Habari za Punde

Hati ya Muungano yatikisa Ikulu

Na Mwandishi wetu
IKULU imeelezea kusikitishwa, kufadhaishwa na kusononeshwa, kuhusu madai kwamba Muungano wa Tanganyika na Zanzibar wa Aprili 24, 1964 si halali, kwa sababu hakuna hati ya Muungano.

Akizungumza na waandishi wa habari Ikulu jana, Katibu Mkuu Kiongozi, Balozi Ombeni Sefue, alisema kauli hizo sio tu zimeisononesha serikali lakini Watanzania pia.

Alisema kamwe Ikulu haikuamini kama hali ingekuwa hivyo kwa baadhi ya Watanzania kuhoji uhalali wa muungano miaka 50 baada ya kuasisiwa kwake.

Alisema hati ya makubaliano ya Muungano ipo na inahifadhiwa kama mboni ya jicho katika maeneo maalum ili isiharibike au kupotea kwa sababu ni nyaraka nyeti na kwa hali ya kawaida huwa hazitolewi.

Hata hivyo, alisema kwa maagizo ya Rais Jakaya Kikwete, wameamua kuitoa hati halisi ya Muungano huo yenye saini za waasisi wake na kwamba saini zao hazikuhushiwa.


Aidha alisema hati hiyo itawasilishwa tu mbele ya bunge maalum la katiba, iwapo serikali itaombwa na Mwenyekiti wa bunge maalum la katiba kufanya hivyo.

Alisema ili kuhakikisha Watanzania wanapata fursa ya kuisoma, alisema serikali itaziweka nakala  za mkataba huo katika makumbusho ya taifa.

Balozi Sefue alitumia fursa hiyo kuwaonesha waandishi wa habari nakala halisi ya Muungano huo na nakala zake kuzigawa kwa waandishi wa habari.


Alisema mbali ya hati hiyo, hati nyengine zilihifadhiwa katika mazingira nyeti ni hati ya uhuru wa Tanganyika na hati ya Tangayika kuwa Jamhuri na kukiri kwamba hawapendi kuionesha.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.