Habari za Punde

Dk. Shein awataka waganga tiba asili kuzingatia maadili

Na Khamis Haji, OMKR
Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Mhe. Dk. Ali Mohamed Shein, ametoa wito kwa waganga wa tiba asili nchini, kuzingatia maadili na taratibu za kazi zao na kuepusha madhara yanayoweza kuwakumba wananchi wanaowapa huduma.

Aliyasema hayo jana katika hotuba yake iliyosomwa kwa niaba yake na Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar, Mhe. Maalim Seif Sharif Hamad, wakati wa maadhimisho ya siku ya waganga wa asili barani Afrika, yaliyofanyika bustani ya Victoria, Mnazi mmoja mjini Zanzibar.

Alisema tiba asili na tiba mbadala inategemewa na wananchi wengi  barani Afrika na duniani kote, ambapo kwa Tanzania asilimia 60 ya wananchi wake imethibitishwa hupata tiba hiyo.

Alisema kutokana na haja iliyopo, waganga wa tiba asili hawana budi kufuata taratibu zilizowekwa na Baraza la Tiba Asilia katika kuhakikisha hawasababishi athari kwa wateja wanaofika kupata huduma wanazozitoa.

Alisema fani ya tiba asili itapata mafanikio na kunufaisha wananchi ipasavyo, iwapo waganga hao watashirikiana na waganga wa kisasa kuhakikisha matibabu yao yanathibitishwa 
kitaalamu na yana ubora unaohitajika.

Alisema serikali inathamini mchango unaotolewa na waganga hao na itahakikisha mamlaka zinazohusika na matibabu wanayoyatoa, zinapewa msukumo na kuwezeshwa kutekeleza 
majukumu yao kwa ufanisi zaidi.

Katika hafla hiyo, Rais wa taasisi ya tiba asili na tiba mbadala ya Afrika Mashariki, Kamuntu Matoke, aliahidi kuwa wataendelea kusimamia maadili na kuhimiza utunzaji wa miti asili ambayo 
imekuwa ikitegemewa na wananchi wengi kwa matibabu.


Hata hivyo, alisema ili waweze kutekeleza majukumu hayo kwa ufanisi na kufikia matarajio ya wateja wao, nchi za Afrika 
Mshariki zikiwemo Tanzania, Kenya na Uganda hazina budi kuwa na sera na sheria za tiba asili zenye lengo moja.

Mapema Mwenyekiti wa Baraza la Tiba Asili Zanzibar, Dk. Mayasa Salum, alisema  wanachukua juhudi kubwa kuhakikisha watu wote wanaofanya kazi za tiba asili na mbadala, wanasajiliwa na kupewa mafunzo ya kazi hizo.


Alisema hadi sasa Zanzibar kuna waganga asili 193 waliosajiliwa rasmi na wamekuwa wakinufaika na mafunzo mbali mbali yanayohusu utoaji wa huduma bora kwa wananchi.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.