Habari za Punde

Dk Shein : Viongozi wa kuchaguliwa washirikiane na wanachama kuimarisha chama

 
STATE HOUSE ZANZIBAR
OFFICE OF THE PRESS SECRETARY
PRESS RELEASE
    Zanzibar                                                          20 Novemba, 2014
TAARIFA KWA VYOMBOVYA HABARI
 
Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Ali Mohamed Shein amewakumbusha viongozi waliochaguliwa kupitia Chama cha Mapinduzi kuwa wanawajibu kushirikiana na wanachama wenzao kukiimarisha chama hicho katika kila ngazi.
 
“Viongozi hawa (wabunge na wawakilishi)tumewapitisha katika vikao vyetu na kuchaguliwa na wananchi hivyo wana wajibu wa kuendelea kukitumikia chama na kwa umoja wetu kushirikiana kukijenga na kukiimarisha kwa nguvu zetu sote” Dk. Shein amesema.
 
Dk. Shein ametoa wito huo leo wakati alipokuwa akizungumza na mabalozi wa nyumba kumi na wenyeviti wa maskani za chama hicho wa wilaya ya kichama ya Dimani mkoa wa kichama wa Magharibi, Unguja katika mfululizo wa mikutano yake na viongozi hao katika wilaya za Unguja na Pemba.
 
Alisema kuwa viongozi hao wanapaswa pia kushiriki kikamilifu katika shughuli za maendeleo katika maeneo yao ikiwemo kuchangia miradi ya maendeleo na shughuli nyingine za wananchi na wanapaswa kuwapimwa kwa kuzingatia ufanisi na ushiriki wao katika shughuli hizo.
 
Dk. Shein aliwaambia viongozi hao kuwa lengo la mikutano hiyo ni kuimarisha chama hicho kwa kuzungumzia mambo muhimu yeye mustakabala wa Chama cha Mapinduzi na maedeleo ya Zanzibar.
 
Kwa hivyo aliwataka viongozi katika ngazi mbali mbali za uongozi kuitisha vikao kama Katiba ya chama hicho inavyoelekeza kuzungumzia masuala yote ya maendeleo ya chama hicho pamoja na kushughulikia hitilafu zinapotokea miongoni mwa viongozi na wanachama.
 
“Hitilafu zinapotokea baina yetu zizungumzwe katika vikao vyetu ili tuelewane na kamwe tusipuuze utaratibu wa chama chetu wa kukosoana vinginevyo tutakuwa tunakaribisha majungu ambayo hayakisadii chama chetu” Dk. Shein aliwaeleza viongozi hao.
 
Katika mkutano huo, Dk. Shein alitoa wito pia wa kuimarishwa kwa matawi na maskani za chama hicho kwa ajili ya kukipa nguvu na kuongeza kasi zaidi ya utekelezaji wa shughuli za chama ikiwemo kushinda chaguzi zijazo.
 
Aliwataka wana CCM na wananchi wa Zanzibar kuendelea kuenzi M uungano wa Zanzibar na Tanganyika ambao ulizaa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ambayo sasa imetimiza miaka 50 kwa mafanikio makubwa.
 
“Muungano ni uamuzi sahihi uliofanywa na viongozi wetu waasisi ... ni uamuzi ambao ulifanywa hadharani kwa kushirikisha Baraza la Mapinduzi kwa upande Zanzibar na kwa Tanganyika lilihusika Baraza la Mawaziri” Dk. Shein alieleza na kusisitiza kuwa kuimarisha Muungano ni sehemu ya utekelezaji wa Ilani ya CCM.
 
Aliongeza kuwa kuimarisha Muungano ndio kuenzi Mapinduzi ya mwaka 1964 kwa kuwa bila ya Mapinduzi hayo hakungekuwa na Muungano hivyo wananchi wa Zanzibar hawana budi kusimama kidete kutetea Muungano kwa nguvu zao zote.
 
Katika mkutano huo uliohudhuriwa na viongozi mbali mbali wa chama hicho wakiwemo wajumbe wa Kamati Kuu na Halmashauri Kuu ya Taifa ya chama hicho pamoja na baadhi ya mawaziri, Dk. Shein aliwahakikishia viongozi hao kuwa Serikali itaendelea kuchukua hatua mbalimbali kushughulikia ahadi zake na pia kuondoa kero mbalimbali zinazowakabili wananchi.
 
Kwa upande wake Mwenyekiti wa Mkoa wa Magharibi Yussuf Mohamed alieleza kuwa wananchi wa Mkoa huo wana kila sababu ya kujivunia uongozi wa Dk. Shein kwa namna ulivyojidhahtiti kutekeleza ahadi na mipango mbali mbali ya maendeleo na kubadili maisha ya wananchi.
“katika miaka mine ya uongozi wako tunmeona jitihada zako, ukereketwa wako na uzalendo kuwatumikia wananchi na kuwaletea maendeleo” alisema Mwenyekiti huyo na kuongeza kuwa jitihada hizo zimebadili maisha kila ya mwananchi.
Naye Nibu Katibu Mkuu wa CCM Zanzibar, Vuai Ali Vuai, akimkaribisha Dk. Shein kuzungumza na viongozi hao, alieleza kuwa chama hicho kimezidi kuimarika tangu uchaguzi wa mwaka 2010 ambapo kimeweza kushinda katika baadhi ya chaguzi ndogo zilizofanyika na kueleza kuwa kimekuwa kikionesha uungwana kwa kukubali matokeo pale kinaposhindwa badala ya kulalamika kama vinavyofanya vyama vingine.
Aidha, alihimiza utangazaji wa mafanikio mbalimbali za utekelezaji wa mipango ya maendeleo ya nchi ili wananchi waweze kuelewa hatua zinazochukuliwa na serikali yao kuwaletea maendeleo.  
Postal Address: 2422 Tel.+255 776 613 015, Fax: 024 2231822 
                                               

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.