Na Fatuma Kitima, Dar es Salaam
Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC)
imesema zoezi la majaribio la uimarishaji wa daftari la kudumu la wapiga kura,
linatarajia kuanza katikati ya Novemba mwaka huu.
Zoezi hilo litafanyika kwa
kutumia mfumo mpya wa biometric voter registration (BVR) katika majimbo matatu
ya uchaguzi ambayo ni Kawe manispaa ya Kinondoni, Kilombero, halimashauri ya
mji wa Kilombero na Mlele, halimashauri ya
Mlele, ambapo vituo vya uandikishaji
vimewekwa katika kata zilizomo kwenye majimbo husika.
Makamu Mwenyekiti wa NEC, Jaji
Mkuu (mstaafu) wa Zanzibar, Hamid
Mahamoud, alisema hayo wakati
akisoma taarifa kuhusu kuanza kwa shughuli za uimarishaji wa daftari
hilo katika mkutano na waandishi wa
habari uliofanyika jijini Dares Salaam.
“Tume tayari imekwishapokea baadhi ya vifaa
muhimu vya uandikishaji zikiwemo fomu za undikishaji, hivyo kinachosubiriwa ni
kupokea BVR 250 zinazotarajiwa kufika wakati wowote kuanzia leo. Zoezi la
uandikishaji litakapoanza, vituo vitafunguliwa kuanzia saa 2:00 asubuhi na
kufungwa saa 12:00 jioni, vyama vya siasa vinaruhusiwa kuweka mawakala wao
katika kituo ili kushuhudia jinsi uandikishaji utakavyofanyika,” alisema.
Alisema baada ya zoezi hilo
kukamilika, litaendelea katika maeneo mengine ya nchi.
“Tunatarajia uimarishaji wa
daftari la kudumu la wapiga kura utafanyika kwa wakati mmoja katika mikoa yote
nchini isipokuwa mkoa wa Dares Salaam na Zanzibar. Uandikishaji katika mikoa ya
Dares Salaam na Zanzibar utafanyika baada ya uandikishaji katika mikoa yote
kukamilika. Muda wa uandikishaji utakuwa
ni siku saba katika kila kituo,” alisema.
Alisema uandikishaji katika
mikoa yote utaanza Januari, mwakani hadi katikati ya Februari wakati mikoa ya Dar es Salaam na
Zanzibar utafanyika mwishoni mwa mwezi Februari.
Alisema uandikishaji huo utafanyika kwa awamu
nne kwenye kila halimashauri ili kutoa fursa ya kuhamisha vifaa vya
uandikishaji kutoka eneo moja kwenda
jingine.
Alisema wapiga kura wa zamani
yaani wale ambao walikuwa wamejiandikisha katika daftari la zamani, watatakiwa
kwenda katika vituo vya kujiandikisha vilivyoko karibu na maeneo wanayoishi
kuchukuliwa taarifa zao hasa alama za vidole, picha na saini zao kuingizwa
katika mfumo BVR na kupewa vitambulisho.
Alisema wenye kadi za kupiga
kura za zamani watatakiwa kwenda na kadi zao katika kituo cha kujiandikisha ili
kurahisisha zoezi la kuhamisha taarifa zao.
Kwa wapiga kura waliopoteza
kadi au wale ambao kadi zao zimeharibika watatakiwa kwenda kituoni ili
kujiandikisha na kupewa kadi mpya.
Alisema wapiga kura wenye
vitambulisho vya taifa kutoka Dares Salaam na Zanzibar wanatakiwa kwenda na
vitambulisho vyao ambavyo vitasomwa na vifaa maalum ili kupunguza muda
utakaotumika kuhamisha taarifa zao.
Alisema uimarishaji huo unahusu
pia kuandikisha wapiga kura wapya waliotimiza umri wa miaka 18 au zaidi na wale
ambao ifikapo siku ya upigaji kura ya maoni na uchaguzi mkuu wa mwaka 2015
watakuwa wametimiza miaka 18.
Alisema jumla ya watu milioni
23.09 wenye umri wa miaka 18 na zaidi wanatarajiwa kuandikishwa.
Alitahadharishwa kwamba mpiga
kura atakaesajiliwa kwenye buku hilo ndie atakaeruhusiwa kupiga kura.
Naye Mkurugenzi wa uchaguzi, Julias
Malaba, alisema shilingi bilioni 15 zimetolewa kwa ajili ya zoezi hilo.
Daftari hilo linatarajiwa kukamilika Aprili 14 mwakani na litawekwa wazi
kwa muda wa siku tano katika maeneo yanayohusika ili kumwezesha kila mtu aliyejiandikisha aende
kukagua taarifa zake.
Akizungumzia mfumo wa BVR,
alisema unasaidia kupunguza ujiandikisha mara mbili na kuwa na taarifa sahihi.
No comments:
Post a Comment