Habari za Punde

Balozi Seif Afanya Ziara ya Hafla Bandari ya Zanzibar.

Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Bandari Zanzibar Nd. Abdullah Juma Abdullah akimkaguza Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif baadhi ya maeneo yaliyowekwa makontena ndani ya Bandari hiyo.
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi akimuagiza Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Bandari Zanzibar Nd. Abdullah Juma Abdullah kuchukuwa hatua ya kuyapeleka TRA Makontena yote yaliyoshindwa kufuata tataribu ambayo yanaleta msongamano ndani ya Bandari hiyo.
Mrundikano mkubwa wa makontena unaoonekana katika Bandari ya Malindi ambapo baadhi ya wafanyabiashara wanashindwa kutoa makontena yao na kuleta usumbufu kwa watendaji wa Bandari hiyo.
(Picha na Hassan Issa OMPR)

Na. Othman Khamis OMPR
Mrundikano Mkubwa wa Makontena uliopo hivi sasa katika Bandari Kuu ya Malindi Mjini Zanzibar unaonyesha dalili ya kuzitia wasi wasi baadhi ya meli kubwa  za Kimataifa zinazopanga kuleta mizigo yake katika nchi za Mwambao wa Afrika Mashariki.

Uchelewaji wa baadhi ya wafanyabiashara kuchukuwa makontena yao Bandarini hapo ndio sababu kubwa inayochangia mrundikano huo usio wa lazima endapo taratibu za sheria ya kibiashara zitachukuliwa kwa wakati.

Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi alifanya ziara ya ghafla katika Bandari ya Malindi kuangalia harakati za Bandari hiyo na kujionea msongamano mkubwa wa Makontena ya wafanyabiashara ambayo hadi sasa bado hayajachukuliwa wakati muda wa kukaa eneo hilo umepita.


Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Bandari Zanzibar Nd. Abdulla Juma Abdulla alimueleza Balozi Seif kwamba baadhi ya wafanyabiashara wanasita kutoa makontena yao kwa wakati wakilitumia eneo hilo kama sehemu ya kuweka bidhaa zao wakiendelea kutafuta wateja wa bidhaa hizo.

Alisema tatizo hilo licha ya Uongozi wa Bandari kutoa matangazo ya kuwataka wafanyabiashara hao wakamilishe taratibu zinazowahusu lakini bado  utekelezaji wake unakuwa wa kusua sua.

Alisema Uongozi huo umekuwa ukiwasiliana na Mamlaka ya Mapato Tanzania          { TRA } ili kulitafutia ufumbuzi tatizo hilo ambalo limekuwa mzigo mkubwa kwa watendaji wa Bandari hiyo.

“ Zipo taratibu za kisheria zilizowekwa kwa wafanyabaishara wanaochelewa kutoa mizigo yao Bandarini ambayo huipa uwezo Mamlaka ya Mapato Tanzania kupiga mnada kwa biadhaa zilizoshindwa kufuata utaratibu “. 

Alisema Nd. Abdulla Juma Abdulla.
“ Sisi tunazo kanuni na taratibu zinazotupa Mamlaka ya kuwatoza  Dola kumi za Kimarekani kwa wafanyabiashara wanaochelewa kutoa Makontena yao katika muda waliopangiwa “. Alifafanua Nd. Abdulla.

Mkurugenzi Mkuu huyo wa Bandari Zanzibar alimfahamisha Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar kwamba lipo tatizo jengine la uhaba wa vifaa vya kazi  Bandarini hapo kutokana na ongezeko la mizigo inayoteremshwa pamoja na ufinyu wa nafasi za kuweka Makontena.

Nd. Abdullah alisema ipo nafasi ndani ya eneo la Bandari ambalo linaweza kusaidia kuweka Makontena yanayoteremshwa kwenye Bandari hiyo ambalo linaweza kusaidia kupunguza ufinyu wa maeneo ya maegesho ya Makontena.

 Alisema tatizo kubwa ni taratibu za Mamlaka ya Mji Mkongwe wa Zanzibar kutoa kibali cha kuruhusu ujenzi katika eneo hilo ambalo limo ndani ya Mji Mkongwe wa Zanzibar uliomo katika Hifadhi ya urithi wa Kimataifa kupitia Shirika la Umoja wa Mataifa la Elimu, Sayansi na Utamaduni { UNESCO }.

Akitoa shukrani zake kwa kazi kubwa inayoendelea kutekelezwa na watendaji wa Shirika la Bandari Zanzibar Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar balozi Seif aliuagiza Uongozi wa Bandari kuyapeleka  Mamlaka ya Mapato Tanzania {TRA } Makontena yote yaliyoshindwa kukamilisha taratibu zilizowekwa.

Balozi Seif alisema Serikali imekuwa ikipokea lawama  na malalamiko siku hadi siku kutokana na harakati zilizopo Bandarini ambazo matatizo mengi husababishwa na watu wasiopenda kufuata taratibu zilizowekwa.

Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar alizishauri Mamlaka zilazohusika na kazi hiyo kuhakikisha kwamba sheria zote za biashara zinafuatwa na endapo yapo makontena yaliyoshindwa kulipiwa ushuru hatua za kupiga mnada zichukuliwe ndani ya siku 40 ili kurejesha gharama zinazotumiwa katika kazi hiyo.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.