Habari za Punde

Pato la Taifa Laongezeka Lafikia Shilingi Trilioni 21.2.

Mkurugenzi wa Takwimu za Uchumi wa Ofisi ya Taifa ya Takwimu (NBS) Bw. Morrice Oyuke (Kulia)akitoa taarifa ya Pato la Taifa kwa kipindi cha robo tatu ya mwaka 2014 leo jiji Dar es salaam. Pato hilo kwa mwaka 2014 limefikia kiasi shilingi trilioni 21.2  kutoka trilioni 19.8 za mwaka 2013, Kushoto ni  Mtakwimu Mkuu wa Ofisi hiyo Bw. Gregory Milinga,

Aron Msigwa –MAELEZO.
Pato la Taifa (GDP)  katika kipindi cha robo ya tatu ya mwaka 2014 limeongezeka hadi kufikia shilingi trilioni 21.2 kutoka shilingi trilioni 19.8  za kipindi kama hicho kwa mwaka 2013.

Akizungumza na waandishi wa habari leo jiji Dar es salaam, Mkurugenzi wa Takwimu za Uchumi wa Ofisi ya Taifa ya Takwimu (NBS) Bw. Morrice Oyuke, amesema kuwa katika kipindi cha robo tatu ya mwaka 2014 sekta nyingi za uchumi zimefanya vizuri katika uzalishaji ikilinganishwa na mwaka 2013. 

Amesema katika kipindi hicho shughuli za uchimbaji wa Madini , Mawe na Kokoto zimekua kwa asilimia 5.2 ikilinganishwa na asilimia 3.3 za mwaka 2013, Uzalishaji wa bidhaa za viwandani  ukikua kwa asilimia 10.8 kutoka asilimia 10.4 pamoja na ongezeko la uzalishaji wa umeme kwa asilimia 10.7 kutoka asilimia 10.3 za mwaka 2013 kutokana na matumizi ya mafuta na Gesi.

Amezitaja sekta nyingine kuwa ni usambazaji maji ambao umekua kwa asilimia 12.7 kutoka 6.9 za mwaka 2013, Habari na Mawasiliano kwa asilimia 11.9 kutoka 7.0, Shughuli za Fedha na Bima zikikua hadi kufikia asilimia 13.9 kutoka asilimia 6.8 za mwaka 2013.

Ameongeza  kuwa  katika kipindi hicho huduma za upangishaji wa nyumba zilikua hadi kufikia asilimia  2.2 kutoka 2.1, shughuli za kitaalamu, kisayansi, ufundi na utawala  zikifikia  asilimia 5.4 kutoka asilimia 1.0 ya mwaka 2013.

 Bw. Oyuke amezitaja  shughuli  nyingine kuwa ni uendeshaji wa Serikali ambazo zilikua  kwa asilimia 4.9 ikilinganishwa na 4.4, huduma za Elimu kwa asilimia 3.7 kutoka 3.5, Afya kwa asilimia 8.1 pamoja na shughuli za Sanaa na Michezo ambazo zilikua kwa asilimia 2.5 ikilinganishwa na 1.6 ya mwaka 2013.

Aidha, amebainisha kuwa uzalishaji wa Almasi katika kipindi cha robo tatu ya mwaka 2014 ulikuwa karatasi 66,508 ikilinganishwa na karatsi 27,828 zilizozalishwa katika kipindi kama hicho mwaka 2013.

Akizungumza kuhusu sekta ambazo hazikufanya vizuri katika kipindi cha Robo tatu ya mwaka 2014 Mkurugenzi huyo amesema kuwa  ni dhahabu  ambayo uzalishaji wake ulifikia Kilogramu 10,137 kwa mwaka 2014 ikilinganishwa na 11,010 za mwaka 2013,Madini ya Tanzanite kilogramu 1,449 kutoka 5140 zilizozalishwa mwaka 2013.

Amefafanua kuwa shughuli za Biashara za Jumla na reja reja, Ukarabati wa magari na pikipiki pamoja na vifaa vingine vya nyumbani zimeonyesha kukua kwa asilimia 6.0 kwa mwaka 2014 ikilinganishwa na kasi ya asilimia 6.7 ya mwaka 2013, shughuli za uhifadhi asilimia 13.9 kwa mwaka 2014 ikilinganishwa na asilimia 19.3 za mwaka 2013.

Aidha, amebainisha kuwa katika kipindi hicho cha miezi mitatu ya mwaka 2014 kuanzia Julai mpaka Septemba, Pato la taifa kwa bei za mwaka 2007 limefikia kiasi cha Shilingi trilioni 10. 7 ikilinganishwa na shilingi trilioni 10.1 ya mwaka 2013.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.