Na
Abdula Ali Maelezo-Zanzibar 29/01/2015
Waziri
wa Habari, Utamaduni, Utalii na Michezo Zanzibar Mhe. Said Ali Mbarouk amesema zaidi
ya shilingi trilioni tatu zinahitajika ili kuyafanya maeneo ya kihistoria kuwa
ni kivutio kikubwa kwa watalii nchini.
Hayo
ameyaeleza katika ukumbi wa Baraza la Wawakilishi Chukwani Wilaya ya Magharibi
Unguja wakati akijibu swali la mwakilishi wa Jimbo la Wawi Mhe. Saleh Nassor
Juma.
Amesema
hadi sasa Zanzibar ina maeneo ya kihistoria yapatayo 85 Unguja na Pemba, ambayo
yatakuwa ni kivutio kikubwa cha Watalii na kuinua Uchumi wa Nchi ikiwa yatatunzwa, kuhifadhiwa na
kutangazwa nje ya nchi.
Ametanabahisha
kuwa kwa sasa Serikali inayashughulikia zaidi maeneo ya Ras Mkumbuu, Chwaka, Tumbe
na Jambangome ambayo hayako katika uhifadhi mzuri na yameandaliwa mpango
maalumu wa kuyashughulikia kwa kuwa kuna maeneo mengi ya kihistoria
yanayohitaji kuhifadhiwa.
Amesema
kuwa kwa mujibu wa mpango wa Maabara ya Utalii, Ras Mkumbuu imewekwa katika
mpango wa mwaka wa fedha wa kujengwa ukuta wa kuzuia maji ya bahari yasiingie
katika eneo hilo ili kuifanya Ras hiyo kubakia katika muonekano wake wa sasa na
mandhari yaliyo mazuri yenye kuwavutia watalii .
Waziri
Mbarouk amefafanua kuwa kuna maeneo mengi yaliyohifadhiwa katika kipindi cha
hivi karibuni miongoni mwa maeneo hayo ni Kijichi, Kwa Bikhole, Maeneo ya Mahandaki
yaliyotumika katika Vita vya Pili vya Dunia, Eneo la Pango la Watumwa na Mnara vyote
vilivyoko Mangapwani Mkoa wa Kaskazini Unguja ambapo ujenzi wa Makumbusho kwenye
Pango la Kumbi tayari umeshamalizika.
Waziri
Mbarouk amesema ipo haja kwa Serikali kushirikiana na Kamati za Vijiji husika
ili kuweza kuyahifadhi maeneo ya kihistoria kwa ajili ya vizazi vijavyo pamoja
na kuzitaka kamati hizo za Vijiji kukarabati sehemu hizo pale wanapoona kuna
maharibiko yamejitokeza.
Aidha
Waziri Mbarouk amesema Serikali imekuwa ikichukua tahadhari kubwa kuona Kazi za
Sanaa zikiwemo za Filamu na Muziki haziendi kinyume na Mila, Silka na Utamaduni
wa Mzanzibari na badala yake ziwe ni zenye kutoa mafunzo pamoja na kuelimisha
jamii.
Amesema
katika kuhakikisha hayo Wizara yake inazingatia utekelezwaji wa Sheria Namba 1
ya Mwaka 2009 ya Bodi ya Sensa, Sheria hiyo iliundwa kwa lengo la kuhakikisha
kazi zote za Sanaa na Utamaduni zinahakikiwa, ili kuhakikisha mafunzo
yanayopatikana katika Sanaa hizo yanaenziwa, kulindwa, kukuzwa na kuendeleza Mila,
Silka na Utamaduni wa Mzanzibari.
Amefafanua
kwamba kwa kiwango kikubwa kazi hiyo imefanyika na hivi sasa Bodi ya Sensa ya
Zanzibar inafanya kazi na Bodi ya Sensa ya Tanzania Bara katika kutekeleza
jukumu la kuzuia uoneshwaji wa kazi za Sanaa zinazokwenda kinyume na Maadili ya
Nchi yakiwemo Mavazi ya Wasanii yasiyokuwa na Stara na yanayokwenda kinyume na Utamaduni
wa Mtanzania.
Waziri
Mbarouk amewataka wasanii wa Filamu pamoja na Muziki kuwacha kuiga utamaduni wa
Kimagharibi kwa kutoa kazi za sana ambazo zinahamasisha Ngono na kupelekea
kumong’onyoka kwa Maadili ya Mtanzania.
No comments:
Post a Comment