wanachi,
Suala la Utawala Bora hivi sasa nimeliweka katika Ofisi ya Rais na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, kufuatia mabadiliko ya Wizara niliyoyafanya hivi karibuni.
Katika kutekeleza dhamira yetu ya kupambana na rushwa, Serikali ya Awamu ya Saba imeanzisha Taasisi ya Kuzuia Rushwa na Uhujumu wa Uchumi kwa kupitisha sheria namba 1 ya mwaka 2012. Kuanzishwa kwa Taasisi hiyo ambayo imeshaanza kufanya kazi kutaisaidia  Serikali kupambana na rushwa nchini kama Ilani ya CCM ya Uchaguzi Mkuu ya mwaka 2010 ilivyoagiza.
Serikali inaendelea kuimarisha Ofisi ya Mkurugenzi wa Mashtaka Zanzibar ili iweze kuendesha mashtaka katika ngazi zote za mahakama. Aidha, Ofisi ya Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali inazidi kuimarisha kwa kuwapa mafunzo wafanyakazi wake kwa lengo la kuimarisha ukaguzi  na  uhakiki wa mali za Serikali.  Asilimia 88 ya wafanyakazi katika ofisi hii wameweza kupatiwa elimu ya juu. Aidha, mazingira ya kufanyia kazi yameimarishwa ikiwa ni pamoja na kuipatia Ofisi kwenye majengo ya kisasa na vitendea kazi vya kisasa.
Ofisi ya Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali imepata sifa ndani na nje ya nchi kama vile katika Jumuiya ya Afrika Mashariki pamoja na SADC kwa ufanisi katika utendaji wake. Baadhi ya nchi zinaleta wataalamu wao  kuja Zanzibar kujifunza hasa Computerized Auditing.   Kadhalika, nchi kadhaa zimekuwa zikitaka  ushauri kutoka Ofisi hii. Utekelezaji wake umefikia asilimia 67 kwenye lengo la ukaguzi.
Ndugu Waandishi wa Habari na Ndugu Wananchi,
Katika kuimarisha utoaji wa haki, Serikali inaendelea kuimarisha Mahakama Kuu na Mahakama ya Kadhi kwa kufanya ukarabati wa majengo yake. Ndani ya kipindi cha miaka mitatu mahakama ya watoto imeweza kuanzishwa kwa lengo la kulinda haki za watoto nchini.
Vile vile, idadi ya majaji imeweza kuongezeka kutoka watatu hadi kufikia 6 wakiwemo majaji wanawake kwa mara ya kwanza. Kadhalika, Mahakama inaendeleza mapitio ya sheria mbali mbali  ili kuweza kuimarisha utoaji wa huduma katika sekta hiyo.
Kuhusu kuanzishwa kwa mahakama ya biashara, sheria imeshapitishwa na sasa kanuni zinaendelea kutayarishwa hivyo, mahakama hiyo itaanza kufanya kazi hivi karibuni.
TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA
Suala la Tawala za Mikoa, Serikali za Mitaaa na Idara Maalum za SMZ nimeziweka kwenye Ofisi ya Rais, katika mabadiliko ya wizara niliyoyafanya hivi karibuni.
Kuwepo kwa serikali za mitaa ni mafanikio makubwa yanayotokana na demokrasia na utawala bora nchi. Ndani ya kipindi cha miaka mitatu Serikali imeanza kuifanyia mapitio Sheria za Serikali za Mitaa na Tawala za Mikoa ambapo Mpango wa Mageuzi ya Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa, umeandaliwa na Sera yake imeshapitishwa na karibuni inatarajiwa kuanza kufanya kazi.  Serikali za Mitaa zimeanza kuimarishwa kwa kuajiriwa watalaamu wa fani mbali mbali, vifaa vya kisasa na vitendea kazi ili kutoa huduma bora kwa wananchi.  Jitihada kubwa inafanywa katika kuwahamasisha wananchi kuunda Kamati za Maendeleo yao ili kusukuma kasi ya maendeleo.  Vitendo vya uhalifu vinadhibitiwa kupitia mfumo wa Ulinzi Shirikishi na Polisi Jamii.  Suala la usafi wa miji na hifadhi ya mazingira nalo linashughulikiwa.
