HOTUBA YA RAIS WA ZANZIBAR NA MWENYEKITI WA BARAZA LA MAPINDUZI, MHE.
DK. ALI MOHAMED SHEIN, KATIKA UZINDUZI WA TAMASHA LA 20 LA UTAMADUNI
WA MZANZIBARI, TAREHE 21/07/2015,
HOTELI YA BWAWANI.
Mheshimiwa Waziri wa Habari, Utamaduni, Utalii na Michezo,Mheshimiwa Naibu Waziri wa Habari, Utamaduni, Utalii na Michezo,Viongozi mbali mbali wa vyama na Serikali,
Mabibi na Mabwana,
Assalamu AlaykumAwali ya yote naanza kwa kumshukuru Mwenyezi Mungu (S.W.T) kwa kutujaalia afya njema tukaweza kukutana hapa kwa ajili ya uzinduzi wa Tamasha la 20 Utamaduni wa Mzanzibari. Kwa dhati kabisa, napenda kuchukua fursa hii kutoa shukurani zangu kwa Wizara ya Habari,
Utamaduni, Utalii na Michezo kwa kunipa heshima ya kuwa Mgeni Rasmi katika Tamasha hili la Utamaduni wa Mzanzibar. Aidha, naipongeza Wizara hii kwa kushirikiana na Kamati Maalum ya Maandalizi na Uendeshaji wa Tamasha hili kwa kuongeza kasi na ubunifu katika matayarisho yake na kulifanya kila mwaka kuwa bora zaidi tangu lilipoanzishwa, mwaka 1994.
Ni dhahiri kuwa juhudi mbali mbali zinazoendelea kuchukuliwa kwa ajili ya kuimarisha Tamasha hili ni hatua muhimu katika kuendeleza mila, silka, desturi na Utamaduni wetu. Vile vile, Tamasha hili linatupa fursa ya kuyakumbuka, kuyafahmu na kuyapima mambo mbali mbali yalivyokuwa yakifanywa na wazee wetu. Kadhalika, Tamasha hili linatupa fursa ya kufahamu namna ambavyo wazee wetu walivyokuwa wakiiendesha shughuli zao za kiuchumi, michezo ya asili na jadi, mashairi, wahenga mashuhuri wa nchi yetu, kazi za mikono kama vile kukuna nazi, kusuka ukili pamoja na mapishi mbali mbali.
Aidha,tamasha hili ni kioo cha kuiangalia jamii yetu kuhus utamaduni hivi sasa na linavyotuzindua na kutuhimiza juu ya umuhimu wa kuulinda utamaduni wetu kwa faida ya vizazi vijavyo.
Ndugu Wageni Waalikwa,
Naamini kuwa Tamasha hili linafanyika katika wakati mzuri. Wakati ambao wananchi wamo katika shamra shamra za kusherehekea Idd - El Fitri, ambazo leo zinamalizika rasmi. Nakutakieni nyote Iddi Njema.
Kwa hivyo, ni dhahiri kuwa kufanyika kwa Tamasha hili katika kipindi hiki kutatoa fursa nyengine kwa wananchi ya kushiriki katika shughuli na sherehe nyengine za kiutamaduni. Vile vile, huu ni wakati mzuri wa kuandaa Tamasha hili tukizingatia kwamba hivi sasa wapo wageni wengi nchini ambao walikuja kuhudhuruia Tamasha la Kimataifa la Filamu la Zanzibar (ZIFF) linalofanyika kila mwaka, ambalo kwa mwaka huu, nililizindua juzi, tarehe 18 Julai, 2015 siku ya sikuu ya Idd el Fitri. Ni vyema, waandaaji wa Tamasha hili wakafanya juhudi za makusudi za kuwaalika wageni waliokuja kwa ajili ya Tamasha la Filamu kama ni njia muhimu ya kuutangaza utamaduni wetu na kulipa hadhi ya Kimataifa Tamasha hili.
Matarajio yangu ni kuwa waandaaji wa Tamasha hili wanafanya juhudi za kutosha za kuweka matangazo katika mahoteli, mitandao na sehemu nyengine za hapa nchini zinazopendwa na watalii, ili nao wapate kuja kuona na kuufahamu utamaduni wetu. Hivi sasa msimu wa utalii umeanza, tunaweza kuyatumia matamasha kama haya ikiwa ni vivutio muhimu vya utalii kama zinavyofanya nchi mbali mbali duniani.
Nimefurahi kusikikia kuwa Sherehe za Mwaka Koga zilizofanyika Makunduchi siku ya Jumapili, ziliwavutia wageni mbali mbali kama kawaida yake na zimemalizika kwa salama. Nawapongeza wale wote walioandaa sherehe hizo pamoja na wanachi kwa kushiriki na kuzifanikisha kwa umahili mkubwa.
