Habari za Punde

Mafunzo ya Wasimamizi na Maafisa Uchaguzi Mkoa wa Dar es Salaam Yafanyika leo.

Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam Said Mecki Sadiki Akifungua mafunzo ya siku mbili ya waratibu wa Uchaguzi,Wasimamizi wa Uchaguzi, Wasimamizi wasaidizi wa Uchaguzi na Maafisa uchaguzi leo jijini Dar es salaam.
Waratibu  wa Uchaguzi,Wasimamizi wa Uchaguzi, Wasimamizi wasaidizi wa Uchaguzi na Maafisa uchaguzi waliohudhuria mafunzo leo jijini Dar es salaam kujiandaa usimamizi wa uchaguzi mkuu wa Rais, Wabunge na Madiwani Oktoba 25 mwaka huu. 
Picha/ Aron Msigwa- MAELEZO.

Na.Aron Msigwa- MAELEZO.
Mkuu wa mkoa wa Dar es slaam Said Mecki Sadiki amewataka Waratibu wa Uchaguzi, Wasimamizi wa Uchaguzi na viongozi wa vyama vya Siasa katika mkoa huo kuhakikisha kuwa wanafanya kazi zao kwa ushirikiano ili kuwawezesha wananchi kupiga kura kwa amani na utulivu na kuepusha manung'uniko yanayoweza kujitokeza.

Akifungua mafunzo ya siku mbili ya waratibu wa Uchaguzi,Wasimamizi wa Uchaguzi, Wasimamizi wasaidizi wa Uchaguzi na Maafisa uchaguzi leo jijini Dar es salaam Mkuu huyo wa mkoa amesema kuwa Dar es salaam ni miongoni mwa maeneo yenye wapiga kura wengi hivyo  mkoa kwa kushirikiana na Tume ya uchaguzi umejipanga kuhakikisha kuwa wananchi wote waliojiandikisha wanapiga kura kwa amani na utulivu Siku ya uchaguzi Oktoba 25 mwaka huu.

Amesema Wakurugenzi wa Halmashauri wa mkoa huo ambao ndiyo wasimamizi wa uchaguzi katika wilaya wanalo jukumu la kuwaita na kuwaelimisha viongozi wa vyama vya siasa juu ya taratibu na kanuni za kufuata wakati wa uchaguzi mkuu ili wajenge mazingira rafiki ya kufanya kazi kwa ushirikiano.

Aidha, amewasisitiza wasimamizi hao kutojihusisha kwa namna yoyote ile na kampeni za siasa wakati wa kutekeleza majukumu yao kwani kufanya hivyo watakuwa wanahujumu ufanisi wa uchaguzi mkuu katika mkoa wa Dar es salaam.

Ili kudumisha amani na utulivu vituoni amewataka kufanya kazi zao kwa umakini mkubwa kwa kuwa suala la amani vituoni litakuwa mikononi mwao wakati wa kipindi chote cha upigaji wa kura Oktoba 25 mwaka huu. 

"Simamieni kanuni, sheria na taratibu, msionyeshe upendeleo wowote wala kufanya kampeni za aina yoyote ile ndani ya vituo vya kupigia kura, jambo hilo halikubaliki hata kidogo,mfanyeni kazi mliyotumwa ili msiwe sehemu ya tatizo katika nchi hii" Amesisitiza Sadiki.


Ametoa wito kwa wananchi kuendelea kutunza kadi zao za kupigia kura ili waweze kuzitumia siku ya uchaguzi na kuvionya vikundi, watu au vyama vinavyojaribu kuwarubuni wananchi kwa kununua kadi zao za kupigia kura kuacha tabia hiyo.

" Watu wanaofanya hivi wanafanya unyang'anyi, nawataka waache tabia hii kwani haina tija kwa mamaendeleo ya taifa letu,ukichukua au kuiba kadi ya mtu unamnyima haki ya kupiga kura muhusika na huo sio uungwana" Amesisitiza.

