Habari za Punde

Mabaraza ya Wafanyakazi Taasisi za Elimu ya Juu Yatakiwa Kufanyakazi kwa Weledi.

Naibu Waziri wa Fedha (Sera) Mhe. Mwigulu Nchemba (katikati) akiwa ameambatana na Mtendaji Mkuu wa Taasisi ya Uhasibu Tanzania Dkt. Joseph Kihanda (kulia) na Mwenyekiti wa Bodi ya Ushauri ya Wizara Prof. Isaya Jairo kabla ya kuzindua Baraza la Pili la Wafanyakazi wa Taasisi ya Uhasibu Tanzania (TIA) lililojumuisha wawakilishi kutoka matawi 6 ya taasisi hiyo katika mikoa ya Kigoma, Singida, Mwanza , Mtwara, Dar es salaam na Mbeya.
Naibu Waziri wa Fedha (Sera) Mhe. Mwigulu Nchemba wakati akizindua Baraza la Pili la Wafanyakazi wa Taasisi ya Uhasibu Tanzania (TIA) leo mjini Bagamoyo.
Wajumbe wa Baraza la Pili la Wafanyakazi wa Taasisi ya Uhasibu Tanzania (TIA) wakiimba wimbo wa mshikamano daima kabla ya kuanza kwa mkutano wao leo mjini Bagamoyo.
Wajumbe na viongozi wa Baraza la Pili la Wafanyakazi wa Taasisi ya Uhasibu Tanzania (TIA) wakiwa katika picha ya pamoja na Naibu Waziri wa Fedha Mhe. Mwigulu Nchemba (katikati) mara baada ya kuzinduliwa kwa baraza hilo leo mjini Bagamoyo.(Picha na Aron Msigwa/MAELEZO).

Na. Aron Msigwa –MAELEZO.
Serikali imeyataka Mabaraza ya wafanyakazi wa Taasisi za Elimu ya juu kote nchini kufanya kazi kwa bidii na kuzingatia weledi, kanuni na sheria zinazosimamia  mabaraza hayo ili yawe chachu katika kuleta maendeleo ya Elimu  na mabadiliko ya kiuchumi ya taasisi hizo.

Kauli hiyo imetolewa  na Naibu Waziri wa Fedha (Sera) Mhe. Mwigulu Nchemba wakati akizindua Baraza la Pili la Wafanyakazi wa Taasisi ya Uhasibu Tanzania (TIA) lililojumuisha wawakilishi kutoka matawi 6 ya taasisi hiyo  katika mikoa ya Kigoma, Singida, Mwanza , Mtwara, Dar es salaam na Mbeya.

Mhe. Mwigulu amesema kuwa iwapo mabaraza hayo yatazingatia weledi katika kusimamia masuala mbalimbali ya taasisi hizo nchini  yataleta mabadiliko ya kiutendaji katika usimamizi wa mapato na matumizi  na kutoa  ushauri utakaoisaidia Serikali kutekeleza mipango mbalimbali ya  maendeleo.

Mhe. Mwigulu ameeleza  kuwa endapo mabaraza hayo yataacha kufanya kazi kwa mazoea na kujikita katika kuzingatia kanuni na taratibu zilizowekwa, taasisi hizo zitaongeza uzalishaji, zitakuza mapato na kutatua kero mbalimbali za wafanyakazi mahali pa kazi.

“ Napenda niweke wazi kuwa mabaraza haya  ni muhimu sana kwa wafanyakazi, hayana tofauti na bunge ,kazi yake  kubwa ni kusimamia mapato na matumizi, kushauri taasisi na Serikali juu ya utekelezaji wa  mipango mbalimbali ikiwemo ajira kwa watumishi wapya” Amesisitiza.

Akizungumzia changamato ya uhaba wa walimu na watumishi wa kada mbalimbali  katika taasisi hiyo na taasisi nyingine za Umma za Elimu ya juu amesema Serikali inaendelea  kutenga fedha katika bajeti ya kila mwaka ili kuondoa tatizo hilo.

Aidha, amesema Serikali inaendelea kulishughulikia suala la usimamizi wa ziada ya mapato yanayozalishwa na taasisi za umma ili yaweze kupelekwa  katika maeneo mengine yenye uhitaji.


“Serikali tunaendelea kuangalia utaratibu wa kutumia ziada ya mapato inayozalishwa na taasisi mbalimbali za umma ili iweze kupelekwa katika maeneo mengine yenye uhitaji maana fedha hizi ni za umma,taasisi moja ya Serikali haiwezi kung’ania ziada ya mapato iliyozalisha, hizo ni fedha za umma lazima zikafanye kazi maeneo mengine yenye uhitaji hasa kwenye kugharamia mahitaji ya wodi za akina mama kote nchini”
Pia amesisitiza mkakati wa Serikali wa kuzifanya taasisi hizo za elimu ya juu kuwa na mamlaka yake katika kuajili watumishi wake na kjitegemea.

Kwa upande wake Mwenyekiti wa Baraza hilo ambaye ndiye Mkuu wa Taasisi ya Uhasibu Tanzania Dkt. Joseph Kihanda  akizungumza na wajumbe wa baraza hilo amesema kuwa taasisi hiyo katika kipindi cha miaka 5 imepata mafanikio makubwa ya kuongeza  ukusanyaji wa mapato kutoka shilingi Bilioni 6 za mwaka 2010 hadi kufikia shilingi Bilioni 18 mwaka 2014/2015.

Amesema Taasisi hiyo licha ya kukabiliwa na changamoto mbalimbali ikiwemo ya uhaba wa miundombinu, ufinyu wa bajeti , uhaba wa walimu wenye shahada za uzamivu (PhD)  na watumishi kimeendelea kupata idadi kubwa ya wanafunzi wanaodahiliwa kutoka  7635 waliodahiliwa mwaka 2011/2012 hadi kufikia 14974 mwaka 2014/2015.

“Licha ya kuendelea kufanya vizuri taasisi yetu inakabiliwa na tatizo la waalimu katika matawi yetu yaliyo mikoani ,jambo hili hutufanya tutumie gharama kubwa kuwasafirisha kutoka makao makuu kwenda kufundisha wanafunzi wetu wanaochukua michepuo ya Biashara, Uhasibu, Rasilimali Watu, Ununuzi na Ugavi,Uhasibu katika Sekta ya Umma na Masoko na Mahusiano kwenye matawi yetu” Amesisitiza. 

Naye Mwenyekiti wa Bodi ya ushauri ya wizara ya Fedha wa Taasisi hiyo Prof. Isaya Jairo akizungumza na wajumbe waliohudhuria mkutano huo amesema kuwa Taasisi ya Uhasibu Tanzania (TIA)katika kukuza na kuongeza mapato ya ndani na kupunguza utegemezi kutoka serikalini itaendelea kufanya shughuli kibiashara ,kufanya utafiti, kutoa ushauri katika Nyanja za uhasibu, ununuzi na ugavi kote nchini.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.