Na Miza Othman -Maelezo Zanzibar 30/01/2015.
Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar imesema Wizara ya Kilimo na Maliasili haina utaratibu wa kutoa mikopo kwa wakulima ikiwemo wafugaji wa nyuki bali suala la kuwawezesha wananchi ikiwemo mikopo ni la Wizara ya Uwezeshaji, Ustawi wa Jamii, Vijana, Wanawake na Watoto.
Naibu Waziri wa Kilimo na Maliasili Mtumwa Kheir Mbaraka ameyasema hayo katika kikao cha Baraza la Wawakilishi wakati akijibu suali la Mh.Saleh Nassor Juma Mwakilishi wa Jimbo la Wawi alietaka mpango wa Serikali kupitia taasisi za fedha kutoa mikopo yenye masharti nafuu ili wafugaji waweze kufuga nyuki kitaalamu.
Amesema Wizara yake inajukumu la kuwashajihisha na kuwahamasisha wananchi katika ufugaji wa nyuki na kujiunga katika vikundi kwa lengo la kujikwamua na umaskini.
Ameongeza kuwa Wizara yake inatoa mizinga ya nyuki na mafunzo ya mbinu bora za ufugaji kwa wale wanaojishughulisha na kazi hiyo kama inavyofanya kwa wanaushirika wa Tujiendeleze wa Jimbo la Wawi Chake chake Pemba.
“Kinachofanyika ni jitihada za kupunguza umaskini na kuwaongezea kipato wananchi kwa kupitia shughuli zao”, Naibu Waziri Mtumwa Kheir amesema.
Alielezea kuwa wafugaji wa nyuki wanaweza kupata mikopo binafsi kwa vikundi vya kukopa na kuweka ikiwemo vikoba au kupitia taasisi za fedha zinazotambuliwa na Serikali kitu muhimu ni kutimiza vigezo na masharti ya taasisi hizo.
Pia amesema nia na lengo la Wizara hiyo ni kuvitembelea vikundi vyote vya wafugaji wa vyuki ili kuwapa mafunzo yaliyo bora katika kuendeleza ufugaji wao.
Wizara ya Uwezeshaji Ustawi wa Jamii, Vijana, Wanawake na Watoto kupitia program mbali mbali hutoa mafunzo ya kusarifu mazao kwa njia mabli mbali kwa vikundi vya akina mama na makundi mengine katika jamii
IMETOLEWA NA IDARA YA HABARI MAELEZO ZANZIBAR.
No comments:
Post a Comment