Ndugu Wageni Waalikwa,
Nimefurahi kutambua kuwa tamasha hili litakuwa na shughuli nyingi zaUtamaduni wa Mzanzibari ili kukidhi hamu na mararajio ya washiriki na wageni mbali mbali watakaohudhuria . Nimeona kwenye ratiba yenu kuwa zitafanyika shughuli zenye kuelezea matumizi ya lugha yetu ya Kiswahili na lahaja zake, kuonesha na kuelimisha jamii juu mavazi yetu ya asili, mapishi ya vyakula vyetu vya asili, matumizi ya vifaa na zana za asili, mashindano ya ngalawa na michezo mingine. Mambo haya yote yana umuhimu wa pekee katika kuuendeleza Utamaduni wetu katika jamii na kuutangaza nje ya nchi yetu.
Ndugu Wageni Waalikwa,
Kwa kuwa wajasiriamali waliopo nchini ni miongoni mwa washiriki muhimu katika matamashasha kama haya, naamini kuwa Tamasha hili litawapa nafasi nzuri wajasiriamali wetu ya kuzitangaza shughuli zao kwa wananchi na wageni mbali mbali watakaohudhuiria au watakaoangalia kupitia vyombo vya habari. Ninawanasihi waandalizi wa matamasha kama haya waongeze kasi na juhudi ya kushirikiana na wajasirimali katika hatua zote za matayarisho na utekelezaji wake.
Ni muhimu sote tukafahamu kwamba utekelezaji wa dhana ya utalii kwa wote unahimiza uhusiano na ushirikiano wa kisekta kwa mujibu wa shughuli zao, ili juhudi za kuutangaza utalii ziendelee kufanywa na sekta zote na faida zitakazopatikana ziwafikie wananchi wote. Kwa hivyo, katika uandaaji wa tamasha kama hili Wizara ya, Habari,Utamaduni, Utalii na Michezo ihakikishe kuwa inashirikiana na Wizara ya Uwezeshaji, Ustawi wa Jamii, Vijana Wanawake na Watoto ili wananchi katika, makundi yote, waweze kuzitumia na kunufaika na fursa zinazoweza kupatikana kwa kuwepo kwa Tamasha la aina hii.
Miongoni mwa mambo yanayoipatia sifa na heshima ya pekee nchi yetu ni historia na utamaduni wetu wenye mchanganyiko wa mambo mengi mazuri na ya kuvutia. Zanzibar ina historiaa na utamaduni unaovutia wageni
mbali mbali. Kutokana na heshima hiyo, nchi yetu imekuwa ni kituo cha kufanyia mikutano ya Kimataifa inayohusu mambo ya historia na Utamaduni.
Tarehe 10 Juni, 2015, Zanzibar ilikuwa ni mwenyeji wa Mkutano wa Kimataifa wa Muziki uliofanyika katika Ukumbi wa “Dhow Countries Music Academy” (DCMA) Forodhani, Unguja. Mkutano huu liwajumuisha wanamuziki, na wasanii kutoka nchi mbali mbali duniani na ulitoa fursa ya kujadili mchango wa wanamuziki na wasanii wetu katika kukuza utamaduni na muziki hapa Zanzibar na katika ngazi ya Kimataifa.
Vile vile, Zanzibar ilipewa heshima ya pekee katika njanya ya utamaduni kwenye Tamasha la Kimataifa la Muziki na Utamaduni wa Afrika liliofanyika nchini Ujarumani mwezi Juni, 2015. Nilipewa heshima ya kuwa Mgeni maalum katika Tamasha hili. Tamasha hilo lilibeba ujumbe wa “Magical Zanzibar”, tafsiri yake, Zanzibar nchi ya Majaabu. Historia, mazingira mazuri ya nchi yetu, ukarimu wetu,utulivu wa nchi yetu pamoja na mambo kama haya ya utamaduni tunayoyaona katika tamasha hili ndiyo yanayopelekea nchi yetu kupewa majina mazuri na ya kuvutia kama hilo la “Megical Zanzibar”. Halikutungwa kwa kubahatisha au kwa kupendelewa.
Vile vile, katika Tamasha hilo la Ujerumani, kikundi cha Taarabu cha Dhow “Countries Music Academy” cha hapa Zanzibar, kilialikwa na kupewa fursa ya kutumbuiza wageni na washiriki wa Tamasha hilo kwa namna na nyakati mbali mbali. Heshima hii ya Kimataifa tunastahili kupewa kutokana na juhudi zetu za kuilinda na kuitangaza historia na utamaduni wetu pamoja na kuheshimu tamaduni za wenzetu. Hii ni heshima kubwa ambayo nawasihi wananchi tuithamini na tushirikiane katika kuilinda na kuiendeleza.
Ndugu Wageni Waalikwa,
Nimefurahi kuona kuwa hivi sasa, mwamko wa kuulinda na kuudumisha utamaduni wetu unazidi kuwa mkubwa na kumekuwa na matamasha yanayofanywa katika ngazi ya vijiji na maeneo mengine ili kuonesha historia na utamaduni wa sehemu hizo. Tarehe 14 Juni, 2013 nilipata fursa ya kuhudhuria na kuwa Mgeni Rasmi katika Tamasha la Urithi wa Kiutamaduni wa Watu wa Mangapwani ambalo liliandaliwa na wananchi wa Mangapwani na maeneo ya karibu kwa ajili ya kuonesha utamaduni wao na utamaduni wa Zanzibar kwa jumla. Nawapongeza wananchi wa Mangapwani kwa mwamko mkubwa walionao juu ya umuhimu wa kuulinda utamaduni wao na wa watu wa Zanzibar.
