Habari za Punde

Kutoka baraza la wawakilishi: Serikali Haiwadharau Wakunga wa Jadi.

Na Abdula Ali   Maelezo-Zanzibar                                            
Naibu Waziri wa Afya Zanzibar Mhe. Mahmoud Thabit Kombo amesema Serikali haiwazarau Wakunga wa Jadi na badala yake imeamua kuwapatia vibali maalumu ambavyo vitawahalalishia ufanyaji wa kazi zao bila ya usumbufu ili kuokoa vifo vya akina mama wajawazito wakati wa kujifungua.

Hayo ameyasema katika ukumbi wa Baraza la Wawakilishi Chukwani Wilaya ya Magharibi Unguja wakati akijibu swali la mwakilishi wa kuteuliwa wa Nafasi Maalumu za Wanawake Mhe. Panya Ali Abdalla.

Naibu Waziri huyo amesema kuwa Wakunga hao watapewa vibali hivyo baada ya kupatiwa mafunzo maalumu na kuhitimu vizuri katika ngazi ya uzalishaji (Ukunga) na kutanabahisha kuwa Wakunga hao wana umuhimu mkubwa katika jamii kutokana na kazi yao hiyo muhimu na hususan kwa akina mama wajawazito ambao wanatarajia kujifungua.

Amefafanua kuwa lengo la Serikali la kuwapa mafunzo wakunga hao ni kupunguza  vifo vya akina mama wajawazito ambao husumbuka kwa kutembea masafa marefu kutafuta huduma ya kujifungua na anaamini kuwa kutokana na elimu watakayopewa wakunga hao watasaidia kina mama hao kujifungua salama bila ya kusumbuka kwa kutembea masafa marefu.

“Mara nyingi vifo hivi huchangiwa na kuchelewa kwa mama mjamzito kufika katika Kituo cha huduma kitu ambacho kinapelekea kukosa huduma ya haraka”, alieleza Naibu Wazir Thabit Kombo.

Naibu Wazir Thabit Kombo ametanabahisha kuwa suala la kupunguza vifo vya kina mama vinavyotokana na Uzazi ni moja kati ya maeneo yanayopewa kipaumbele katika Sekta ya Afya na ili kupunguza tatizo hilo serikali inahitaji mashirikiano ya pamoja kati ya Wizara ya Afya, Jamii na Sekta nyengine.

Amesema jamii ina wajibu mkubwa katika kukabiliana na tatizo hilo kwa kufanya maamuzi ya haraka wakati mama mjamzito anapohisi dalili za kutaka kujifungua ili kuokoa uhai wa mama huyo na mtoto, kwani vifo vya uzazi hushuka na kupanda kati ya Mwaka hadi Mwaka, takwimu za vifo zinaonesha kuwa Mwaka 2011 vifo 77 vilitokea na kushuka hadi vifo 62 Mwaka 2012 na baadae kupanda tena Mwaka 2013 ambapo vifo 103 viliripotiwa kutokea na vifo 80 kwa Mwaka 2014.


Amesema kutokana na vifo hivyo Wizara yake imechukua hatua mbalimbali katika kuhakikisha tatizo hilo linapungua kadri itakavyowezekana, ikiwemo kupeleka huduma ya kujifungua karibu na wananchi, kuongeza wahudumu wa afya ya uzazi katika vituo vinavyotoa huduma hiyo, kuandaa mpango maalumu wa upatikanaji wa dawa na vifaa vya akina mama na watoto.

Akielezea hatua nyengine Mhe. Thabit Kombo amesema Serikali imeanzisha mpango wa kusomesha masomo ya juu yanayohusu kina mama na watoto (Obstetrics and Gynaecology, Peadiatrics and Child Health Care, Neonatology), kuendelea kutoa elimu kwa akina mama juu ya umuhimu wa kuhudhuria katika vituo vya afya mapema ili kugundua matatizo kwa wakati na kuyafanyia kazi kwa wakati unaostahiki, na kuendelea kushirikiana na Wakunga wa Jadi ili kuwapeleka akina mama katika vituo vya afya na Hospitali kwa ajili ya kujifungua. 


Amefafanua kuwa sambamba na jitihada hizo wizara yake imepanga mpango maalumu wa kujadili kila kifo kinachotokea (Maternal Death Audit) ili kujua sababu ya kifo cha mama huyo na kuweza kujipanga ili kifo kama hicho kisitokee tena pale inapowezekana.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.