Na Kija Elias, Moshi
Watu saba wamefariki dunia mkoani
Kilimanjaro, akiwemo mzee mwenye umri wa miaka 83, katika kipindi cha kuanzia
Januari hadi Oktoba mwaka huu, baada ya kunaswa na umeme kutokana na
kujiunganishia umeme kinyume cha sheria.
Mzee huyo aliefahamika kwa jina la
Thadei Mushi, mkazi wa Otaruni kata ya Kibosho kati, alifariki wakati
akijiunganishia umeme kutoka kwenye nyumba ya mtoto wake, baada ya nyumba yake
kukatiwa umeme kutokana na kulimbikiza madeni.
Mhandisi Mthibiti wa Mapato wa Shirika
la Umeme (TANESCO) mkoa wa Kilimanjaro, Bakabuje Joseph, alisema
kumekuwepo na wizi mkubwa wa umeme na miundombinu ya umeme hali iliyoisababishi
shirika hasara ya zaidi ya shilingi milioni 110.
Akizungumza na waandishi wa habari ofisini
kwake, alisema wananchi wengi wamekuwa na tabia ya kujiunganishia umeme
kinyume na taratibu jambo ambalo linasababisha wengine kupoteza maisha.
Aidha alisema shirika linahujumiwa
kutokana na miundombinu yake kuharibiwa ambapo wezi wamekuwa wakikata waya
zenye shaba na kuziuza kama nyuma chakavu.
Aidha, alisema wizi hao wamekuwa
wakiiba mavuta ya transfoma hali inayosababisha hasara kubwa kwa shirika.
Naye mtoto wa marehemu, Venance
Mushi, alisema kifo cha baba yake, kimesababishwa na hitilafu za umeme wakati
akijiunganishia huduma hiyo.
No comments:
Post a Comment