Habari za Punde

Balozi Seif awashukuru wanaCCM jimboni kwake

 Mgombea Nafasi ya Ujumbe wa Baraza la Wawakilishi Jimbo la Mahonda  kwa tiketi ya CCM Balozi Seif Ali Iddi kwa niaba ya wagombea wenzake wa nafasi mbali mbali akiwashukuru wanachama  wa CCM wa Matawi yaliyomo ndani ya Jimbo hilo  katika Mikutano tofauti kwa kuwachaguwa katika kura za Maoni zilizopita mwezi Agosti mwaka huu.

 Wanachama wa CCM wa Tawi la Kitope “B” wakiwa katika Mikutano ya kupongezwa baada ya kuwachagua wagombea wao wa nafasi tofauti kwenye kura za Maoni.

Baadhi ya wanachama wa Chama cha Mapinduzi wa Tawi la CCM  Kazole wakiwa katika Mikutano ya kupongezwa baada ya kuwachagua wagombea wao wa nafasi za Uwakilishi, Ubunge na Udiwani ndani ya Jimbo la Mahonda.

Picha na –OPMR – ZNZ.

Na Othman Khamis Ame. OMPR

Usimamizi na utatuzi wa changamoto zinazowakabili wananchi wa shehia na Wadi zilizomo ndani ya Jimbo la Mahonda zitapatiwa suluhisho  kwa kutumia Ilani na CCM  ya mwaka 2015 – 2020 endapo wananchi hao wataamua kuwachagua Wagombea wa Nafasi zote za Uongozi  ndani ya Jimbo hilo kupitia CCM kwenye Uchaguzi Mkuu utakaofanyika mwishoni mwa mwezi huu.

Wagombea hao walitoa kauli hiyo wakati wakizungumza na Wanachama wa CCM wa Matawi yaliyomo ndani ya Jimbo la Mahonda katika mikutano tofauti ya kuwashukuru  baada ya uamuzi wao wa kuwateuwa kugombea nafasi hizo katika kura za Maoni zilizopita mwezi Agosti mwaka huu.

Balozi Seif Ali Iddi anayewania nafasi ya  Uwakilishi alisema  mambo watakayoyapa kipaumbele endapo watachaguliwa kushika nyadhifa wazizoomba kwa kupitia Ilani ya Uchaguzi ya CCM ni kuhakikisha  wanasiamia upatikanaji  wa huduma za kijamii kama Maji, Umeme pamoja  na  Elimu katika Jimbo hilo.

Alisema zipo baadhi ya shehia hasa zile zilizounganishwa katika Jimbo Jipya la Mahonda ukiachilia mbali za Kitope hadi sasa bado zinakabiliwa na ukosefu wa huduma hizo jambo ambalo ndani ya kipindi cha miaka mitano zitapatiwa ufumbuzi unaofaa.


Balozi Seif  alisema huduma za kusambaza umeme ndani ya Jimbo zima zimeanza rasmi katika vile vijiji ambavyo huduma hiyo haijafika zikianzia katika Kijiji cha Matetema hadi Kichungwani.

Alifahamisha kwamba huduma hizo zitakwenda sambamba na zile za Maji safi na salama pamoja na uimarishaji wa Sekta ya Elimu kwa kuhakikisha kwamba wanafunzi wa skuli zote zilizomo ndani ya Jimbo la Mahonda  wanapata vikalio, Maabara na Maktaba.

Akigusia chuki zinazoendelea kuenezwa na baadhi ya wanasiasa kwa wapiga kura wa Jimbo la Mahonda Balozi Seif  alisema bila ya Chama cha Mapinduzi kushinda kwenye Jimbo hilo wananchi wake wako hatarini  na chuki za upinzani.
Alisema chuki hizo ziko wazi kutokana nabaadhi ya watu kuanza kupita maeneo tofauti ya Jimbo hilo na kufanya zoezi la kuhakikishi pamoja na kupiga picha mashamba yaliyomo ndani yake wakitaraji kurejeshewa.

Balozi Seif alifahamisha kwamba upinzani umeahidi kwamba endapo utashika madaraka ya Nchi jambo la kwanza ni kirejesha  mashamba na Nyumba zote zilizotaifishwa mara baada ya Mapinduzi ya Mwaka 1964.

Alitahadharisha kwamba Wananchi wakifanya makosa ya kutoa kura kwa chama kisichokuwa cha Mapinduzi waelewe kuwa wamejiangamiza wenyewe na wasije tafuta mchawi.

