STATE HOUSE ZANZIBAR
OFFICE OF THE PRESS SECRETARY
PRESS RELEASE
Zanzibar
28.10.2014
RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi
Dk. Ali Mohamed Shein amesema kuwa kufanikiwa kwa udhibiti na ukaguzi mzuri wa
fedha za serikali ndio silaha kubwa ya
maendeleo ya nchi.
Dk. Shein aliyasema
hayo leo wakati alipofanya mazungumzo na aliyekuwa Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa
Hesabu za Serikali wa Tanzania, Bwana Ludovick Utoh aliyefika Ikulu mjini
Zanzibar kusalimiana na Rais pamoja na kumuaga rasmi baada ya kumaliza muda
wake wa kazi.
Katika maelezo
yake Dk. Shein alimueleza Bwana Utoh kuwa mafanikio makubwa yameweza kupatikana
katika Serikali zote mbili ile ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania pamoja na
Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar kutokana na usimamizi mzuri wa fedha za umma.
Dk. Shein alisema
kuwa fedha ndio jambo kubwa katika kuendesha serikali, hivyo iwapo usimamizi na
udhibiti wake utafanyika vizuri, mafanikio pamoja na maendeleo endelevu yanaweza
kupatikana kwa ufanisi mkubwa.
Aidha, Dk. Shein
alimpongeza Bwana Utoh kwa utendaji kazi wake mzuri katika kipindi chake chote
cha kazi ndani ya miaka minane aliyoitumikia afisi hiyo sambamba na kuonesha
mashirikiano mazuri kati ya afisi yake na afisi ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za
Serikali wa Zanzibar.
Sambamba na hayo,
Dk. Shein alisifu mabadiliko makubwa yaliyopatikana chini ya uongozi wa Bwana
Utoh katika afisi hiyo kwani alianza kazi vizuri sambamba na mikakati
aliyoiweka katika kufikia malengo yaliokusudiwa na serikali hatua ambayo
matunda yake yameonekana. “Hakuna atakaesahau juhudi zako”alisema Dk. Shein.
Nae Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za
Serikali wa Tanzania Mstaafu Bwana Ludovick Utoh alitoa shukurani zake kwa Dk. Shein na
kumpongeza kwa kumpa mashirikiano mazuri tokea akiwa Makamu wa Rais wa Jamhuri
ya Muungano wa Tanzania hadi hivi leo akiwa Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa
Baraza la Mapinduzi.
“Nashukuru kwa
mashirikiano yako mazuri uliyonipa Mhe. Rais,
katika muda wangu wote wa kazi katika afisi hii, tokea siku ile
niliyoapishwa hadi kustaafu kwangu, nashukuru sana... kwani fedha ya umma zinahitaji
usimamizi mzuri...fedha za umma sio shamba la mtu”alisema Bwana Utoh.
Aidha, Bwana Utoh
alimpongeza Dk. Shein kwa kuiimarisha vyema afisi ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu
wa Hesabu za Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar hatua ambayo imeipelekea
Zanzibar kuendelea kupata maendeleo makubwa.
Bwana Utoh
alisisitiza kuwa katika suala zima la udhibiti, ukaguzi na usimamizi wa fedha
za umma, uwajibikaji ndio jambo la msingi kwani bila ya uwajibikaji fedha za
umma hazifikii malengo yaliokusudiwa huku akimwagia sifa Dk. Shein kwa
kufanikiwa kulisimamia hilo katika uongozi wake.
Bwana Utoh
alisema kuwa mafanikio makubwa yameweza kupatikana hasa katika uimarishaji wa
Serikali za Mitaa, usimamizi na udhibiti wa fedha za umma sambamba na ujenzi wa
majengo kwa ajili ya shughuli za afisi hiyo katika maeneo mbali mbali Tanzania
Bara.
Alieleza kuwa
katika kipindi chote cha uongozi wake, mashirikiano makubwa yameweza kupatikana
kati ya afisi hiyo na ile ya Zanzibar na kutoa pongezi kwa Rais Dk. Shein kwa
ujenzi wa jengo la kisasa la afisi ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za
Serikali hapa Unguja sambamba na ujenzi wa afisi kama hiyo huko kisiwani Pemba.
Rajab Mkasaba, Ikulu
Zanzibar
Postal Address: 2422 Tel.:0777427449. Fax: 024
2231822
E-mail:
rajabmkasaba@yahoo.co.uk
No comments:
Post a Comment