Habari za Punde

Mjadala mkali Bunge la Katiba.

Na Mwantanga Ame, Dodoma
BAADA ya kuzuka utata mkubwa juu ya hati ya Muungano kama ipo ama haipo, Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais, Mahusiano na Utaribu, Steven Wasirra, amekubali yaishe baada ya kusema hati ya Muungano ipo na ipo salama katika miaka 50 ya Muungano.

Akiwasilisha ripoti ya kamati namba sita, Wasira  alisema hati hiyo itawasilishwa kwa Mwenyekiti wa bunge, Samuel Sitta, katika kipindi cha siku mbili zijazo.

“Kwa niaba ya dola ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, nitawasilisha hati ya makubaliano ya Muungano yenye saini marehemu Abeid Amani Karume na Mwalimu Julius Nyerere,” alisema Wasira na kuamsha nderemo.

Wakichangia mjadala, mjumbe Moses Machale, alionesha kushangazwa na serikali kutangaza kuwa na  hati ya Muungano katika kipindi kifupi kiasi hicho na kuhoji uhalali wake.

Mohammed Chombo, alisema Muungano wa Tanganyika na Zanzibar una maadui ndani na nje ya Tanzania na ndani ya bunge hilo.

Alisema wenye nia mbaya wanataka kuvunja Muungano na kuifanya Tanzania isiwe na amani na kusababisha vurugu, ubaguzi na chuki.


Bunge lilichangamka zaidi pale mjumbe Asha Bakari, alipohoji sababu ya watu kuanza kudai hati ya muungano wakati Zanzibar imeunda Serikali ya Umoja wa kitaifa bila ya hata kuwapo mkataba uliofikiwa na kwamba ni vyema wanaodai hati ya Muungano wangelianza kudai mkataba huo.

Nae Dk. Khamis Kigangwala, alisema kuna tatizo kubwa kwenye takwimu za Tume ya Jaji Warioba, kwani takwimu alizokuja nazo ni za watu wa mikoa miwili.

Kwa upande wake Zakia Meghji, alisema yeye binafsi alikuwa hana wasiwasi wa kutokuwepo hati ya Muungano kwa sababu kuna machapisho mengi yanayothibitisha kuwepo  hati hiyo.

Alisema kinachoonekana kuna watu walikuwa na dhamira ya kuifanya Tanzania isifikie hapo ilipo.

Wasira akizungumzia juu ya suala la mfumo wa serikali mbili,  alisema si vyema kwa wajumbe wa bunge hilo kutumia nafasi zao kuwadanganya wananchi juu ya mfumo huo.

Alisema Tume ya Warioba, imeshindwa kufanya uchambuzi wa kina katika kuingiza sehemu kubwa ya mapato ya serikali ya Tanzania kuwa jambo la Muungano, na balada yake imeangalia baadhi ya wizara zinazoshughughulikia mambo ya Muungano.

Alisema mfumo wa serikali mbili una uwezo mkubwa wa kutanua biashara na masoko kwa mtu mmoja mmoja na waliowa chache bila ya kuwepo masharti ya uhamiaji na utapofanyiwa marekebisho utaweza kuondoa kero na manung’uniko yaliyopo sasa.

Alisema licha ya ubishi unaoendelea kutokea juu ya suala la gharama za uendeshaji wa serikali tatu  kuna uwezekano mkubwa serikali ya shirikisho ikaanguka, na kwamba hata Prof. Ibrahim Lipumba, amelikiiri hilo katika moja ya mada zake.

Alisema hali hiyo pia inajionesha kwa upande wa Tanzania Bara ambako kati ya watu 16,321 waliochangia hoja ya Muungano wa serikali tatu ni 8682 kutoka mkoa wa Kigoma ambao ni sawa na asilimia 52 na waliobakia kati  7,000 walitokea mikoa mengine ikiwemo Tabora, lakini anashangaa kuona tume kusema watu wengi wanataka muungano wa serikali tatu.

Alisema kama tume inaona ipo haja ya kuwa na mfumo huo wa serikali tatu basi ililazimika kwanza kupendekeza kuvunjika Muungano.

Akizungumzia juu ya maoni ya wachache, alisema sehemu kubwa ya maoni ya wajumbe hao walikubaliana na maoni ya Tume ya katiba.

Alisema katika maoni yao, waliorodhesha mambo manane ambayo yanaonekana kuwa na matatizo ya kisheria juu Muungano ikiwemo suala la kutunga sheria, msingi wa Muungano na utaifa, mgawanyo wa mambo yasiokuwa ya Muungano, bajeti na mambo ya fedha za muungano, udhaifu wa jumla wa mambo ya Muungano na rasilimali za Muungano.

Mjadala huo ulionekana kugeuka mwiba baada ya kuwepo msisitizo wa kuletwa hati ya Muungano.


Asha Mtwangwi alisema kinachoonekana baadhi ya wajumbe wanashindwa kufanya utafiti kabla ya kusema kwani wanasahau kuwa nchi haina uwezo wa kuhesabika kuwa nchi kama haina muhimili huku Amon Mpanji akisema bado Tanzania inahitaji amani katika mfumo wa serikali mbili.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.