Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk.Ali Mohamed Shein akisalimiana na Mhe,Wang Jiarui Makamu Mwenyekiti wa Kamati ya Baraza la Ushauri wa Kisiasa la Watu wa China pia Waziri wa Idara ya Kimataifa wa kamati Kuu ya Chama cha Kikomunisti cha China alipofika Ikulu Mjini Zanzibar akiwa na ujumbe wake leo,[Picha na Ikulu.]
STATE HOUSE ZANZIBAR
OFFICE OF THE PRESS SECRETARY
PRESS RELEASE
Zanzibar
27.3.2015
SERIKALI ya Jamhuri ya Watu wa China imeahidi
kuendelea kuiUnga mkono Zanzibar katika kuimarisha miradi yake ya maendeleo
sambamba na kuimarisha uhusiano na ushirikiano wa muda mrefu ulioasisiwa na viongozi wake wakuu.
Makamo Mwenyekiti
wa Kamati ya Kitaifa ya Baraza la Ushauri wa Kisiasa la Watu wa China ambae
pia, ni Waziri wa Idara ya Kitaifa wa Kamati Kuu ya Chama Cha Kikomunisti cha
China Mhe. Wang Jiarui, aliyasema hayo leo huko Ikulu mjini Zanzibar wakati
alipokuwa na mazungumzo na Rais wa Zanzibar na Mwekitiwa Baraza la Mapinduzi
Mhe. Dk. Ali Mohamed Shein.
Katika mazungumzo
hayo, Mhe. Wang Jiarui, alimueleza Dk. Shein kuwa China inathamini uhusiano na
ushirikiano huo wa muda mrefu kati yake na Tanzania ikiwemo Zanzibar hatua
ambayo imeweza kuleta maendeleo makubwa kwa pande zote mbili.
Mhe. Jiarui alisisitiza
kuwa China itaendeleza yale yote yalioasisiwa na viongozi hao na kuendelea
kuiunga mkono Zanzibar katika miradi yake mbali mbali kwani inatambua juhudi
kubwa zinazochukuliwa na Serikali ya Mapinduzi Zanzibar chini ya uongozi wa Dk.
Shein.
Aidha, Waziri
huyo wa Idara ya Kitaifa wa Kamati Kuu ya Chama cha Kikomunisti cha China,
alimueleza Dk. Shein kuwa mafanikio yaliopatikana nchini mwake na kumueleza
kuwa hatua hiyo imefikiwa kutokana na msimamo madhumuti sambamba na mikakati
iliyowekwa chini ya chama cha Kikomunisti cha nchi hiyo.
Alisema kuwa
viongozi wa China na Tanzania wamekuwa na uhusiano na ushirikiano mwema katika
kuendeleza maendeleo ya kiuchumi, kisiasa na kijamii hatua ambayo hupelekea
viongozi wa pande zote mbili kufanya ziara kwa ajili ya kupanua wigo wa
maendeleo.
Kiongozi huyo
pia, alisisitiza haja ya kuimarishwa kwa uhusiano na ushirikiano wa kibiashara
kati ya China na Tanzania ikiwemo Zanzibar kwa kutambua kuwa hivi sasa nchi
hiyo imepiga hatua kubwa kiuchumi ikiwa inashika nafasi ya pili duniani.
Pamoja na hayo,
kiongozi huyo alisisitiza haja ya kuwajengea misingi imara vijana kwa kutambua
mchango wao mkubwa katika kuziletea nchi zao maendeleo katika sekta zote
muhimu.
Alisema akuwa
vijana ndio nguvu kazi ya Taifa hivyo kuna kila sababu kuwapa kipaumbele katika
kuhakikisha wanajenga nchi yao na kueleza kuwa vijana ndio waliosimama kidete
wakati wa kudai huru kwa upande wa China
na Tanzania hivyo kuna kila sababu ya kuwaunga mkono katika juhudi zao za
kimaendeleo.
