Habari za Punde

Walinda amani watanzania wapoteza maisha DRC

Mwakilishi Maalum wa  Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa  katika Jamhuri ya Kidemokrasia ya  Kongo ( DRC) Bw. Martin Kobler akiwafariji  walinzi wa amani  kutoka  Jeshi la Wananchi wa Tanzania ( JWTZ) wanaohudumu katika Misheni ya MONUSCO ( DRC)  kufuatia shambulio  lililotokea siku ya  Jumanne huko Ben,i Magharibi ya Jimbo la Kivu. Katika shambulio hilo na ambalo limelaaniwa vikali na  Katibu Mkuu, Ban  Ki Moon, walinzi wawili wamepoteza maisha na wengine 13 wamejeruhiwa

·         BAN KI MOON ALAANI  VIKALI

Na Mwandishi Maalum

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Ban  Ki Moon,  amelaani vikali kuuawa kwa walinzi  wawili wa amani kutoka  Tanzania wanaohudumu katika Misheni ya Kulinda Amani katika Jamhuri ya   Kidemokrasia ya  Kongo ( MONUSCO).

Walinzi hao wamepoteza maisha  baada ya kushambuliwa na kundi la   waasi linalosadikiwa kuwa ni  la  Allied Democratic Forces ( ADF), shambulio hilo limetokea siku ya   jumanne katika  eneo la Beni,  Magharibi ya  Jimbo la  Kivu ambapo walinda Amani wengine 13 wamejeruhiwa.

Shambulio hilo  limetokea wakati kikosi hicho cha  walinzi wa Amani kutoka JWTZ wakielekea kutoa ulinzi  kwa wananchi na ndipo waliposhambuliwa.

 Walinzi  wa Amani waliopoteza maisha  ni  Private Juma Ally Khamis na Koplo John Leonard Mkude.

Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na  msemaji wa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa  jumanne jioni,  inaelezea  masikitiko makubwa ya  Katibu Mkuu, Ban ki Moon,  kufuatia tukio hilo la kusikitisha na ametoa pole kwa   serikali ya  Jamhuri  ya Muungano wa Tanzania na familia  za marehemu.


Ban Ki Moon katika salamu zake  amesema,  walinzi hao wamepoteza maisha yao wakati wakielekea kutoa ulinzi  kwa raia kwa mujibu wa mamlaka waliyokabidhiwa na Umoja wa Mataifa, na kusisitiza kwamba suala la kuwalinda raia litaendelea kupewa muhimu kama ilivyoainisha kupitia azimio  namba  2211(2015) la Baraza Kuu la Usalama la Umoja wa Mataifa.

Aidha taarifa ambazo Uwakilishi wa Kudumu wa Tanzania katika Umoja wa Mataifa, imezipata kutoka Idara ya Ulinzi wa Amani ya Umoja wa Mataifa ( DPKO) zimetaarifu kwamba walinzi  wengine wanne ambao walikuwa hawajulikani walipo wamepatikana wakiwa hai.

Wakati huo  huo,  Mshauri wa Masuala ya Kijeshi katika Umoja wa Mataifa,  Luteni General Magsood Ahmed  naye ametoa salamu zake za pole kwa Serikali  na familia ya  marehemu kufuatia shambulio hilo.

Katika  salamu zake kupitia kwa Mwakilishi wa Kudumu wa Tanzania katika Umoja wa Mataifa,  Lt. General Ahmed pamoja na kulaani shambuli hilo amesifu na kupongeza  namna  wanajeshi wa Tanzania wanaolinda Amani  kupitia  Misheni hiyo ya MONUSCO wanavyotekeleza majukumu yao ya ulinzi kwa weledi mkubwa.

Katika  hatua nyingine,  Mwakilishi  Maalum wa Katibu MKuu katika DRC. Bw. Martin Kobler naye ameelezea kusikitishwa kwake kufuatia shambulio hilo.  Na kwamba hatavumilia kuona matukio ya kushambuliwa kwa walinzi wa Amani katika eneo hilo ya Beni yakiendelea.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.