Habari za Punde

Dk Shein azindua maonyesho ya Fursa za ajira na uzalishaji kwa vijana



STATE HOUSE ZANZIBAR
OFFICE OF THE PRESS SECRETARY

PRESS RELEASE

    Zanzibar                                                                               22 Novemba,2014

---

TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI

SERIKALI ya Mapinduzi Zanzibar imekuwa ikichukua juhudi mbali mbali zinazolenga kujenga mazingira yatakayowawezesha vijana kuimarisha fursa za ajira ikiwa ni utekelezaji wa mipango mikuu ya maendeleo pamoja na kuridhia na kutekeleza mipango inayoendelea kupangwa na taasisi za Kimataifa.

Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Ali Mohamed Shein aliyasema hayo leo katika ufunguzi wa maonyesho ya Fursa za Ajira na Uzalishaji kwa Vijana, yaliyofanyika huko katika hoteli ya Bwawani mjini Zanzibar.

Katika maelezo yake Dk. Shein alisema kuwa Serikali imekuwa ikisiamamia utekelezaji wa Sera ya Ajira ya Zanzibar ambayo inatilia mkazo suala la kuwashajiisha vijana kujiajiri wenyewe na kujenga mazingira mazuri ili vijana wanawake na wanaume wapatiwe nyezo muhimu za kuansiha na kuimarisha biashara na shughuli nyengine za kuendesha maisha yao.

Dk. Shein alisema kuwa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar imelipa kipaumbele suala la maendeleo ya vijana, ikiwemo suala zima la uimarishaji wa fursa za ajira, ili nguvu kazi ya taifa iweze kutumika vyema katika kuleta maendeleo ya kiuchumi na kijamii.

“Serikali ya Mmapinduzi Zanzibar katika awamu zake zote tangu yaliopofanyika Mapinduzi Matukufu ya Zanzibar ya mwaka 1964, imekuwa ikizingatia sana suala la maendeleo ya vijana na nafasi katika jamii... Awamu ya saba, imekuwa ikipanga na kutekeleza mipango mbali mbali yenye lengo la kuimarisha ystawi na fursa za vijana”,alisema Dk. Shein

Aidha, Dk. Shein alisema kuwa serikali imechukua hatua za kuansiha mifuko mbali mbali kwa lengo la kupata fedha na kuwasaidia vijana ili waweze kujiajiri wenyewe ambapo imeanzisha Mfuko wa uwezeshaji ambao aliuzindua tarehe 21 Decemba, 2013 na tayari vikundi mbali mbali vya Unguja na Pemba vimeanza kupata mikopo.

Dk. Shein  aliwafahamisha vijana na wananchi kuwa Serikali inaendelea kutafuta njia bora za kuimarisha mafunzo ya amali pamoja na kuhamasisha mabadiliko katika Sera ya Elimu kwa lengo la kuhakikisha kuwa elimu inayotolewa inawaongoza vijana katika ubunifu wa mbinu bora za kujiajiri wenyewe.

Katika maelezo yake Dk. Shein alisema kuwa Serikali itachukua hatua za maandalizi ya awali katika kutafuta uwezekano wa kuchimba mafuta hapa Zanzibar na vijana wana fursa nzuri ya kunufaika na ajira mbali mbali zitakazokuwepo na kueleza hatua zilizofikiwa juu ya suala hilo.

Alieleza kuwa kwa kutambua mahitaji ya utaalamu na nguvu kazi inayohitajika katika sekta ya mafuta na gesi, jambo la kwanza la kulifanyia kazi ni kuanza kuwatayarisha vijana, ili wakati utakapowadia wawe mstari wa mbele katika kuitumikia na kuiongoza sekta hiyo.

Dk. Shein alisisitiza kuwa katika Makubaliano ya Awali waliyotiliana saini na Kampunin ya SHELL kutoka Uholanzi ni kuwapatia mafunzo ya muda mrefu na mfupi vijana wa Kizanzibari ili kujenga nguvu kazi iliyopo yenye utaalamu na maarifa yanayokwenda sambamba na  mahitaji ya sekta hiyo na mipango ya nchi ambapo tayari vijana 19 wanasomea fani ya mafuta na gesi.

Pamoja na hayo, Dk. Shein  alitoa ushauri kwa vijana kuwa mstari wa mbele katika kuunga mkono juhudi za Serikali kwa kuonesha uzalendo na ari ya kujifunza mambo mbali mbali wanayotayarishiwa na Serikali yao.

