Habari za Punde

Nchi 188 zapiga kura ya ndio kutaka Cuba iondolewe vikwazo

Naibu Mwakilishi wa Kudumu wa Tanzania katika Umoja wa Mataifa, Balozi Ramadhan Mwinyi, akizungumza muda mfupi kabla wajumbe wa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa hawajapigia kura ya  kutaka vikwazo vya kiuchumi,  kibiashara na kifedha ambavyo Marekani imeiwekea Cuba viondolowe. Nchi 188 zilipiga kura ya ndiyo, mbili zilipiga kura ya hapana na  tatu zilipiga kura ya kutofungamana na upande wowote
 
Na  Mwandishi Maalum , New York
 Kwa mwaka wa 23 sasa  hapo  jana (  Jumanne ) Nchi wanachama wa Umoja wa Mataifa  wamepigia kura  Azimio linaloitaka Marekani  iondoe vikwazo vya kiuchumi,  kibiashara na kifedha dhidi ya  Cuba.
Katika   upigaji kura  huo ,  nchi  188  ikiwamo Jamhuri ya Muungano wa Tanzania  zilipiga kura ya ndiyo   Azimio hilo  ambalo liliwasilishwa mbele ya wajumbe  na Waziri wa Mamb ya Nje wa Cuba, Bw.  Bruno Rodriquez Parrilla
Marekani  na Israel zenyewe zilipiga kura ya hapana, huku   Micronesia, Marshall Islands na Palau  wakipiga kura ya kutoegemea upande wowote ( abstentions).
Akizungumza  kabla ya  upigaji kura huo kufanyika,  Naibu Mwakilishi wa Kudumu  wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Balozi Ramadhan Mwinyi aliungana na wazungumzaji wengine katika  kuitaka Marekani   na Cuba  kumaliza tofauti zao  za kidiplomasia  ili waweze kushirikiana  na nchi nyingine katika kuzitafutia ufumbuzi changamoto mbalimbali zinazomkabili mwanadamu.
Akasema  dunia imeshuhudia namna gani mataifa mengi yalivyojitoa  muhanga zikiwamo Cuba na Marekani ambapo wamepeleka wataalamu wao wa afya, wanajeshi na  vifaa ili kuukabili ugonjwa wa Ebola katika nchi  za  Liberia,  Sierra Leone na Guinea ambazo zimeathirika vibaya  kwa ugonjwa huu.
Akasisitiza kuwa mlipuko huo  wa Ebola umethihirisha namna gani mataifa yanavyoweza kushirikiana na kufanya kazi kwa pamoja na kwamba  mataifa yanatakiwa  kujenga  mshikamano imara dhidi  ya maadui wa binadamu na siyo kupingana wenyewe kwa wenyewe.
Balozi  Mwinyi akaongeza kuwa   Tanzania  ambayo ni  nchi rafiki kwa Marekani na Cuba, kwa mara nyingine inasikitika  kusimama na  kuzungumzia kuhusu vikwazo hivyo ambavyo licha ya maazimio mengi kupitishwa na Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa. Bado vikwazo vinaendelea.
Vile vile  Balozi Mwinyi  amesema hali ya kuendelea kwa vikwazo hivyo kunasikitisha kutokana na sababu kuu mbili za msingi. Kwanza  kuchelewa kulipatia ufumbuzi tatizo hilo kunadhoofisha hadhi ya  Umoja wa Mataifa, chombo chenye dhamana ya kuhifadhi Amani  na usalama wa kimataifa,  kuhuisha haki za binadamu, uchumi na ustawi wa wote.
Akasema inaposhindikana kutekelezwa kwa maazimio yanayopitishwa   na Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa ni kushindwa kwa   wanachama wote.
Sababu ya pili ambayo  amesema inasikitisha  ni  kuona kuwa Nchi ambayo ilikuwa mwazilishi wa Umoja wa Mataifa ( Marekani) inaendelea kupuuza wito ambao umekuwa ukitolewa mara kwa mara, wito unaotolewa wanachama wa  Umoja wa Mataifa wa kutaka kusitishwa mara moja na bila masharti yoyote vikwazo dhidi ya Cuba.
“ Tatizo hili ( vikwazo) linaweza kuwa ni la kati ya nchi hizo mbili. Lakini  kuendelea kwake na   muda mrefu kunavuka  mipaka ya nchi hizi mbili” akasema Balozi Mwinyi
 

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.