Aidha, nawapongeza wananchi wa Ndijani kwa maonesho mazuri ya historia na utamaduni wa watu wa Ndijani waliyofanya tarehe 14 Juni, 2015 katika Sherehe za kuadhimisha kutimia miaka 90 tangu ilipoanzishwa Skuli ya Ndijani. Wito wangu kwa wananchi wote, waige mifano hii ya watu wa Mangapwani na watu wa Ndijani.
Ndugu Wageni Waalikwa,
Ili kuhakikisha kuwa juhudi zetu za kuulinda na kuukuza utamaduni wetu zinafanikiwa, ni lazima uwepo ushirikiano wa kutosha baina ya sekta mbali mbali. Kwa mfano, Viongozi waliopewa dhamana ya kushughulikia Sekta ya Utamaduni lazima wazidishe kasi ya kushirikiana na viongozi wenzao wenye dhamana ya kushughulikia sekta ya Elimu ili kuhakikisha panakuwa na mazingira ya kufundisha Mila, Silka na Utamaduni kupitia mitaala ya elimu katika ngazi zote za elimu; maandalizi hadi vyuo vikuu.
Hoteli za kitalii nazo zihamasishwe kuutangaza utamaduni wetu kupitia vyakula wanavyotayarisha, vifaa avyotumia kupikia na mavazi ya wafanyakazi wao. Aidha, sisi wenyewe tuwe na mkakati wa kutaka wageni watuige kufanya mambo yetu ya asili na utamaduni wanaotutembelea, badala ya sisi kuiga tamaduni zao. Tuwe mfano wa tabia njema.
Tukumbuke kuwa heshima na tabia njema iliyojengeka katika nyoyo za watu wa Zanzibar kutokana na kupenda urafiki, amani na utulivu ni sehemu muhimu ya utamaduni wetu. Kwa hivyo, ni muhimu kila mmoja wetu akahakikishe kuwa anatoa mchango wake katika kulinda, kuukuza na kuutangaza utamaduni wetu kwa kuzingatia mambo mazuri tunayoyapenda sisi wenyewe. Bila ya shaka wageni wetu wavutiwa na mambo yetu na kwa vyovyote vile nao watayapenda na hatimaye mambo haya yataipatia sifa nchi yetu.
Kila mmoja wetu ashiriki kikamilifu katika kuvikataa na kuvipinga vitendo vinavyotia doa, desturi, mila na tamaduni wetu, ikiwa ni pamoja na vitendo vya unyanyasaji wa kijinisia, ambayo hivi sasa Serikali inaendeleza juhudi mbali mbali za kuvikomesha. Kwa mara nyengine, natoa wito kwa wananchi waendelee kuunga mkono Kampeni dhidi ya Unyanyasaji wa Kijinsia tuliyoianzisha rasmi tarehe, 6 Disemba, 2014. Zanzibar bila ya Udhalilishaji na Unyanyasaji wa kijinsia inawezekana.
Ndugu Wageni Waalikwa,
Nimefurahi sana kuona kuwa Katika tamasha hili la 20 la Utamaduni wa Mzanzibari mmemualika Msanii wa muziki wa asili kutoka Comoro Bibi Shamsia Sagaf ambaye atatoa burudani kwa wazanzibari katika Tamasha
hili la Utamaduni. Imani yangu ni kuwa mwaliko huu, ni hatua muhimu katika kuimarisha ushirikiano wa utamaduni na ndugu zetu wa Comoro, sekta ambayo tulikubaliana kuimarisha ushirikiano baina yetu na ndugu
zetu wa Comoro wakati nilipotembelea nchi yao mwezi Septemba 2014.
Wizara ifanye kila liwezalo ili iendeleze juhudi za kasi ya kuwaalika wasanii wengine mashuhuri kutoka nchi za Mwambao wa Mashariki mwa Afrika na sehemu nyenginezo, ili kulipa Tamasha hili umaarufu na hatimae liweze kuwavutia wageni na washiriki wengi zaidi.
Ndugu Wageni Waalikwa,
Kwa mara nyengine tena, natoa shukurani kwa Wizara ya Habari, Utamaduni, Utalii na Michezo pamoja na Kamati Maalumu ya Maandalizi na Uendeshaji wa Tamasha la Utamaduni wa Mzanzibari kwa kunialika kuwa
Mgeni Rasmi. Napenda niwahimize wananchi wajitokeze kwa wingi kuja kuangalia mambo muhimu ya utamaduni wetu yaliyopangwa kufanywa na kuoneshwa katika tamasha hili.
Baada ya maelezo haya machache, sasa natamka kuwa Tamasha la 20 la
Utamaduni wa Mzanzibari limezinduliwa rasmi.
AHSANTENI KWA KUNISIKILIZA
No comments:
Post a Comment