Habari za Punde

Dk Shein aipongeza Marekani kwa kuiunga mkono Tanzania kwenye miradi ya maendeleo kupitia Mfuko wa Milenia


STATE HOUSE ZANZIBAR
OFFICE OF THE PRESS SECRETARY
PRESS RELEASE
Zanzibar                                                                 8.10.2015
---
RAIS  wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Ali Mohamed Shein amezipongeza hatua za Serikali ya Marekani ya kuahidi na kuhakikisha kuendelea kuiunga mkono Tanzania ikiwemo Zanzibar katika uendelezaji wa awamu ya pili ya miradi inayofadhiliwa na Mfuko wa Changamoto za Milenia (MCC).

Dk. Shein aliyasema hayo leo, huko Ikulu mjini Zanzibar wakati alipofanya mazungumzo na Balozi wa Marekani katika Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Mark Childress.

Katika mazungumzo hayo, Dk. Shein alimueleza Balozi huyo wa Marekani kuwa hatua hizo zinaonesha dhahiri uhusiano mwema na ushirikiano uliopo kati ya Tanzania na Marekani hali ambayo itaimarisha na kukuza zaidi uimarishaji wa sekta za maendeleo kwa upande wa Tanzania Bara na Zanzibar.

Dk. Shein alisema kuwa azma ya Marekani ya kuendelea kuiunga mkono Tazania katika kuendeleza awamu ya pili ya Mfuko wa Changamoto za Milenia (MCC) ni heshima kubwa kwa Tanzania kwani ni miongoni mwa nchi chache zilizopata bahati za kuendelea katika awamu hiyo ya pili ya MCC.


Pamoja na hayo, Dk. Shein aliipongeza nchi hiyo kwa kuendelea kuiunga mkono Zanzibar katika kuimarisha miradi mbali mbali ya maendeleo hapa nchini.

Nae Balozi Mark Childress alimuhakikishia Dk. Shein kuwa awamu ya pili ya Mfuko wa MCC itatekelezwa na nchi yake na tayari fedha zake zimeshatengwa kwa ajili ya miradi mbali mbali itakayotekelezwa na Mfuko huo kwa Zanzibar na Tanzania Bara.

Balozi Childress alitumia fursa hiyo kumueleza Dk. Shein kuwa nchi yake inathamini uhusiano na ushirikiano mkubwa uliopo kati yake na Tanzania ikiwemo Zanzibar na kuahidi kuuendelea kuiunga mkono Zanzibar katika kuimarisha miradi ya maendeleo.

Pamoja na hayo Balozi huyo wa Marekani alimueleza Dk. Shein kuwa hatua nzuri imefikiwa na Marekani katika kutekeleza azma yake ya ujenzi wa  maabara ya kisasa huko kisiwani Pemba unaotarajiwa kuanza hivi karibuni.

Dk. Shein pia alitukutana na Balozi wa Sweden katika Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Katarina Rangnitt na kumueleza kuwa Zanzibar inathamini uhusiano na ushirikiano na nchi hiyo hasa katika kuimarisha sekta za maendeleo ikiwemo sekta ya afya ambapo Sweden imekuwa ikiiunga mkono Zanzibar kwa muda mrefu

Wakati huo huo Dk. Shein alifanya mazungumzo na Balozi mpya wa Denmark katika Jamhuri ya Muungano wa Tanzani na kumueleza jinsi Zanzibar inavyothamini uhusiano na ushirikiano mzuri uliopo kati ya pande mbili hizo.

Dk. Shein aliipongeza Denmark kwa kuisaidia Zanzibar katika kuimarisha sekta za maendeo ikiwemo sekta ya elimu kwa kupitia Shirika lake la Maendeleo la DANIDA.

Kwa nyakati tofauti wa mazungumzo ya Mabalozi hao na Rais Dk. Shein, Mabalozi hao walitumia fursa hiyo kumpongeza Dk. Shein kwa kuiongoza vyema na mashirikianom mazuri Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar yenye Muundo wa Umoja wa Kitaifa.

Pia, Dk. Shein alifanya mazungumzo na Balozi Mteule wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania nchini Malawi Mhe. Victoria Mwakasege aliefika Ikulu kwa ajili ya kuaga ambapo katika mazunguzo yao, Dk. Shein alimueleza Balozi huyo kuwa Tanzania na Malawi zina uhusiano na ushirikiano wa muda mrefu hivyo kuna kila sababu za kuuimarisha.

Dk. Shein alimueleza Balozi huyo haja ya kuimarisha uchumi wa Kidiplomasia kwa kuishajiisha sekta ya utalii, uwekezaji na biashara kati pamoja na kuitangaza lugha ya Kiswahili nchini Malawi kwa kuzingatia kuwa kiswahili kimekuwa kikisomesha hadi vyuo vikuu hapa nchini vikiwemo Chuo Kikuu cha Dar-es-Salama na Chuo Kikuu cha Taifa cha Zanzibar (SUZA).

Aidha, Dk. Shein alitumia fursa hiyo kuwaeleza Mabalozi hao kuwa uchaguzi mkuu ujao utakuwa huru, wa haki na utakuwa wa amani na utulivu mkubwa . 

Rajab Mkasaba, Ikulu Zanzibar

Postal Address: 2422 Tel.:0777427449. Fax: 024 2231822
E-mail: rajabmkasaba@yahoo.co.uk

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.