Mh. Bahati Ali Abeid Nassir  anayewania nafasi ya Ubunge  kupitia  tiketi ya Chama cha Mapinduzi alisema katika kukabiliana na changamoto ya ajira hasa kwa Vijana ameahidi kushirikiana na Viongozi wenzake  katika  kuwakusanya Vijana kuunda vikundi vya ujasiria amali kwa lengo la kujiajiri wenyewe.

Mh. Bahati alisema hakuna njia ya mkato katika kukabiliana na changamoto ya ajira ambayo imekuwa ikiyakumba pia Mataifa mbali mbali Ulimwenguni yakiwemo yale yaliyoendelea kiviwanda.

Alifahamisha kwamba Vikundi hivyo vitapatiwa vifaa pamoja na zana zitakazowawezesha kuendesha miradi yao ya kujitegemea kutegemea na maeneo wanayoishi kwa vile Serikali kuu tayari imeshakusudia kuimarisha miundo mbinu mbali mbali ya kiuchumi ikiwemi Utalii na Kilimo cha umwagiliaji.

Aliwatanabahisha Wananchi hasa Vijana kuwa hadhari  na ushawishi unaoendeleza kufanywa na baadhi ya Watu hasa wanasiasa wa kuwarubuni vijana kwamba watawapatia ajira endapo watawachagua katika kinyang’anyiro cha uchaguzi kinachotarajiwa kufanyika Tarehe 25 Mwezi huu wa Oktoba.

 Mh. Bahati aliwakumbusha wazazi kwamba bado wana dhima ya kuwaelekeza watoto wao juu ya Historia ya Taifa hili lililopatikana kwa njia ya Mapinduzi kutoka mikononi mwa wakoloni waliokuwa wakiendeleza udhalimu dhidi ya Wazawa wa Taifa hili.

 Kwa upande wake akitoa shukrani kwa wanachama hao wa CCM wa Matawi tofauti  ya Jimbo la Mahonda  Bibi Hadia  Juma Chum  anayewania nafasi ya Udiwani Wadi ya Fujoni.

Akigusia chaguzi za maoni zilizomaliza mchakato wake Mh. Bahati alisema si vizuri kwa wana CCM kwenda kwenye uchaguzi Mkuu wakiwa na vidonda vya uchaguzi wa kura za Maoni.

Alisema wakati wa makundi umekwisha na kufutwa  kabisa na liliopo mbele kwa wana CCM hao ni kuhakikisha Chama cha Mapinduz kinashinda ili kiendelee kuongoza Dola. 

Mh. Bahati alifahamisha kwamba Vijana wa Chama cha Mapinduzi kusema kwamba mgombea wa chama hicho hawamtaki waelewe kuwa wao ndio wenye matatizo.

Nao  Nd. Haji Hadhil  Mkadam  Mgombea nafasi ya Udiwani Wadi ya Mahonda na Bibi Hadia Juma Chum anayewania Udiwani wadi ya Fujoni aliwaasa Wananchi hasa Vijana kuelewa kwamba amani ya Nchi ndio hazina kubwa inayoringia Tanzania katika nyanja ya Kimataifa.

Walisema kuchezewa kwa amani hiyo ni kuliangamiza Taifa na watakaoathirika na kudhalilika zaidi ni kundi kubwa la akina mama na Watoto mambo ambayo kila mwananchi anapaswa kusaidia kupambana nayo.

Wagombea Udiwani hao wa Wadi za Mahonda na Fujoni Nd. Haji Fadhil Mkadam na Bibi Hadia Juma Chum walifahamisha kwamba kazi kubwa iliyopo kwa wananchi wa Mahonda ni kushirikiana na wenzao Nchini katika kuisimamia CCM iendlee kuongoza Dola ya Tanzania kwa kuwachagua wagombea wake.

Walisema Chama cha Mapinduzi kinachotokana na mifupa ya Vyama vya TANU na ASP ndicho Chama chenye dhamira sahihi ya kuendelea kuyalinda Mapinduzi ya Zanzibar ya Mwaka 1964 yaliyozaa Muungano wa Tanganyika na Zanzibar.

Wagombea hao wa nafasi tofauti za Uongozi Jimbo la Mahonda kupitia Chama cha Mapinduzi tayari wameshakamilisha ziara ya kushukuru kwa Matawi ya CCM  ya Kinduni, Kitope “B”, Kazole, Matetema pamoja na Mkadini.

Matawi mengine yaliyobaki  ya CCM ambayo pia wataendelea na ziara hiyo ya kushukuru ni pamoja na Zingwezingwe, Mangapwani, Kiomba Mvua pamoja na Wadi ya Upenja ambayo kwa sasa imo ndani ya Jimbo Jipya la Kiwengwa.


No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.