HOTUBA YA MHE. RAMADHAN A. SHAABAN KATIKA KONGAMANO LA
MWISHO LA MRADI WA SMOLE II KATIKA UKUMBI WA SALAMA, HOTELI YA BWAWANI
21 MEI 2015
Waheshimiwa Mawaziri wa Serikali ya
Mapinduzi ya Zanzibar
Mhe. Balozi wa Finland nchini
Tanzania, Bibi Sinikka Antila
Waheshimiwa Wawakilishi wa Kibalozi
Waheshimiwa Wakuu wa Mikoa
Waheshimiwa Wakuu wa Wilaya
Ndugu Makatibu Wakuu
Ndugu Wageni Waalikwa
Mabibi na Mabwana
Kwanza kabisa napenda kumshukuru
Mwenyezi Mungu kwa kutajaalia afya njema na kutupa fursa ya kukutana hapa leo.
Pili nachukua fursa hii kukushukuruni kwa kuweza kuacha shughuli zenu na
kushirikiana nasi katika hafla hii muhimu ya mashirikiano baina ya Finland na
Zanzibar. Nachukua fursa hii pia kuwashukuru waandaaji wa hafla hii kwa
kunialika kuwa ni mgeni rasmi. Nasema Ahsante sana.
Ndugu Wananchi,
Sina budi kuishukuru Serikali ya
Finland na watu wake kwa msaada mkubwa wa kimaendeleo uliokuwa unaipa Zanzibar
katika nyanja mbali mbali. Finland imeisaidia Zanzibar katika sekta ya maji,
sekta ya misitu na sekta ya ardhi na mazingira kwa muda mrefu tangu kwenye
miaka 1980. Kwa hili namuomba Mhe. Balozi, awasilishe shukurani zetu za dhati
kwa Serikali ya Finland na watu kwa jinsi wanavyotuunga mkono katika jitihada
zetu za kuleta maendeleo kwa watu wa Zanzibar.
Mhe Balozi wa Finland
Nikiwa kama Waziri wa Ardhi nautambua
mchango wako mkubwa katika kuisaidia Zanzibar kupiga hatua za mara kwa mara.
Mapema mwaka 2014 ulisaidia kumleta nchini Waziri Mkuu wa Finland ambaye pia
alifika kuangalia shughuli za usimamizi wa ardhi na mazingira. Aidha mwaka huu,
mwezi wa Februari, ulishiriki katika uzinduzi wa ZALIS katika Jengo la Ardhi. Hii
ni ishara tosha ya jinsi unayoithamini Zanzibar na watu wake.
Ndugu
Wananchi,
Leo
ni siku nzuri lakini ni siku ya huzuni. Ni siku ya huzuni kwa sababu tunaagana
na kipenzi chetu tuliyekuwa naye kwa muda mrefu. Tumekutana hapa kwenye kongamano
hili kwa nia ya kuufunga rasmi mradi wa SMOLE II. Mradi huu ulianza mwaka 2010
ambapo mchango wa Zanzibar ni Shilingi million 828 za Kitanzania na mchango wa
Finland ni Euro million 9 ambazo ni karibu sawa na bilioni 20.
Mradi
huu ingawa si mkubwa lakini haukuwa rahisi kiutekelezaji kwani ulihusisha Idara
tano za serikali Idara ya Misitu na Maliasili Zisizorejesheka, Idara ya
Mazingira, Idara ya Ardhi na Usajili, Idara ya Mipango Miji na Vijiji na Idara
ya Upimaji na Ramani. SMOLE II katika
utekelezaji wake ilisimamiwa na Wizara nne tofauti Wizara ya Fedha, Wizara ya
Ardhi, Wizara ya Kilimo na Afisi ya Makamo wa Kwanza wa Rais.
Muundo
huu peke yake ulikuwa na changamoto kubwa mbali na lengo kuu la mradi la
kupunguza umaskini kupitia usimamizi endelevu wa ardhi na mazingira. Hata hivyo
mtakubaliana nami kuwa Idara zilizotekeleza Mradi wa SMOLE II zimefanya kazi
kubwa tena kwa ufanisi. Mliopo hapa leo mmeona mafanikio ya Idara hiyo.
