Na Othman Khamis OMPR
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi amewashukuru na kuwapongeza Wananchi wa Mtaa wa Kibweni Wilaya ya Magharibi kwa moyo wao waliouonyesha katika kusaidia kuuzima moto ulioibuka majira ya saba 7.00 usiku juzi kwenye nyumba ya Sheha wa Shehia ya Kibweni Bibi Asha Ali Nassor.
Alisema licha ya kwamba vitu vyote vilivyokuwemo ndani ya chumba cha mmoja wa watoto wa Sheha huyo alitwae Asumini Moh’d Juma kuteketea kwa moto huo lakini juhudi za pamoja kati ya wakaazi wa nyumba hiyo na wananchi jirani zimesaidia kuepuka maafa zaidi katika janga hilo.
Balozi Seif Ali Iddi alisema hayo wakati alipofika Kibweni kuwafariji wakaazi wa nyumba hiyo na kuwapa mkono wa pole kutokana na maafa hayo akiambatana na Mkuu wa Wilaya ya Magharibi Nd. Ayoub Moh’d Mahmoud.
Alishauri na kuomba mpango huo uendelezwe zaidi ili kutoa faraja kwa wananchi wanaopatwa na maafa katika matukio mbali mbali yakiwemo yale ya moto na hata ya tabia nchi.
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar alimtaka mpatwa na maafa hayo Bibi Asumini Moh’d Juma kuwa na moyo wa subira katika kipindi hichi cha mtihani na kumtakia hali ya utulivu katika maisha yake ya baadaye.
Mapema Mmmoja wa mashuhuda ya tukio hilo anayeishi ndani ya nyumba hiyo Abdulla Kombo Hamad alimueleza Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif kwamba moshi mkubwa uliotanda ndani ya nyumba hiyo ndio chanzo kilichowatanabahisha kuwepo kwa hali isiyo ya kawaida vyumbani humo.
Bwana.Abdullah Kombo alisema wakazi wa nyumba hiyo kwa kusaidiana na majirani walilazimika kuvunja mlango wa Chumba kilichokuwa na moshi mwingi cha Bibi Asumini ambaye kwa wakati huo alikuwa Harusini na kufanikiwa kuuzima moto huo.
Alifahamisha kwamba baada ya kuangalia kwa kina chanzo cha moto huo walichodhania kuwa ni hitilafu za umeme, wakagundua kuwa ni chupa ya mafuta ya Petroli iliyopenyezwa kwenye durisha la nyuma la chumba hicho.
Bwana.Abdullah Kombo Hamad alielezea faraja yake baada ya kuona juhudi zao pamoja na majirani zilisaidia kuudhibiti moto huo usiathiri mfumo wa waya za umeme zilizomo ndani ya nyumba hiyo.
Naye Mkaazi wa chumba hicho Bibi Asumini Moh’d Juma alisema kwamba moto huo umesababisha kuteketeza vitu vyote vilivyokuwa vimehifadhiwa ndani ya chumba chake.
Bibi Asumini alivitaja baadhi ya vitu vilivyokuwemo ndani ya chumba chake kuwa ni pamoja na kabati lililohifadhiwa nguo zote, Kitanda na Godoro lake,Charahani, vyakula pamoja na baadhi ya vitu vya ndani.
Alisema licha ya mtihani huo lakini anawashukuru watu wa wasamaria mbali mbali kwa moyo wao wa huruma waliomuonyesha wa kumpatia baadhi ya huduma zikiwemo nguo za kujistiri hali iliyompa faraja kubwa.
No comments:
Post a Comment