Habari za Punde

ZBS watakiwa kuainisha vipaumbele

STATE HOUSE ZANZIBAR
OFFICE OF THE PRESS SECRETARY
PRESS RELEASE
    Zanzibar                                                    28 Oktoba, 2014
TAARIFA KWA VYOMBOVYA HABARI
Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Ali Mohamed Shein ameitaka Taasisi ya Viwango Zanzibar-ZBS kuainisha vipaumbele vitakavyoiwezesha kutekeleza majukumu yake hatua kwa hatua kwa kuzingatia ubora wa huduma inazitoa kwa taasisi na jamii.
 
Akizungumza na Bodi ya Taasisi hiyo ofisini kwake Ikulu leo, Dk. Shein alisema kutokana na uchanga wake, taasisi hiyo haiwezi kuanza kutekeleza majukumu yote iliyopangiwa kwa wakati mmoja hivyo haina budi kuainisha maeneo maalum ambayo itayaona kuwa ni muhimu kuanza nayo ili kuyatafnyia kazi na kuanza kutoa huduma.
 
“Lazima muainishe vipaumble vyenu na kujua ni bidhaa gani muhimu mtakazoanza nazo ili muanze kwa ufanisi na kuweka viwango vinavyokubalika kimataifa” Dk. Shein alisema.
 
Aidha, aliieleza bodi hiyo iliyoongozwa na Mwenyekiti wake Profesa Mshimba, kuwa ili ZBS iweze kutekeleza majukumu yake ipasavyo ni lazima iwe na maabara zake zenye vifaa vya kisasa.
 
Hata hivyo aliishauri Taasisi hiyo kwa sasa ambapo bado haijawa na maabara zake wenyewe waanze kwa kutumia maabara za Serikali na taasisi zake zilizopo Zanzibar na Tanzania Bara ili iweze kutekeleza majukumu yake.
 
“Tunazo maabara za taasisi zetu za Serikali hapa Zanzibar... kama Mkemia Mkuu wa Serikali, Kituo cha Utafiti wa Kilimo Kizimbanzi, Bodi ya Chakula na Dawa na nyinginezo” alizitaja Dk. Shein na kusisitiza kuwa maabara za taasisi hizo zina vifaa vya kisasa na wataalamu waliobobea.
 
Kwa hivyo, alihimiza ushirikiano wa karibu kati ya Wizara zinazohusika na Biashara na viwanda za Serikali ya Muungano na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar pamoja na Taasisi ya Viwango Zanzibar na Taasisi ya Viwango Tanzania –TBS ili kuiwezesha ZBS kufanya shughuli zake kwa ufanisi.
 
Dk. Shein pamoja na kuipongeza Bodi hiyo kwa kazi nzuri iliyoifanya katika kipindi cha miaka miwili tangu kuanzishwa kwa taasisi hiyo, aliishauri pia ZBS kuweka utaratibu wa kufanya uthibiti wa nje wa viwango wa bidhaa (external quality control) wanazipitisha ili kuhakikishs bidhaa hizo zinakubalika kwenye masoko yote.
 
Akitoa taarifa ya Bodi ya ZBS kwa kipindi cha Septemba 2012/2013 hadi Septemba 204/2015 Mwenyekiti wa Bodi hiyo Profesa Ali Seif Mshimba alitaja mafanikio ya taasisi hiyo katika kipindi hicho kuwa ni pamoja  kukamilisha kanuni tatu muhimu za kusaidia utekelezaji wa Sheria ya Viwango ya Zanzibar ya mwaka 2011.
 
Alizitaja kanuni hizo kuwa ni utoaji wa Cheti cha Ubora kwa bidhaa zinazozalishwa Zanzibar(The Zanzibar Standards-certification-Regulations-2014), Upimaji wa Bidhaa (The Zanzibar Standard-Tested Products- Regulations,2014) na Udhibiti wa Ubora wa Bidhaa zinazoingia nchini kutoka nje(The Zanzibar Standards-Compulsory Batch Certification of Imports-Regulations, 2014).
 
Aidha taasisi hiyo alieleza kuwa imeweza katika kipindi hicho kuandaa viwango 23 ambavyo vimeshafikia hatua ya kutangazwa na kuanza kutumika huku viwango vingine 17 vikiwa vimeshajadiliwa na kukubaliwa na kamati za kitaalamu ambavyo sasa vinasubiri idhini ya Bodi.
 
Mkutano huo ulihudhuriwa pia na Naibu wa Waziri wa Biashara, Viwanda na Masoko Thuwaiba Kisasi na Mshauri wa Rais masuala ya Ushirikiano wa Kimataifa, Uwekezaji na Uchumi Balozi Mohamed Ramia Abdiwawa.
 
Postal Address: 2422 Tel.+255 776 613 015, Fax: 024 2231822 

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.