Habari za Punde

Mwenyekiti wa Tume ya Uchaguzi Zanzibar ZEC Atangaza Majimbo ya Uchaguzi Zanzibar.

TUME YA UCHAGUZI YA ZANZIBAR

Taarifa ya Mwenyekiti wa Tume ya Uchaguzi Mhe. Jecha Salim Jecha Katika

Mkutano na Waandishi wa Habari Juu ya Mabadiliko ya Idadi, Mipaka na

Majina ya Majimbo ya Uchaguzi ya Zanzibar
Tarehe 6 Julai, 2015
Hoteli ya Grand Palace Malindi

Wawakilishi wa Vyombo vya Habari;
Viongozi wa Asasi za Kijamii;
Mabibi na Mabwana.
Assalam Aleykum

Kwanza kabisa naomba nichukuwe nafasi hii kumshukuru Mwenyezi Mungu kwa kutuwezesha kukutana tukiwa wazima na wenye afya. Kwa niaba ya Tume ya Uchaguzi natoa shukurani nyingi kwa kukusanyika nasi muda huu ili kusikiliza taarifa muhimu tutakayoiwasilisha kwa wananchi na wadau wa uchaguzi kupitia katika vyombo mbalimbali mnavyoviwakilisha.

Katika mkusanyiko wa leo tutaitoa taarifa hiyo, lakini naomba muwe na subira kidogo na msikilize maelezo mafupi juu ya chanzo cha kazi hii na katika kuifanya kazi hii ni mambo gani muhimu yaliyozingatiwa na Tume

Ndugu Waandishi, Katiba ya Zanzibar, 1984, Kifungu cha 120(4), kinaielekeza, Tume ya Uchaguzi ya Zanzibar kuwa katika kipindi cha miaka 8 hadi 10 au wakati mwengine wowote, kuchunguza idadi ya mipaka na majimbo ya uchaguzi na baada ya uchunguzi
wake inaweza kubadili idadi, mipaka na majina ya majimbo hayo.

Ndugu Waandishi, kwa kuzingatia maelekezo hayo ya kisheria na kwa kuwa ilikuwa tayari inakaribia miaka 10 tangu mapitio ya mwisho ya majimbo ya uchaguzi yalipofanyika (2004), na kwa kuwa kuacha kuitekeleza kazi hizo, Tume ingekuwa inakiuka Katiba ya Zanzibar, Juni 2014 Tume iliandaa Mpangokazi wa kazi ya uchunguzi wa majimbo na iliusambaza mpango kazi huo kwa Wadau mbalimbali vikiwemo vyama vya siasa.

Mpangokazi huo ulikuwa na maeneo manane ambayo yalipangwa kutekelezwa na Tume katika kazi hiyo. Maeneo hayo ni utoaji wa taarifa kwa wadau juu ya kazi ya uchunguzi wa majimbo na kupitia vyombo vya habari na mikutano na wadau tuliwajulisha wananchi juu ya kazi hiyo muhimu.

Eneo jengine lilikuwa ni kupokea maoni ya vyama vya siasa. Katika kazi hii, Tumeilikutana ana kwa ana na Wawakilishi wa vyama 18 vya siasa vyama vinne vilituma maoni yao kwa maandishi.

 Aidha, Tume ilipokea maoni kutoka Taasisi za Serikali ambapo katika utaratibu huu tulikutana na Wakuu wa Mikoa na Wakuu wa Wilaya,tulikutana na Wawakilishi wa Wizara zote zinazohusika na masuala ya Utawala Bora,masuala ya Tawala za Mikoa, Jeshi la Polisi. Vile vile, tulikutana na Viongozi wa kuchaguliwa kama vile vile Wawakilishi, Wabunge na Madiwani wote wa Unguja na Pemba na hatimae tulifanya mikutano ya wazi ya upokeaji wa maoni ya wananchi na Asasi za kijamii kwa Wilaya zote.

Ndugu Waandishi, baada ya mikutano yote hiyo na wadau tulifanya ziara za kutembelea maeneo ya mipaka ya Shehia yaliyolalamikiwa wakati wa kupokea maoni pamoja na kuwa maeneo hayo yako chini ya mamlaka nyengine, tulitembelea mipaka ya wadi na majimbo yote yaliyokuwa yanagusiwa sana wakati wa kupokea maoni.

Tume ililazimika kutembelea maeneo yote yaliyolalamikiwa nchi nzima, ili kuona maeneo ya mipaka ya majimbo na wadi yaliyolalamikiwa wakati wa upokeaji wa maoni na hatimae kufanya uchambuzi wa maoni yote.


Uchambuzi wa maoni yaliyopokelewa ulifanyika kwa kuzingatia maelekezo ya Katiba, Kifungu cha 120(3) kinasomeka kuwa ; majimbo yote yatakuwa karibuni na wakaazi sawasawa kama inavyoonekana na Tume, lakini Tume inaweza kuepuka shuruti hii
kwa kiwango kile kinachofikiria kuwa inafaa kwa ajili ya kuzingatia

i.  idadi ya watu na zaidi katika kuhakikisha uwakilishi unaofaa katika miji mikubwa na miji ya mashamba yenye idadi ndogo ya watu;

ii.  ukuaji wa idadi ya watu;

iii.  njia za usafiri; na

iv.  mipaka ya sehemu ya utawala.

Ndugu Waandishi kutokana na maoni ya wadau, ziara ambazo tulizifanya katika maeneo mbalimbali na takwimu zinazohusiana na watu na makaazi, Tume ilishawishika kuwa kuna ongezeko kubwa la idadi ya watu katika baadhi ya majimbo na eneo lililozidiwa sana ni Wilaya ya Magharibi.

Eneo hilo limeonyesha kuwa na ongezeko kubwa la idadi ya watu kulinganisha na eneo jengine lolote lile la Zanzibar. Lakini kwa kutumia vigezo hivyo hivyo, Tume ilibaini kuwa kuna baadhi ya majimbo ambayo yana idadi ndogo sana ya watu.

Kufuatia matokeo hayo ya uchunguzi, Tume ilikubaliana kuwa kuna haja kubwa ya kufanya marekebisho ya idadi, majina na mipaka ya majimbo ya uchaguzi kwa kuzingatia maelekezo ya Sheria yanayoelekeza kuwepo na uwiano wa watu baina ya jimbo na jimbo.

Ndugu Waandishi, Tume tayari imekamilisha taarifa ya kazi ya uchunguzi wa idadi, majina na mipaka ya majimbo na iko tayari kuitangaza rasmi mipaka mipya ya majimbo ya uchaguzi kwa umma. Kazi hii kwa asilimia mia kubwa sana imefanywa kwa
kuzingatia maoni ya wadau wote. Tume ya Uchaguzi imeongeza idadi ya majimbo ya Uchaguzi na hivyo kupelekea mabadiliko makubwa ya mipaka ya majimbo kwa takriban majimbo yote. Mabadiliko hayo yatapelekea baadhi ya majina ya majimbo
kubadilika.

Ndugu Waandishi Tume ya Uchaguzi inapenda kutoa taarifa kuwa imekamilisha kazi yake ya uchunguzi wa Idadi, Mipaka na Majina ya majimbo ya Uchaguzi. Tume imeongeza idadi ya majimbo manne ya uchaguzi ya Wawakilishi na kufanya jumla majimbo yote kuwa 54 badala ya 50 yalokuwa ya awali. Baada ya maelezo hayo, sasa naomba niwatangazie majimbo ya uchaguzi yatakayotumika katika uchaguzi wa mwaka 2015.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.