UTUMISHI WA UMMA
Katika kipindi hiki cha miaka mitatu nimeanzisha utaratibu wa Watendaji na Mawaziri kubainisha utekelezaji wa bajeti za Wizara zao na jinsi wanavyosimamia mipango iliyoandaliwa kwa kila robo mwaka hapa Ikulu. Aidha,  Serikai  imeandaa miundo ya  Utumishi ya Wizara na Taasisi zake kwa lengo la kuleta uwiano wa kimaslahi kwa  kuzingatia viwango vya elimu na uzoefu wa utumishi wa wafanyakazi. Utekelezaji wa miundo ya utumishi utaanza hivi karibuni.  Masuala ya Kazi na Utumishi wa Umma nayo nimeyaaweka katika Ofisi ya Rais katika mabadiliko ya Wizara niliyoyafanya hivi karibuni.
Ndugu Waandishi wa Habari na Ndugu Wananchi,
Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar, Awamu ya Saba, imefanya jitihada ya kuimarisha mishahara na stahili nyengine za wafanyakazi mara mbili katika kipindi cha miaka mitatu. Vile vile, Serikali imeongeza nafasi za mafunzo kwa watendaji wa Serikali ndani na nje ya nchi. Chuo cha Utawala  wa Umma kimezidi kuimarishwa kwa kupatiwa jengo jipya huko Tunguu ambalo lilizinduliwa tarehe 5 Januari, 2013.
WAZEE, WATU WENYE ULEMAVU NA WATOTO
Ndugu Waandishi wa Habari na Ndugu Wananchi,
Katika jitihada za Serikali za kuanzisha makundi maalumu, Serikali ya Awamu ya Saba imeweza kuzimiimarisha huduma za wazee kwa kuwaongeza posho hadi Tsh. 40,000 kwa mwezi, kuwapatia chakula cha uhakika kwa kila siku, kuimarisha huduma za maji pamoja na kuimarisha ulinzi kwa wazee wanaoishi kwenye nyumba za Sebleni, Limbeni na Gombani Pemba. Vile vile, Serikali imeimarisha juhudi za kulinda haki  za watoto kwa kuanzisha sheria mpya ya kumlinda mtoto ya mwaka 2011, kuongeza vituo vya Mkono kwa Mkono hadi kufikia vinne pamoja na kuanzisha mahakama ya watoto hapa Zanzibar  kwa lengo la kuzilinda haki zao.
Katika kipindi hiki cha miaka mitatu,huduma za watu wenye ulemavu zimeimarishwa.  Zoezi la usajili kwa ajili ya kuimarisha huduma na haki zao, likiwemo suala la elimu kwa watoto limefanyika.  Tarehe 28 Septemba, 2012 Serikali iliizindua Mfuko wa kuwasaidia watu wenye ulemavu na  hadi sasa jumla ya Tsh. 198 milioni zimepatikana.
HABARI, UTAMADUNI NA MICHEZO.
Ndugu Waandishi wa Habari na Ndugu Wananchi,
Katika eneo la vyombo vya Habari, Ilani ya Uchaguzi ya CCM ya Uchaguzi Mkuu ya mwaka 2010-2015 inaelekeza Serikali kusimamia utekelezaji wa Sera ya Habari na kuendeleza uhuru wa vyombo vya habari nchini. Katika kutekeleza agizo hili, Serikali katika kipindi cha miaka mitatu imetoa vibali vya kuanzishwa Redio nne (4) za FM na Televisheni tano (5). Sambamba na hatua hizo, Shirika la Magazeti ya Serikali limeweza kuwafikia wasomaji wengi zaidi kwa kuongeza maeneo ya usambazaji Unguja na Pemba na Tanzania Bara.
Ndugu Waandishi wa Habari na Ndugu Wananchi,
Katika kipindi hiki Shirika la Utangazaji la Zanzibar (ZBC) lilianzishwa na Serikali ililazimika kuchukua hatua kadhaa, kama vile kununua  vifaa na mitambo ya kisasa, ili viweze kuyarusha matangazo yake kwa ufanisi, kuonekana na kusikika katika sehemu mbali mbali ndani na nje ya Zanzibar na Tanzania kwa ujumla. Katika kipindi hiki Serikali ilifanya uamuzi wa kuingia katika utaratibu wa kisasa wa digitali kwa kununua vifaa na mitambo mipya, kwa ajili ya kuimarisha shughuli za utangazaji Zanzibar na mafunzo ya kuwaendeleza wanahabari mbali mbali yalitolewa kwa lengo la kuyatekeleza majukumu yao kwa ufanisi mkubwa. Katika kipindi hiki jumla ya waandishi 38 wameweza kupatiwa mafunzo katika viwango vya stashahada, shahada ya kwanza na shahada ya pili. Vile vile, Serikali  iliyaimarisha matangazo ya redio kwa kuuhamisha mnara wa masafa ya kati (medium waves) kutoka Chumbuni na kuupeleka Bungi, ambako Ofisi na Studio mpya na nyumba mbili (2) za kisasa za familia nne za wafanyakazi zimejengwa.  Aidha, ukarabati wa mnara wa mawimbi mafupi (short wave) nayo umefanyika. Ukarabati huo umefanywa kwa ushirikiano wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar na Serikali ya Jamhuri ya Watu wa China.
