Habari za Punde

Wanafunzi wa kike watakiwa kupuuza vishawishi

Na Anna Nkinda, Maelezo
WANAFUNZI wa kike wa vyuo vikuu nchini wametakiwa kujitambua na kufahamu wajibu wao kwa jamii inayowazunguka na kujiepusha na vishawishi vikiwemo vya ngono na kujikomboa  kifikra, kiutamaduni na kiuchumi.

Pia wametakiwa kujua thamani yao na kuepuka kutumiwa vibaya na kushinda majaribu ya watu wanaotaka kuivuruga safari yao ya maisha.

Wito huo umetolewa na mke wa Rais, mama Salma Kikwete, wakati akizungumza na wanafunzi wa kike wa vyuo vikuu waliohudhuria kongamano la mustakabali wa mtoto wa kike katika mazingira ya sasa lililofanyika katika ukumbi wa Chimwaga uliopo Chuo Kikuu cha Dodoma (UDOM).

Mama Kikwete ambaye pia ni Mwenyekiti wa Taasisi ya Wanawake na Maendeleo (WAMA), alisema kila mtu amepewa karama za kumuwezesha kufikia wito wa kutimiza ndoto zake ili kuweza kufanikisha hayo hana budi kujitambua, kuvitunza na kuvilea vipawa na karama zake na kuyakubali mapungufu yake katika kutimiza azma zake.


“Kataa kabisa mawazo ya kukatisha tamaa kwani hofu kama ilivyo furaha huuambukiza, jaribu kuwaepuka marafiki wenye mawazo ya kukatisha tamaa kwani hao ndiyo maadui wakubwa wa maisha yako na wa kukukwamisha kufikia malengo yako,” alisema.

“Kuna wakati inawezekana ukawa na hamu ya kuona malengo yako yanatimia mara moja ukweli ni kwamba hamu yako ya kuleta mabadiliko ya haraka yanaweza kukuletea madhara makubwa kuliko faida na hapa ndipo mabinti wengi huharibikiwa kwa sababu wanakosa subira na hivyo kufanya mambo yao kinyume na utaratibu na malengo,” aliasa.

Aliwahimiza wanafunzi hao kugombea nafasi mbalimbali za uongozi katika vyuo vyao kwa kufanya hivyo watajiwekea mazingira mazuri ya kuwa viongozi wa baadaye pindi watakapomaliza masomo.

 “Wanawake tuna nafasi ya pekee ya uongozi kwani sisi ndio wazazi na walezi tunaokabiliwa na changamoto nyingi, hivyo basi sisi tuna mchango wa pekee katika kutatua changamoto hizo lakini tutaweza kufanya hivyo kama tutaingia katika ngazi ya maamuzi jambo la muhimu ni kupendana na kuungana katika mambo ya maendeleo kwa ajili ya maslahi yetu kama wanawake,” alisema.

Akisoma risala ya wanafunzi hao, mwakilishi wa wanafunzi, Hamida Salum, alisema katika maisha suala la kujitambua ni la muhimu kwakuwa wanafunzi wengi wa elimu ya juu wanasoma bila ya kuwa na malengo hali inayosababishwa na kutojitambua.

 “Changamoto zinazomkabili mtoto wa kike ni nyingi baadhi ni kutokuwa na  elimu ya afya ya uzazi na jinsia jambo ambalo limesababisha wasichana wengi kujihusisha katika mahusiano yasiyo salama, dhana potofu ambayo imejengeka katika jamii kwamba wanawake hawawezi kuwa viongozi kiasi cha kuwaathiri hata watoto wa kike wenye uwezo wa kuongoza,” alisema.

Alisema sera nyingi za nchi zimemsahau mtoto wa kike katika mambo yanayomuhusu na hivyo kumfanya aonekane duni kwenye jamii.

Wanafunzi hao pia waliiomba serikali itazame upya sera ya utoaji wa mikopo kwa wanafunzi wa elimu ya juu hasa wasichana kwakuwawengi wao hawakidhi vigezo vya kupewa mikopo na wanahitaji kusoma hivyo wanafunzi wanaotoka katika familia zenye uwezo duni kiuchumi kushindwa kuendelea na masomo.


Kongamano hilo la siku moja  liliandaliwa na Chuo kikuu cha Dodoma na kuhudhuriwa na wanafunzi wa kike zaidi ya 3000 kutoka Chuo cha Elimu ya Biashara (CBE), Chuo kikuu cha Mt. John, Chuo kikuu Mzumbe, Chuo cha Mipango, Chuo cha Hombolo, Chuo cha Madini na Shule ya sekondari Dodoma.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.