Aidha, alisema kuwa maonyesho hayo ni miongoni mwa mikakati ya Serikali ya kukabiliana na tatizo la ajira kwa vijana na kuona fursa zilizopo hasa wakati huu ambapo tatizo la ajira kwa vijana limekuwa ni changamoto kubwa kwa takriban Serikali za nchi zote duniani.

Alisema kuwa tatizo la ukosefu wa ajira kwa vijana linaonekana kuwa kubwa zaidi kwani kwa mujibu wa utafiti huo, Zanzibar inakisiwa kuwa na asilimia 17 hadi 18 ya vijana wenyewe umri kati ya miaka 15-24 wasiokuwa na ajira ambapo pia, Dk. Shein alitumia fursa hiyo kuwataka vijana kutochagua kazi.

Aliwasihi vijana kutofuata mambo mabaya wala wasishawishiwe kuingia katika mambo hayo maovu na badala yake washawishike kuingia kwenye mambo mazuri ikiwa ni pamoja na kutafuta njia za kuweza kujiajiri, kuwa na busara kwani wanahitajika kuanza familia zao huku akiwasisitiza kuisikiliza serikali yao.

Dk. Shein alitumia fursa hiyo kutoa pongezi kwa taasisi taasisi zote za serikali na binafsi zilizohusika pamoja na Shirika la Huduma za Kujitolea (VSO) kwa kazi kubwa ya kufanikisha maonyesho hayo, pia alitoa pongezi kwa Shirika la SHELL kwa kuiunga mkono Zanzibar.

Mapema Dk. Shein alikagua maonyesho yalioandaliwa kwa mantiki ya kuonesha fursa za ajira na uzalishaji kwa vijana na kupata maelezo kutoka kwa wahusika ambapo nae alitumia fursa hiyo kupongeza kutokana na juhudi zao hizo sambamba na ushiriki wao mkubwa.

Nae Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais Kazi na Utumishi wa Umma Mhe. Haroun Ali Suleiman kwa niaba ya Waziri wa Uwezeshaji, Ustawi wa Jamii, Vijana Wanawake na Watoto alisema kuwa hatua hiyo ni utekelezaji wa Dira ya Maendeleo 2020 sambamba na kukuza uchumi na kupunguza umasikini MKUZA  huku akieleza umuhimu wa vijana katika jamii.

Nae Mwenyekiti wa Shirika la SHELL International  Bwana Axel Knospe na Mkurugenzi Mkaazi wa VSO Bwana Jean Van Wetter walitumia fursa hiyo kutoa pongezi kutokana na juhudi za Serikali ya Mapinduzi Zanzibar katika kupambana na tatizo la ajira kwa vijana huku wakiahidi kuendelea kuunga mkono juhudi hizo.

Nao vijana wakitoa neno lao la shukurani walipongeza juhudi za Serikali ya Mapinduzi Zanzibar chini ya uongozi wa Dk. Shein pamoja na nasaha zake alizowapa sambamba na juhudi za Serikali katika uwezeshaji na uimarishaji wa ajira kwa vijana, kuwepo kwa Baraza la Vijana, huduma rafiki kwa vijana na uimarishaji na upatikanaji wa elimu ya juu na vyuo vya amali.

Dk. Shein pia alikabidhiwa Ripoti ya Idadi ya watu duniani na Dk. Lutosho Dadi kutoka UNFPA ambapo kabla ya kumkabidhi Dk. Dadi alieleza kuwa hivi sasa vijana wameweza kufikia Bilioni 1.3 duniani ambapo kwa upande wa Zanzibar Sensa ya mwaka 2012 ilionesha kuwa vijana wa Zanzibar ni asilimia 77 chini ya umri wa miaka 35 na kueleza kuwa juhudi za makusudi zinahitajika katika kuwaletea maendeleo vijana.

Viongozi mbali mbali walihudhuria katika maonyesho hayo, akiwemo Spika wa Baraza la Wawakilishi Mhe. Pandu Ameir Kificho, Mawaziri mbali mbali, Makatibu Wakuu,Wawakilishi wa Mashirika ya Maendeleo pamoja na vijana na wananchi na wajasiria mali mbali mbali.

Rajab Mkasaba, Ikulu Zanzibar

Postal Address: 2422 Tel.:0777427449. Fax: 024 2231822
E-mail: rajabmkasaba@yahoo.co.uk

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.