Ndugu Waandishi wa Habari na Ndugu Wananchi,
Chuo cha Uandishi wa Habari nacho kimeimarishwa kwa lengo la kujitosheleza kwa wanahabari.  Vifaa vya kufundishia vilinunuliwa na walimu wenye ujuzi waliajiriwa.  Katika kuimarika kwa chuo hicho, hivi sasa wanafunzi wanaosomea cheti na stashahada wameongezeka kutoka 75 mwaka 2009/2010 hadi kufikia 122 kwa mwaka 2010/2011. 
Kwa upande mwingine, Serikali imelishughulikia tatizo la uingizaji wa vifaa vya utangazaji vilivyopitwa na wakati TV na redio ili kuepusha Zanzibar kugeuzwa jaa.  Serikali ilitekeleza kwa mafanikio makubwa Mkakati wa Mageuzi ya Teknolojia ya Utangazaji kutoka analogi kwenda dijitali nao umetekelezwa vyema.
Vile vile, jengo la Utangazaji la zamani liliopo Rahaleo limefanyiwa ukarabati mkubwa ili liweze kutumika kwa ajili ya studio za kurikodia nyimbo za wasanii wetu.  Hivi sasa Serikali tayari ishachukua hatua ya kununua vifaa vya studio hio.
Ndugu Waandishi wa Habari na Ndugu Wananchi,
Katika kipindi cha miaka mitatu iliyopita, Serikali imechukua hatua za kuifanyia mapitio marekebisho sera ya Utamaduni na Michezo na sheria zinazoongoza taasisi zinazosimamia utamaduni ili ziweze kuenda sambamba na wakati huu wa kuihusisha sekta ya utamaduni na utalii kwa wote.
Katika kuufanya utamaduni uwe na tija zaidi, wizara imeweza kukamilisha mchoro wa ramani ya Utamaduni katika shehia za Unguja na Pemba pamoja na Utafiti wa Urithi wa Utamaduni katika mikoa mitano ya Zanzibar na hatimaye ihifadhiwe na itangazwe nchi za nje kwa kuingizwa katika orodha ya “UNESCO” ya tamaduni zinazohifadhiwa. Hivi sasa Serikali imo katika mchakato wa kuifanyia marekebisho makubwa sheria ya sanaa inayokusanya mambo yote ya utamaduni.  Mswada huo wa sheria hivi sasa unaandaliwa.
Kuhusu ujenzi wa kiwanja cha kisasa cha michezo na sherehe za kitaifa, Serikali imeuchagua uwanja wa Mao Tse Tung uliopo mjini Unguja utumike kwa  shughuli hizo. Hatua iliofikiwa hivi sasa ni kukamilika michoro ya awali. Serikali ya Jamhuri ya Watu wa China imekubali kushirikiana na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar katika ujenzi huo na mkataba wa makubaliano tayari umetiwa saini na pande mbili.
Ndugu Waandishi wa Habari na Ndugu Wananchi,
Uwanja wa Gombani Pemba tayari ulifanyiwa marekebisho kwa kuweka nyasi bandia na hivyo kukidhi haja ya mashindano ya kimataifa ya mpira wa miguu. Halikadhalika, matengenezo ya taa za uwanja yamekamilika ambayo yanauwezesha uwanja kutumika hata wakati wa usiku. Serikali hivi sasa imeanza utaratibu wa kuezeka paa jipya na ujenzi wa njia ya kukimbilia ili kutoa fursa ya michezo ya riadha kufanyika kukidhi viwango vya kimataifa. Aidha, kwa kushirikiana na Serikali ya Japan ujenzi wa kiwanja cha michezo ya ndani umeanza na unategemewa kukamilika mwishoni mwa mwezi wa Disemba 2013.
Kwa upande wa Uwanja wa Amaan, ukarabati mkubwa unafanyika kuimarisha eneo la kuchezea ambapo utawekewa nyasi bandia. Kazi hii inatarajiwa kukamilika katikati ya mwezi wa Disemba na utatumika kwa ajili ya mashindano ya maadhimisho ya miaka 50 ya Mapinduzi.
