Habari za Punde

Balozi Seif Akutana na Ujumbe wa Kampuni ya Aksh Opti Fibre na Balozi wa Israel Nchini Tanzania.

Na Othman Khamis OMPR.
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi alisema Zanzibar inaweza kupiga hatua kubwa katika uzalishaji wa chakula kwa kutumia mpango wa umwagiliaji iwapo wazalishaji wake watakuwa na taaluma ya kutosha katika kuendesha miradi hiyo.

Balozi Seif alieleza hayo hapo Ofisini kwake Vuga Mjini Zanzibar wakati akizungumza na Balozi wa Israel Nchini Tanzania Bwana Gil Haskel ambae amefika Zanzibar kuaga rasmi baada ya kumaliza muda wake wa utumishi wa kidiplomasia hapa Nchini.

Alisema kilimo cha umwagiliaji kimekuwa na tija kubwa na kumuomba Balozi Haskel kujaribu kuzishawishi taasisi za kilimo Nchini Israel kufikiria njia ya  kusaidia taaluma za kilimo hicho kwa vile nchi hiyo tayari imeshapiga hatua kubwa katika sekta ya kilimo Duniani.

Alisema uanzishwaji wa mradi maalum wa mafunzo ya kilimo hapa Zanzibar na Tanzania kwa ujumla kwa msaada wa wataalamu wa Israel ndio njia pekee itakayosaidia kuwakomboa wakulima walio wengi nchini kuondokana na kilimo cha asili.

Akizungumzia suala la kukabiliana na maafa hapa nchini Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif alimueleza Balozi wa Irael Nchini Tanzania Bwana Gil Haskel kwamba Serikali bado iko katika mchakato wa kuanzisha kituo maalum kitakachoshughulikia matukio yanayosababisha na maafa hapa nchini.

Naye Balozi wa Israel Nchini Tanzania Bwana Gil Haskel alisema Serikali ya Israel wakati wote iko tayari kugawa taaluma iliyonayo katika kuona nchi rafiki zinafaidika sambamba na taaluma hiyo.


Balozi Haskel alimuhakikishia Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar kwamba licha ya kumaliza muda wake wa utumishi hapa nchini lakini atalazimika kufanya juhudi za ziada katika kuona ile miradi iliyoanzishwa au kuahidiwa kati ya pande hizo mbili inashughulikiwa ipasavyo.

Wakati huo huo Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi alikutana na Uongozi wa Kampuni ya Mkongo wa Mawasiliano { Aksh Opti Fibre } yenye Makao Makuu yake katika Mji wa Dubai hapo Ofisini kwake Vuga Mjini Zanzibar.

Katika mazungumzo yao Mkurugenzi wa Kampuni hiyo Bwana Chetan Choudhari alimueleza Balozi Seif nia ya Kampuni yake kutaka kusaidia taaluma ya masuala ya mitandao ya mawasiliano ya Kisasa kwa kuanzisha vituo maalum vitakavyolenga kutoa huduma kwa wananchi wa maeneo ya Vijijini.

Bwana Chetan Choudhari alisema mradi kama huo ambao tayari unatumika na kuleta mafanikio makubwa katika visiwa vya Mauritius  umeundwa ili kuwajengea uwezo  wananchi wa vijijini katika harakati zao za kiuchumi na ustawi wa jamii.

Alisema wananchi wa  Vijijini  kupitia mradi huo watakuwa na taaluma ya mawasiliano katika miradi ya elimu ya afya, compyuta, huduma za umeme ambayo baadaye huwajengea uwezo wa kupata ajira na kuendesha maisha yao ya kila siku.

“ Ni huduma inayopangwa kutolewa katika vibanda maalum maarufu Kioski na kuhudumia wana vijiji wasiopungua 5,000 ikiwemo huduma za internet pamoja na matengenezo ya miundombinu “. Alisema Bwana Chetan Choudhari.

Akitoa shukrani zake Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi alimueleza Mkurugenzi huyo wa Aksh Opti Fibre Bwana Chetan kwamba Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar hivi sasa iko katika mikakati ya kutumia mfumo wa mtandao wa kisasa { E. Government } kwenye ofisi zake za Serikali.

Balozi Seif alisema mradi huo endapo utaanzishwa hapa Zanzibar utasaidia kuongeza nguvu za utendaji kupitia mfumo huo kwa kushirikisha moja kwa moja wananchi na Taasisi za Serikali na mashirika ya Umma.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.