Habari za Punde

Jaji Ramadhani: Mniombee mapenzi ya Mungu yatimie

Na Peter Elias
Dar es Salaam. Mgombea urais kupitia Chama cha Mapinduzi (CCM), Jaji mstaafu Augustino Ramadhani amewataka Watanzania kuendelea kumwombea ili mapenzi ya Mungu ya kumfanya kuwa kiongozi wa Taifa yatimie.
Jaji Ramadhani alisema hayo jana wakati wa sherehe za maadhimisho ya miaka 50 ya Dayosisi ya Dar es Salaam. Katika sherehe hizo, mgombea huyo alikuwa mgeni rasmi akiambatana na Dk Mwele Malecela ambaye pia anawania nafasi hiyo.
Jaji Ramadhani, ambaye ni mchungaji wa kanisa hilo alisema haikuwa mapenzi yake kutangaza nia ya kugombea urais, bali alipata msukumo kutoka kwa Mungu mwenyewe.
“Kila siku watu wananipongeza kwa kujitokeza kuwania urais. Ninawaambia safari bado ni ndefu, wazidi kuniombea ili mapenzi ya Mungu yatimie,” alisema.
Azungumzia rushwa
Kiongozi huyo alisema rushwa imekuwa tatizo kubwa nchini na kubainisha kuwa yeye anachukia na hata Mungu pia haipendi.
Alisema CCM imekuwa ikipambana na rushwa chini ya msemo wake ‘rushwa ni adui wa haki’ na kuwataka wananchi wabadilike na kuepuka rushwa.
Awali akimkaribisha Jaji Ramadhani, Askofu wa Dayosisi ya Dar es Salaam, Dk Valentino Mokiwa alimpongeza kwa kujitokeza kuwania urais, akisema kati ya waliojitokeza, yeye ameonekana kuwa na karama nyingi.
Alisema Jaji Ramadhani amekuwa ni Kasisi wa Kanisa la Anglikana, aliwahi kuwa Brigedia Jenerali, alikuwa Jaji Mkuu wa Mahakama Kuu na pia ni Rais wa Mahakama ya Afrika ya Haki za Binadamu.
“Tuko nyuma yako, tunakuombea kwa Mungu ushinde nafasi ya urais ili utende haki na kupambana na rushwa,” alisema Askofu Mokiwa.
Askofu Mokiwa alisisitiza kuwa wala rushwa wote wafungwe bila huruma ili kuondoa tatizo hilo.
Alipoulizwa kuhusu Jaji Ramadhan kuwa mgeni rasmi katika maadhimisho hayo licha ya kuwa yeye ni kasisi tu wa kanisa hilo, mjumbe wa kamati ya maandalizi ya sherehe hiyo, Mchungaji John Kamoyo alisema uamuzi huo unatokana na uhusiano kati ya Jaji Ramadhani na Askofu Mokiwa.
“Majibu ya swali hilo ni mengi, lakini nadhani ni uhusiano tu kati ya Askofu Mokiwa na Jaji Ramadhani. Kuna mambo mengi lakini nisingependa kueleza hapa,” alisema Mchungaji Kamoyo.

Chanzo: Mwananchi

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.