Habari za Punde

DK.Shein Azungumza na Uongozi wa Kampuni ya ZANCHICK.

Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi DK.Ali Mohamed Shein akisalimiana na Kiongozi wa Kampuni ya ZANCHICK inayojishuhulisha na biashara ya Kuuza  Kuku  (Perdue)kutoka Marekani  Dk.David Elua akiwa na ujumbe wa kampuni hiyo ulipofika Ikulu Mjini Unguja jana kwa mazungumzo
Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi DK.Ali Mohamed Shein akizungumza na Uongozi wa Kampuni ya ZANCHICK inayojishuhulisha na biashara ya Kuuza  Kuku (Perdue) kutoka Marekani unaoongozwa na  Dk.David Elua  katika ukumbi wa  Ikulu Mjini Unguja jana .[Picha na ramadhan Othman Ikulu.]

STATE HOUSE ZANZIBAR
OFFICE OF THE PRESS SECRETARY
PRESS RELEASE
  Zanzibar                                                                                                                                    1.10.2014
---
RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Mhe.Dk. Ali Mohamed Shein ameeleza kuwa hatua ya Kampuni ya ZANCHICKS kuekeza Zanzibar zitaweza kufikisha malengo ya uekezaji hapa nchini  sambamba na kuinua soko la ajira na kukuza uchumi.

Dk. Shein aliyasema hayo leo wakati alipofanya mazungumzo na uongozi wa Kampuni ya ZANCHICK huko Ikulu mjini Zanzibar. Kampuni ambayo kwa hivi sasa inajishughulisha na uagizaji wa malighafi zake kutoka nje ambazo ni nyama ya kuku na kuuza hapa nchini.

Katika maelezo yake Dk. Shein aliueleza uongozi huo kuwa miongoni mwa azma na malengo la Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar kuinua sekta ya uekezaji ni kuhakikisha wananchi wake wanapata ajira hatua ambayo pia, itachochea ukuaji wa uchumi wa nchi.

Dk. Shein alisema kuwa kuanzisha biashara ya nyama ya kuku hapa nchini kunatoa fursa kwa wananchi kutumia chakula hicho ambacho kimekuwa na walaji wengi hivi sasa sambamba na kuimarika kwa wafanyabiashara hiyo hapa Zanzibar.

Aidha, Dk. Shein aliueleza uongozi huo haja ya kutoa ushirikiano na msaada mkubwa kwa wafanyabiashara wa aina hiyo wazalendo hapa Zanzibar ambao nao pia, wanahitaji kuimarika zaidi kibiashara kama ilivyo kwa kampuni hiyo hivi sasa.

Dk. Shein alisisitiza kuwa hatua hiyo itawasaidia kwa kiasi kikubwa wafanyabiashara wazalendo kuweza kuimarika kibiashara hali ambayo itasaidia lengo la Serikali ya Mapinduzi Zanzibar katika kupambana na umasikini pamoja na kufikia lengo la Dira 2020 katika ukuaji uchumi wa Zanzibar.

Pamoja na hayo, Dk. Shein aliueleza uongozi huo kuwa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar kupitia Wizara pamoja na Taasisi zake husika zitaendelea kutoa ushirikiano wake kwa Kampuni hiyo ili kuhakikisha inaendelea kufanya shughuli zake kwa ufanisi zaidi.
  
Dk. Shein aliueleza uongozi huo kuwa soko la biashara hiyo kwa hapa nchini ni kubwa sana hivyo, jambo kubwa linalohitajika ni kuendeleza na kupanua soko la biashara hiyo ili Kampuni hiyo iweze kupata mafanikio zaidi na kufikia lengo ililojiwekea katika biashara zake.

Sambamba na hayo, Dk. Shein aliueleza uongozi huo kuwa katika biashara yoyote ile suala la ushindani wa kibiashara haliepukiki hivyo, ni jambo la busara kwa Kampuni hiyo kufanya biashara zake kwa kuwavutia watumiaji pamoja na kutoa ushirikiano kwa jamii.

Nae kiongozi wa Kampuni hiyo Dk. David Elua alimueleza Dk. Shein kuwa Kampuni yake imeweza kupata mashirikiano mazuri kwa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar kupitia Wizara husika na Taasisi zake zote na kupongeza kwa hatua hiyo ambayo imeiwezesha Kampuni ya ZANCHICK kufanya shughuli zake kwa ufanisi mkubwa hapa Zanzibar.

Dk. Elua alieleza kuwa Kampuni yake kwa hivi sasa tayari imeshatoa ajira kwa vijana zaidi ya 300 wa hapa Zanzibar wakiwemo wanaofanya kazi kiwandani pamoja na wasambazaji wa bidhaa zake.

Aidha, kiongozi huyo, alimueleza Dk. Shein azma ya Kampuni ya ZANCHICKS ambayo imeanza shughuli zake hapa nchini mnamo mwaka 2011, kuanzisha Kiwanda cha kusarifu bidhaa za kuku na kusafirisha nje ya nchi sambamba na kupanua zaidi soko la ajira kwa wananchi wa Zanzibar.

Kiongozi huyo wa Kampuni ya ZANCHIKS yenye Makao Makuu yake nchini Marekani alieleza kuwa Kampuni hiyo inafanya biashara zake katika maeneo mbali mbali duniani pia, alieleza kuwa  taratibu za utayarishaji wa kuku hao ni halali.

Sambamba na hayo, Dk. Elua alieleza mafanikio yaliopo katika shughuli za Kampuni hiyo hapa Zanzibar na kueleza azma ya Kampuni yake kupanua zaidi soko la nje ya nchi licha ya baadhi ya changamoto zilizopo.

Rajab Mkasaba, Ikulu Zanzibar
Postal Address: 2422 Tel.:0777427449. Fax: 024 2231822 
 E-mail: rajabmkasaba@yahoo.co.uk


No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.