Alisisitiza kuwa
China imeweza kushirikiana vyema na nchi za Afrika katika kuimarisha sekta za
maendeleo na uchumi na kuahidi kuendelea kuunga mkono juhudi za maendeleo kwa
nchi hizo ikiwemo Tanzania.
Sambamba na hayo,
Kiongozi huyo alieleza kuvutiwa kwake na visiwa vya Zanzibar kutokana na
maumbile yake kiutalii na kueleza azma ya watalii kutoka nchi hiyo kuendelea
kuja kuitembelea Zanzibar.
Aidha, Makamu
Mwenyekiti huyo wa Kamati ya Kitaifa ya Baraza la Ushauri wa Kisiasa la Watu wa
China alisema kuwa chama hicho kina
historia kubwa na ya muda mrefu kati yake na Chama Cha Mapinduzi (CCM) na
kueleza kuwa uongozi wa chama hicho utaendeleza uhusiano na ushirikiano huo
kama ulivyoasisiwa na viongozi wake wakuu.
Nae Dk. Shein kwa
upande wake alitoa pongezi kwa kiongozi huyo kwa kufanya ziara yake hapa
Zanzibar hatua ambayo inaonesha jinsi China inavyothamini uhusiano na
ushirikiano uliopo kati ya pande mbili hizo na kuahdi kuwa Zanzibar nayo
itauendeleza.
Dk. Shein alisema
kuwa China ina historia kubwa katika juhudi za kuiunga mkono Zanzibar na ni
miongoni mwa nchi za mwanzo zilizoyatambua Mapinduzi matukufu ya Januari 12,
1964 na kusisitiza kuwa ni miaka 51 hivi
sasa tokea China iwe na uhusiano na mashirikiano na Tanzania ikiwemo Zanzibar
muda ambao umeweza kuleta mafanikio makubwa ya kimaendeleo, kiuchumi, kisiasa
na kijamii.
Dk. Shein
alitumia fursa hiyo kutoa pongezi kwa China kutokana na kuendelea kuiunga mkono
Zanzibar katika kuimarisha sekta mbali mbali za maendeleo ikiwemo sekta ya afya
kwa kuendelea kuleta madaktari kutoka nchini humo sambamba na juhudi zilizokuwa
zikifanywa na nchi hiyo kwa kuleta wataalamu wa sekta mbali mbali.
Aidha, Dk. Shein
alimueleza kiongozi huyo juhudi zinazochukuliwa na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar
katika kutekeleza malengo yake sambamba na mikakati yake ukiwemo Mkakati wa
Kukuza Uchumi na Kupunguza Umasikini Zanzibar (MKUZA) ambao hivi sasa uko awamu
ya pili sambamba na Dira ya 2020.
Alieleza kuwa
juhudi zimekwua zikichukuliwa katika kuimarisha sekta za afya, elimu, kilimo,
miundombinu, maji safi na salama na nyenginezo huku akigusia suala la
kuimarisha sekta ya utalii ambayo imekuwa ikichangia kwa kiasi kikubwa pato la
Taifa sambamba na ukuaji wa uchumi wa Zanzibar.
Dk. Shein, pia, alieleza haja ya kuwepo kwa mashirikiano
kati ya Manispaa za mji wa Beijing na Zanzibar hatua ambayo itaimarisha zaidi
uhusiano na ushirikiano wa viongozi na wananchi wa maeneo hayo sambamba na
kuimarisha sekta ya utalii hapa Zanzibar.
Sambamba na hayo,
Dk. Shein alimueleza kiongozi huyo kuwa mara zote azma ya vyama vya siasa ni
kuleta maendeleo hivyo kwa upande wa CCM hilo ndilo jambo ililolipa kipaumbele na
tayari imefanikiwa kwa hilo kwa upande wa Zanzibar na Tanzania Bara na
kusisitiza kuwa CCM itaendeleza uhusiano na Chama Cha Kikomunisti cha China.
Rajab Mkasaba, Ikulu
Zanzibar
Postal Address: 2422 Tel.:0777427449. Fax: 024
2231822
E-mail:
rajabmkasaba@yahoo.co.uk
No comments:
Post a Comment