Na Asya Hassan
MTU mmoja anaejulikana kwa jina la Fadhili Yussuf
Khamis (34) mkaazi wa Magomeni na Jambiani Unguja, anashikiliwa na jeshi la
polisi mkoa wa kusini Unguja, kwa madai ya kumtorosha mwanafunzi.
Tukio hilo lilitokea Januari 14, 2014 majira ya
saa 5:30 za asubuhi katika maeneo ya Jambiani Kikadini mkoa wa Kusini Unguja.
Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na Kamanda wa
polisi mkoa huo Agostino Ulomi, mtuhumiwa anashughulika na utunzaji wa msikiti
wa Jambiani na kwamba uongozi wa msikiti ulimpatia chumba kwa ajili ya
kupumzika.
Alisema polisi walipata taarifa za tukio hilo kupitia
uongozi wa shehia na walipofika eneo la tukio walimkuta mtuhumiwa akiwa pamoja
na mwanafunzi huyo chumbani.
“Mtu huyu anaedaiwa kufanya vitendo hivi
anaishi Magomeni ambako ndipo ilipo
familia yake lakini shughuli zake nyingi anazifanyia Jambiani kwa sababu
amekabidhiwa kazi ya kutunza msikiti na uongozi wa msikiti umempatia chumba,”
alisema kamanda huyo.
Alisema mtuhumiwa anashikiliwa kituo cha polisi
Paje na anatarajiwa kufikishwa mahakamani leo.
Kuhusu kuingiliwa, alisema hawezi kuthibitisha kama
kitendo hicho kimefanyika, lakini daktari aliemfanyia uchunguzi anaweza
kuthibitisha hilo.
Katika tukio jengine mtoto Muzdalifa Mohammed
Khamis (3) mkazi Koani amejeruhiwa baada ya kugongwa na vespa yenye namba za
usajili Z 746 AF iliyokuwa ikiendeshwa na Juma Bakar Khamis (28) mkaazi wa
Amani.
Alisema mtoto huyo alipata majeraha katika maeneo
mbalimbali ya mwili wake lakini aliwahishwa hospitali kuu ya Mnazimmoja kwa
matibabu na hali yake inaendelea vizuri.
No comments:
Post a Comment