Ndugu Waandishi wa Habari na Ndugu Wananchi,
Katika kipindi hiki cha miaka mitatu ya Uongozi wangu, Serikali imechukua hatua mbali mbali kuzilinda, kuzihifadhi na kuzidumisha mila, silka na maadili mema ya Wazanzibari. Hatua zimechukuliwa za kuzikagua kazi za sanaa na kuchukuliwa hatua za kuilinda na kuhifadhi mila na silka kulingana na matokeo ya ukaguzi huo. Kukamilika kwa kamusi la Kipemba, Kimakunduchi, Kitumbatu kutapelekea wananchi kuyatumia makamusi hayo ili kuulinda utamaduni wetu.
Aidha, kumekuwa na  uhakiki wa Matamasha,  Matangazo  ya  kibiashara,  Video  za  nyimbo,  Tenzi  zenye  maudhui  mbali mbali  na  Filamu tofauti  katika  maduka  ya  kukodishia  kanda  Unguja  na  Pemba. Bodi imekagua pia vikundi vya ngoma, michezo ya kuigiza jukwaani, tenzi na mashairi ya kughani ili kuhakikisha mila, silka na utamaduni wa Kizanzibari hauathiriwi na mambo hayo.
Hatua hizo zimekwenda sambamba na hatua za kuhifadhi kumbukumbu za kihistoria na Mambo ya Kale. Utafiti wa uchimbaji wa eneo la Ngome Kongwe, Forodhani Unguja kulingunduliwa vigae vya vyungu, ‘Kwale pottery’ vya karne ya kwanza. Aidha, matengenezo yamefanyika kwa jengo la makumbusho la Mahodhi ya Hamamni (Hamamni Baths) ili kulirudisha katika hadhi yake ya awali na kuweza kuongeza idadi ya vivutio kwa wageni. Serikali imeyafanyia matengenezo majengo ya Mangapwani kwenye Mahandaki ya Vita Kuu ya Pili ya Dunia pamoja na mnara wake na magofu ya Kizimbani na Hamamni na jengo la Beit el Ajaib.
MAZINGIRA
Ndugu Waandishi wa  Habari na Ndugu Wananchi,
Katika kipindi cha miaka mitatu iliyopita Serikali imeweza kutekeleza majukumu muhimu ya kuyalinda na kuyahifadhi mazingira ya nchi yetu kwa kulingana na Sheria, Sera na Ilani ya CCM ya Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2010- 2015.
Mambo  makuu yote yaliyozingatiwa kwenye Ilani na kwenye MKUZA II yameweza kutekelezwa kwa mafanikio makubwa. Serikali imeweza kufanya mapitio ya Sera ya Mazingira ya mwaka 1992 na kuzindua Sera ya Mpya ya Mazingira ya mwaka 2013 ambayo inatoa muongozo kwa shughuli za uhifadhi wa mazingira nchini kwa kuzingatia hali halisi ya kimazingira ilivyo na kwa kuzingatia athari za mabadiliko ya tabianchi. Mapitio ya Sheria ya Mazingira ya mwaka 1996 yamelenga katika kuongeza nguvu za kisheria katika kuyahifadhi na kuyasimamia mazingira nchini.  Sambamba na hatua hizo, Serikali imepitisha kanuni mbili za usimamizi wa mazingira.
Kanuni ya kwanza ni ya usimamizi wa maliasili zisizorejesheka, ambayo inatoa miongozo ya uvunaji endelevu wa maliasili hizo na kupunguza wimbi la uchimbaji kiholela wa mawe na mchanga.  Kanuni ya pili ni ya kupiga marufuku mifuko ya plastiki, ambayo inakataza kuingiza, kutumia, kusafirisha na kuhifadhi mifuko ya aina yote ya plastiki hapa Zanzibar.  Jumla ya tani 288 za plastiki zimekamatwa na kuteketezwa na wanaohusika wanachukuliwa hatua za kisheria.
Hivi karibuni Serikali ilianzisha na kuzindua Kikosi kazi cha udhibiti wa uharibifu wa mazingira katika visiwa vya Zanzibar.  Uanzishwaji wa Kikosi kazi hicho ni hatua muhimu na ya lazima ya kulinda mazingira yetu, dhidi ya vitendo vyote vibaya vinavyoathiri mazingira.  Tangu kilipozinduliwa  kikosi kazi hicho watu kadhaa wameshakamatwa na taratibu za kisheria zimechukuliwa dhidi yao.