Ndugu
Wananchi
Naomba
nichukue fursa hii nami kuelezea machache baadhi ya mafanikio hayo kwa upande
wangu. Naelewa kuwa sasa Wizara yangu ya Ardhi, Makaazi, Maji na Nishati
imefanikiwa kutayarisha rasimu ya Sera ya Taifa ya Ardhi ambayo imo mbioni
kuwasilishwa serikalini. Aidha Mradi wa SMOLE II umefanikisha Marekebisho ya
Sheria ya Usajili wa Ardhi, imesaidia utayarishaji wa Sheria ya Kamisheni ya
Ardhi na pia kuchangia katika utayarishaji wa Sheria ya Uthamini. Huu si
mchango mdogo katika usimamizi endelevu wa ardhi. Mama Balozi nasema Ahsante
sana
Vile
vile kwa upande wa Idara ya Mazingira na Idara ya Misitu na Maliasili
Zisizorejesheka, Mradi wa SMOLE II umesaidia kuzifanyia marekebisho Sheria kuu
za Idara hizo pamoja na kusaidia mapitio na marekebisho ya Sera za Misitu na
Mazingira. Sambamba na hayo naelewa kuwa Idara zote tano hivi sasa zina Mipango
Mikakati yake iliyotayarishwa kwa mashirikiano na Mradi wa SMOLE II. Kwa maoni
yangu lengo la kuzijenga uwezo wa kitaasisi idara hizi tano limefanikiwa hasa.
Kwa hili sina budi kuwapongeza viongozi na watendaji wa Idara hizi tano kwa
utendaji wao mzuri.
Mheshimiwa
Balozi
Pamoja
na kwamba tupo hapa leo kuagana na kuufunga mradi wa SMOLE II lakini sina budi
nikiri kuwa kuna baadhi ya maeneo hatukuwa kufikia malengo yetu. Maeneo hayo ni
maeneo ya Usajili wa Ardhi na Uwekaji wa Taarifa za Ardhi chini ya mfumo wa
ZALIS.
Serikali
ya Mapinduzi ya Zanzibar kupitia MKUZA II mwaka 2010 uliweka lengo la kusajili
asilimia 50 ya Ardhi ya Zanzibar ifikapo mwaka 2015. Kwa bahati mbaya sana
zoezi la usajili wa ardhi kutokana na sababu za kitaalamu na kisheria
lilichelewa kuanza hadi mwaka 2013. Hadi wakati huu ni vikataa karibu 5,000
ndiyo vimeweza kusajiliwa. Hata hivyo, pamoja na matokeo hayo, napenda
kukuhakikishia kuwa zoezi hili halitasimama na tutaendelea nalo kwani lengo kuu
hasa ni kusajili ardhi yote kwa asilimia
100.
Aidha
lengo la kuanzisha mfumo wa kuweka taarifa za ardhi yaani ZALIS nalo
lilichelewa kuanza hadi mwaka 2014. Uwekaji wa miundo mbinu ya mfumo wa ZALIS
umekamilika na utayarishaji wa programu za kukusanyia taarifa hizo za ardhi
unaendelea. Hapa napenda kukuhakikishia kuwa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar
itaendelea na shughuli hii ya kutayarisha mfumo kamili wa uwekaji wa kumbukumbu
zote za ardhi ili uwe ni kichocheo cha usimamizi endelevu wa ardhi na ukuaji wa
uchumi.
Mheshimiwa
Balozi
Let me say this in English for
clarity, the Goverment of Zanzibar is committed to support the land
registration process in Zanzibar as well as support the development of ZALIS. However,
thorough you, we request Government of Finlad to renew their support in the
areas of Systematic Land Registration and Development of ZALIS. These areas
were implemented very late in the SMOLE II support.
Ndugu Watendaji
Mradi wa SMOLE II umetusaidia
kutupatia ala mbali mbali za usimamizi na uendeleshaji w sekta zetu. Sasa
ninachoweza kukunasihini kuwa wakati umefika wa kuonekana kuwa ala hizo za
usimamizi kwa maaana ya sera, sheria, mipango mikakati inatekelezwa katika
usimamizi endelevu wa ardhi.
Ndugu Wananchi na Wageni Waalikwa
Baada ya maelezo hayo mafupi, kwa
niaba yangu binafsi na Wizara ya Ardhi, Makaazi, Maji na Nishati naomba
kutangaza kuwa Mradi wa Usimamizi Endelevu wa Ardhi na Mazingira wa Awamu ya
Pili umefungwa rasmi.
Ahsanteni kwa kunisikiliza.
No comments:
Post a Comment