Habari za Punde

Tanzania Kuanzisha Duka la Kudumu la Bidhaa zenye Asili ya Kitanzania Nchini Oman

Faki Mjaka-Muscat-Oman 
 
Tanzania inatarajia kuanzisha Duka la kudumu la Bidhaa zenye asili ya Kitanzania katika Mji wa Mascut nchini Omani. Bidhaa hizo ni pamoja na Mavazi, Mapambo, Vyakula na Huduma mbalimbali ambazo zitakuwa zinapatikana muda wote nchini Oman. Hayo yameelezwa na Balozi wa Tanzania Nchini Oman Bw. Ali Ahmed Saleh kufuatia ziara yake ya kuwatembelea Watanzania wanaoshiriki Maonesho ya Kimataifa ya Sanaa Ubunifu na Utamaduni yanayoendelea katika Mji wa Mascut nchini humo. 

Amesema baada ya kuwatembelea Watanzania hao na kujua Mahitaji ya Wananchi wa Omani amebaini ipo haja ya kuanzisha Duka hilo ambalo litawafanyia wepesi Waoman wanapohitaji bidhaa za Kitanzania. Balozi Saleh amefahamisha kuwa Oman ni Nchi yenye Watu wengi wenye Asili ya Tanzania na ambao wanapenda Bidhaa halisi za kitanzania hivyo uwepo wa Duka hilo utakuwa ni ukombozi kwao. 

“Baada ya kuwatembelea hawa ndugu zangu nimejifunza kuwa ipo haja ya kuanzisha Shoo room ya Bidhaa zetu hapa Oman,Wateja wapo wengi maana Wenye Asili ya Kitanzana na Wanaopenda bidhaa za kwetu ni wengi” 

Alisema Balozi. Aidha ameongeza kuwa utekelezwaji wa jambo hilo utakuwa ni sehemu ya kuwakomboa Wajasiriamali wakitanzania hasa wanawake ambao ni kipaumbele kwa Ofisi yake. 


Kwa upande wao Watanzania Wanaoshiriki Maonesho hayo wamemuelezea Balozi Saleh maendeleo ya Maonesho hayo na namna walivyojifunza mambo mengi ikiwemo kujua mahitaji ya Soko la Kimataifa. mmoja ya Wajasiriamali wa Mavazi ya Kimasai Bi Anna Matinde amemuelezea Balozi Saleh umuhimu wa kujua Utamaduni wa Wateja kabla ya kupeleka bidhaa sokoni. 

Bi Anna amesema alichobaini ni kuwa Waomani wengi wanapenda Nguo ndefu na zenye mikono Mirefu kinyume na Utamaduni wa Watu wengine wanaopenda nguo fupi zilizopasuliwa. Hata hivyo Washiriki hao matarajio yao ni kuwa bidhaa walizokuja nazo katika Maonesho hayo zote zitapata Wateja wa kuzinunua kama walivyopanga. 

Tanzania imepeleka Wasanii na Wajasiriamali wa Bidhaa mbalimbali ikiwemo Uchoraji, Uchongaji,
Ufumaji wa Nguo tofauti ikiwemo za Kimasai, Viungo kama vile Karafuu na Ususi wa Mikoba. Katika Maonesho hayo ya kimataifa ya Sanaa na Utamaduni Nchi mbali mbali zimepeleka Washiriki wake kuja kuonesha bidhaa mbalimbali zinazotengenezwa kwa Mikono na Wananchi wake na kuakisi utamaduni wa Nchi husika ambapo Wateja nao hujinunulia Bidhaa hizo.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.