Ndugu waandishi wa  Habari na Ndugu Wananchi,
Sera mpya ya Mazingira ya 2013 inaelekeza kutoa elimu kwa wananchi juu ya umuhimu wa utunzaji na hifadhi ya mazingira na kuimarisha ukaguzi katika maeneo  ya makaazi, viwanda na mahoteli.  Elimu imesisitizwa juu ya umuhimu wa kuhifadhi misitu,umuhimu wa mikoko, maliasili zisizozalishika,uhifadhi wa bioanuwai, na kadhalika.
Ndugu Waandishi wa  Habari na Ndugu Wananchi,
Kwa upande mwingine Serikali imefanya mapitio ya Uchaguzi ya miradi ya vitega uchumi ili kujua athari za mazingira na kupendekeza hatua za utekelezaji. Katika kipindi hicho jumla ya miradi 160 imefanyiwa ukaguzi na kupewa miongozo na ushauri wa kimazingira. Vilevile miradi ya maendeleo na vitega uchumi 51 imefanyiwa tathmini ya athari za kimazingira na kutolewa vyeti vya mazingira kwa miradi hiyo.
Masuala mengine yaliyotekelezwa katika kipindi hicho ni kushughulikia suala la mabadiliko ya tabianchi kwa kufanya utafiti, kuangalia athari za mabadiliko ya tabianchi kwa uchumi wa Zanzibar na kuorodhesha maeneo yanayoingia maji ya chumvi ambapo jumla ya maeneo 148 yameathirika Unguja (maeneo 25) na Pemba (123).
Aidha, Serikali imeandaa ramani ya mazingira na kuanzisha mfumo wa kuweka taarifa za kimazingira kwa njia ya ramani kwa kutumia kompyuta yaani Zanzibar Environmental Information Management System (ZEIMS). 
USHIRIKIANO WA KIMATAIFA NA WAZANZIBARI
WANAOISHI NCHI ZA NJE (DIASPORA)
Ndugu Waandishi wa Habari na Ndugu Wananchi,
Serikali ya Mapinduzi ya Awamu ya Saba imeanzisha  Idara ya Ushirikiano wa Kimataifa na Uratibu wa Wanzanzibari Wanaoishi Nje (Dispora) kwa lengo  la kurahisisha na kushajishisha ushiriki wao  katika harakati za  maendeleo ya nchi yao. Kwa kupitia idara hii, Wazanzibari walioko nje wanaendelea kutoa michango mbali mbali ikiwemo ya fedha na kitaalamu katika sekta mbali mbali za kiuchumi na kijamii. Aidha, Idara imekuwa ikifanya kazi ya kuwahamasisha Wazanzibari walioko nje kuja kuwekeza nchini.
Kupitia Wizara ya Mambo ya Nchi za Nje na Ushirikiano wa Kimataifa wa Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania,  Idara ya Ushirikiano wa Kimataifa na Uratibu wa Wanzanzibari Wanaoishi nje  imeimarisha ushiriki wa Serikali yetu katika masuala na mikutano mbali mbali ya Kimataifa.
Vile vile, Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar, Awamu ya Saba, imeimarisha mashirikiano na nchi mbali mbali, Taasisi za Kimataifa na washirika wote wa Maendeleo.
MWISHO
Ndugu Waandishi  na Ndugu Wananchi,
Napenda nitoe shukurani zangu za dhati kwa wananchi wote kwa kushirikiana na Serikali. Ni matumaini yangu kwamba wananchi wataendelea kushirikiana na Serikali na vile vile wafanyakazi wote wa Serikali wataendelea kuongeza juhudi zao ili tuweze kutekeleza malengo yetu ya DIRA YA MAENDELEO 2020.  Hivi sasa tumebakiwa na miaka sita tu hadi kuyafikia malengo hayo. Pindi kama tukiyafikia, hapana shaka tutaitoa nchi katika kundi la nchi za kipato cha chini na kuwa katika kundi la nchi za kipato cha kati (Middle income).
