Habari za Punde

Dk Shein asisitiza dhamira ya Zanzibar kutekeleza mashirikiano na Serikali ya muungano wa Comoro

STATE HOUSE ZANZIBAR
OFFICE OF THE PRESS SECRETARY
PRESS RELEASE
    Zanzibar                                                    04 Julai, 2015
TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI
Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Ali Mohamed Shein amesisitiza dhamira ya Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar ya kutekeleza makubaliano yaliyofikiwa kati yake na Serikali ya Muungano wa Comoro wakati wa ziara yake rasmi aliyoifanya nchini humo mwezi Septemba mwaka jana.

Amesema utekelezaji wa makubaliano hayo umo katika hatua mbalimbali kulingana na maeneo ya ushirikiano yaliyoanishwa katika makubaliano hayo lakini kwa maeneo mengi kitu kinachofanyika hivi sasa ni kupanga namna bora ya utekelezaji wake.

Akizungumza na Waziri wa Mambo ya  Nje na Ushirikiano wa Muungano wa Comoro Bwana Abdoulkarim Mohamed Ikulu jana, Dk. Shein alisema ziara ya wafanyabiashara wa Tanzania  nchini Comoro hivi karibuni ni miongoni mwa hatua za utekelezaji wa makubaliano hayo.

Dk. Shein alimueleza waziri huyo kuwa ziara yake nchini Comoro ilikuwa ya mafanikio makubwa na iliimarisha udugu na urafiki uliopo kati ya watu wa Zanzibar na Comoro ambapo alieleza kuwa kutiwa saini makubaliano ya ushirikiano kati ya nchi mbili hizo kumeupandisha ushirikiano wao katika ngazi nyingine ya daraja la mafanikio.


Katika mazungumzo hayo alimpongeza Rais wa Muungano wa Comoro Dk. Dhoinine Ikulilou kwa jitihada zake za kuimarisha ushirikiano kati ya nchi yake na Zanzibar wakati wote wa uongozi wake.
Aidha alimshukuru Rais wa Muungano wa Comoro kwa kumtumia yeye binafsi na wananchi wa Zanzibar salamu za Kheri ya Mwezi Mutukufu wa Ramadhani.

Kwa upande wake, Waziri wa Mambo yaNje na Ushirikiano wa Muungano wa Comoro, Bwana Abdoulkarim Mohamed aliishukuru Zanzibar na Tanzania kwa msaada wake ikiwemo katika ukombozi wa nchi hiyo.Alieleza kuwa sekta za elimu na habari ndizo zitapewa kipaumbele katika mashirikiano hayo.

Alimueleza Mheshimiwa Rais kuwa Muungano wa Comoro imejidhatiti kutekeleza makubaliano yaliyofikiwa kati yake na Zanzibar na wananchi wa Comoro walifurahishwa sana na ziara ya Dk. Shein nchini Comoro.   

Wakati wa ziara yake nchini humo mwezi Septemba 2014 Zanzibar na Muungano wa Comoro  walitia saini Makubaliano ya Ushirikiano katika maeneo tisa ya ushirikiano ambayo ni elimu, afya, usafiri wa baharini, habari na utamaduni, utalii, kilimo, biashara, uvuvi na masuala ya dini.


Postal Address: 2422 Tel.+255 776 613 015, Fax: 024 2231822 

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.