Habari za Punde

Cheyo aikana ripoti ya Kamati Namba 11

Na Daniel Mjema, Mwananchi
 
Dodoma. Mjumbe wa Bunge la Katiba, John Cheyo juzi aliomba mwongozo wa mwenyekiti akidai kuwa taarifa iliyosomwa bungeni na Mwenyekiti wa Kamati namba 11, Anne Kilango ni tofauti na ile waliyoijadili.
Cheyo ambaye pia ni Mbunge wa Bariadi Magharibi (UDP), alisema: “Pamoja na heshima zote za mheshimiwa aliyeisoma (taarifa), lakini mimi nilikuwa mmojawapo wa wajumbe wa kamati ya 11. Mengi ambayo aliyosoma hatukuyazungumza,” alisema Cheyo na kuongeza:
“Sasa hii inatupa taabu tunafanyaje sasa? Maana yake sisi tumerekebisha mambo mengi, ya uraia tumesema pawapo na fursa ya uraia wa nchi nyingine, yote hayakusemwa.”
Cheyo alisema mambo muhimu hayakusemwa labda ni kwa sababu wajumbe wa kamati hiyo hawakupata fursa ya kuitwa na kuipitisha taarifa hiyo.
“Tungepata nafasi ya kuipitisha tungesema hili hapana, hili sawa,” alisisitiza Cheyo.
Hata hivyo, Mwenyekiti wa Bunge hilo, Samuel Sitta alisema tatizo huenda likawa ni muda, kwani mambo mengi yapo kwenye kitabu lakini kutokana na muda hayakusomwa.

“Tatizo ni muda tu, ukisoma hayo ya uraia kwenye kitabu hiki yapo tu. Mimi nadhani uwasilishaji tu kwa sababu tunakatiza, tunagonga kengele hapa, lakini ukitazama kwenye ukurasa wa 25 mpaka 26 mpaka 27 yapo,” alisema.
Jana, Katibu wa Bunge hilo, Yahaya Khamis Hamad alisema tatizo lilitokana na kamati ya Kilango kutofanya uhakiki wa maandishi na kuwa wameelezwa wahakikishe wanahakiki kazi yao kabla haijapelekwa kusomwa bungeni.
 
Chanzo: Mwananchi

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.