Habari za Punde

Wadau wa utalii Ufaransa wachangia gari tano

Na Joseph Ngilisho, Arusha
Wadau wa sekta ya utalii nchini Ufaransa, wameisaidia Tanzania magari matano aina ya Toyota Land Cruiser yenye thamani ya shilingi 599,338,330, yatakayotumika kupambana na ujangili katika maeneo mbalimbali yenye uhifadhi wa wanyama pori nchini.

Msaada huo umekabidhiwa kwa Waziri wa Maliasili na Utalii,Lazaro Nyalandu na mwakilishi wa wadau hao hapa nchini,Mohsin Shem,ambaye alieleza kuwa msaada huo umetokana na michango ya taasisi mbalimbali za kusaidia na kupambana na ujangili nchini humo.

Alisema gari hizo zitasaidia kupunguza changamoto inayotokana na ujangili,unaosababisha sekta ya utalii kushuka,kupoteza watalii wa ndani na nje pamoja na kutoweka kwa wanyama ambao ni kivutio kikubwa cha utalii nchini.

“Kwa umoja uliooneshwa na taasisi za utalii,wameahidi kuendelea kutoa misaada mingine mingi ikiwemo vitendea kazi vya kupambana na ujangili,lengo ni kuhakikisha wanatokomeza vitendo vya uharamia wa wanyama nchini,” alisema.


Waziri Nyalandu aliwashukuru wadau hao na kusema suala la ujangili nchini bado ni kubwa, hivyo alitoa wito kwa wadau wengine kuendelea kujitokeza kupiga vita vitendo vya ujangili ili kutokomeza kabisa.

Hata hivyo,alisema serikali ipo mbioni kunununua helkopta mbili zitakazotumika kuongeza nguvu kwa kufanya doria maeneo mbalimbali ya uhifadhi,huku helkopta iliyoanguka hivi karibuni ikiwa mbioni kulipwa na bima.


Aidha alisema serikali inakabiliwa na uhaba wa marubani,ambapo aliitaka jamii kujitokeza kusomea urushaji wa ndege ili kupunguza changamoto hiyo,hata hivyo alizishukuru kampuni mbalimbali za uwindaji zaidi ya 50 zilizojitokeza kumsomesha rubani wa kike,Anna Lorayo (32) atakayesaidia kurusha ndege kwa ajili ya doria ya kupambana na ujangili.

1 comment:

  1. Hapa ndipo ninapoona kuwa katiba iliyopendekezwa haina maana sasa magari wamepewa Tanzania mbona sijaona pahala palipoainisha Zanzibar, au wamepewa Tanganyika?

    ReplyDelete

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.