Bila ya shaka yoyote, hali hiyo tutaifikia tu tukiwa makini, watiifu wa amani na utulivu nchini. Utiifu wa sheria ni hatua moja muhimu katika kuyafanikisha hayo. Ni jukumu la viongozi wote wa Serikali,  wanasiasa, viongozi wa dini na viongozi wengine katika jamii, sote kwa pamoja tutekeleza wajibu wetu kwa kuhakikisha kwamba amani na utulivu unadumishwa na sheria za nchi zinafatwa.  Ilivyokuwa Serikali inaongozwa kwa misingi ya Katiba na Sheria zake, basi vyama vyote vya siasa, taasisi zisizokuwa za Serikali na zile za jamii nazo ni lazima ziongozwe kwa kuzingatia katiba za nchi, katiba zao na kanuni zao na kuzifuata sheria za nchi.  Sura ya Tatu ya Katiba yetu imeelezea kuhusu Kinga ya Haki za Lazima, Wajibu wa Uhuru wa Mtu Binafsi, kuanzia kifungu cha 11 hadi kifungu cha 25.  Lakini kila mtu ana wajibu wa kufuata na kuitii Katiba ya Zanzibar na Sheria zake. Hili ni jambo muhimu na ni lazima tuyaenzi na tuyadumishe Mapinduzi yetu na tuudumishe na tuuendeleza Muungano wetu kwani  ndio nguzo yetu kubwa ya maendeleo na vilivyotufikisha hapa tulipofika hivi sasa na tunakokusudia kufika katika miaka mingi ijayo.  Katika kipindi hiki tumeshuhudia Muungano wetu umeendelea kuwa imara zaidi tangu pale ulipoanzishwa na nchi yetu imepata heshima kubwa sana katika Jumuiya ya Kimataifa.  Tumepata mafanikio makubwa ya kisiasa, kiuchumi na ustawi wa jamii, ingawa zimekuwepo baadhi ya changamoto lakini zitaendelea kushughulikiwa hatua kwa hatua.
Napenda niwahakikishie wananchi wote kwamba Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar itaendelea kushirikiana na Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania katika kuendeleza Muungano wetu, kuimarisha na kuwatumikia wananchi.  Katika kuuimarisha Muungano wetu, sote tumetimiza wajibu kwa kutoa maoni yetu kwa ajili ya kuandaliwa Katiba Mpya ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.  Tume ya Kuratibu Maoni ya Katiba Mpya umefanya kazi nzuri na itaendelea kuifanya kazi hio kama vile sheria inavyoiongoza.  Hatua zilizobakia nazo zitakamilishwa kwa kuzingatia sheria iliyopo ili hatimae tupate Katiba Mpya itakayoliongoza Taifa letu na kuimarisha Muungano wetu. Napenda nimshukuru na nimpongeze sana Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dk. Jakaya Mrisho Kikwete kwa kusimama imara katika kuutetea na kuuendeleza Muungano wetu na kwamba siku zote yuko tayari kuzizungumzia changamoto zinazoukabili Muungano wetu na kutafuta njia za kuzipatia ufumbuzi kila zinapotokea.
Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar itaendelea kushirikiana na Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania katika kuuendeleza na kuudumisha Muungano kwa manufaa ya nchi zetu mbili.
Hivi sasa tumemaliza miaka mitatu tangu SMZ yenye Mfumo wa Umoja wa Kitaifa imeingia madarakani.  Hata hivyo, bado ipo kazi kubwa mbele yetu ambayo inahitaji jitihada zetu sote.  Tuendelee kushikamana na kupendana, tushindane kwenye mfumo wa vyama vingi vya siasa bila ya kugombana, kukashifiana, kulaumiana, kutukanana na kudharauliana. Zanzibar haitajengwa kwa mambo hayo yasiyokuwa na tija wala faida.  Huu ni wakati wa kuongeza kasi na kuijenga nchi yetu, ili tusije tukaachwa nyuma.
Napenda kuwahakikishia wananchi wote kuwa serikali kwa upande wake itaendelea kutekeleza wajibu wa kikatiba na sheria kwa kuilinda amani, utulivu, mali na maisha ya watu. Hakuna atakayedhulumiwa wala kuonewa, lakini pia hakuna atakayevumiliwa kwa kuvunja sheria.
Tukiwa tumo katika kipindi cha shamrashamra ya kusherehekea miaka 50 ya Mapinduzi ya Zanzibar, natoa wito kwa kila mmoja wetu awe ni sehemu ya kuzifanikisha sherehe zetu kwa furaha, salama, amani na utulivu. Tushirikiane sote kwa pamoja na tuendeleze umoja na mshikamano katika kuzifanikisha sherehe zetu, ili tuioneshe dunia mafanikio yetu ya miaka 50, utamaduni wetu na kwamba tunauthamini umoja wetu, amani na  mshikamano.
Ahsanteni kwa kunisikiliza.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.