Ametoa wito wananchi wa mkoa wa Dar es salaam kudumisha amani wakati wa upigaji wa kura na kuwataka wananchi wote waliopanga kufanya vurugu wakati wa uchaguzi kuacha

"Sisi kama Serikali hatuvumilia aina yoyote ya uvunjifu wa amani, tutaimarisha ulinzi yapo maeneo korofi ambayo yamekuwa na vitendo vya uvunjifu wa amani tunayajua, tunawahakikishia wananchi watapiga kura kwa amani na kurudi makwao wakiwa salama"

Kuhusu waangalizi wa Kimataifa waliowasili nchini ambao baadhi yao watafanya kazi jijini Dar es salam amesema watafanya kazi zao kwa mujibu wa taratibu na kanuni walizopewa na Tume na kuongeza kuwa kazi yao itakua ni kuangalia kama tumnazingatia na kufuata sheria tulizojiwekea na si kuingilia shughuli za wasimamizi wa zoezi la upigaji wa kura.

"Suala la kusimamia zoezi la upigaji wa kura ni letu wenyewe, msiwaruhusu waanze kuwapa taratibu za upigaji wa kura wa nchi walizotoka wala kutoa maamuzi yoyote, kazi yao itakua ni kuangalia mwenendo wa uchaguzi wetu na si vinginevyo" amesisitiza.

Aidha, amevitaka vyama vya siasa kuhakikisha kuwa vinawapeleka mawakala wao mapema katika vituo vya kupigia kura kabla ya kuanza kwa zoezi la upigaji wa kura ili kuondoa manung'uniko yanayoweza kujitokeza.

Kwa upande wake Bi. Clesensia Mayala ambaye ni Kaimu Mkuu wa Sehemu, Kanda ya Kusini Tume ya Taifa ya Uchaguzi amesema lengo la mafunzo hayo ni kuwakumbusha wasimamizi na Maafisa uchaguzi kuzingatia na kufuata taratibu zilizotolewa na Tume ili waweze kufanya kazi zao kwa ufanisi.

Amesema katika mafunzo hayo washiriki hao watajadili masuala mbalimbali ikiwemo wajibu na majukumu ya waratibu na wasimamizi wa uchaguzi,majukumu ya makarani waongozaji wa vituo vya kupigia kura ,kuangalia fomu zitakazotumika wakati wa upigaji kura,taratibu za upigaji kura, Fomu zitakazotumika wakati wa kuhesabukura, kujumlisha na kutangaza matokeo ya Urais,Wabunge na Madiwani.

Amefafanua kuwa wasimamizi wote wa uchaguzi watakua na jukumu la kuhakikisha kuwa vituo vyote ya uchaguzi vinafunguliwa kwa wakati na kufungwa kwa kuzingatia muda uliopangwa ili kuhakikisha kuwa wananchi wote wanatimiza wajibu wao wa kikatiba.


Kwa upande wake Msimamizi wa Uchaguzi Wilaya ya Temeke Bw. Photidas Kagimbo amesema uchaguzi mkuu katika eneo analolisimamia utafanyika kwa uhuru na usalama na kuongeza kuwa wamejipanga vyema kuwahudumia wananchi wote waliojiandikisha ambao watajitokeza kupiga kura siku hiyo.

Amesema Tume ya Taifa ya Uchaguzi inaendelea kupeleka vifaa mbalimbali katika maeneo mbalimbali ili kuwawezesha wananchi kupiga kura Oktoba 25 na kufafanua kuwa  kazi  inayoendelea sasa ni utoaji wa elimu ya mpiga kura kwa wananchi.

Kuhusu uhakiki wa taarifa za wananchi katika daftari la kudumu la Wapiga kura kwa wananchi walioshindwa kuhakiki kutokana na sababu mbalimbali amesema liko mikononi mwa Tume ya Taifa ya uchaguzi na kwamba wao wanasubiri maelekezo ya Tume hiyo na daftari kamili litakalokuwa na orodha ya wapiga kura wote litakalopelekwa kwenye vituo vya kupigia kura kabla ya tarehe ya  uchaguzi ili kutoa fursa kwa vyama vya siasa na wananchi kupitia majina yote.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.