Afisa Mawasiliano Mwandamizi wa TPA,
Bw. Focus Mauki (kushoto) akifafanua jambo kwa Waandishi wa Habari (hawapo
pichani) kuhusu matumizi ya Mfumo mpya wa malipo wa Kelektroniki kulipia huduma
za Bandari. Mfumo huo wa malipo tayari umeanza kutumika tangu mwezi Julai mwaka
huu na umeongeza ufanisi wa Bandari na kurahisisha kazi ya kutoa mizigo
Bandarini. Katikati ni Kaimu Mkurugenzi wa TEHAMA wa Mamlaka, Bw. Kilian Challe
na Afisa Habari wa Idara ya Habari Maelezo, Bw. Frank Mvungi.
Kaimu Mkurugenzi wa TEHAMA wa TPA,
Bw. Kilian Challe akiwaeleza Waandishi wa Habari kuhusu mipango ya Mamlaka kuanza
kutumia huduma za simu za mkononi, Master Card na Visa kulipia gharama za
Bandari kwa kupitia mfumo wake mpya wa Malipo kwa njia ya Kielektroniki (IePS).
Kushoto ni Afisa Mawasiliano Mwandamizi TPA, Focus Mauki na Afisa Habari kutoka
Idara ya Habari Maelezo, Bw. Frank Mvungi.
Na Focus
Mauki-TPA
Wateja wa Bandari ambao ni Mawakala
wa kutoa mizigo Bandarini sasa wataanza kutumia huduma za malipo kupitia njia
za Simu za Mkononi, Visa Card na Master Card wakati wa kulipia gharama za
huduma Bandari.
Hayo yamesemwa na Kaimu Mkurugenzi wa
TEHAMA, Bw. Kilian Chale wakati wa mkutano wake na Waandishi wa Habari uliofanyika
katika ukumbi wa Idara ya Habari Maelezo Ijumaa, Oktoba 9.
“Napenda kuwatangazia wateja wetu na
Watanzania wote kuwa katika siku za karibuni Mfumo wetu wa Malipo kwa njia ya
Kielektroniki (IePS) ambao tuliuzindua Julai 2015 utaanza kuruhusu matumizi ya
Master Card, Visa na simu za mkononi katika kulipia huduma za Bandari,” amesema
Kilian.
Kilian ametoa wito kwa Mawakala wa
Mizigo Bandarini kuendelea na usajili wa kutumia mfuo huu ili kurahisisha na
kuharakisha kazi ya kutoa mizigo Bandarini na kuongeza ufanisi wa Bandari
katika kuhudumia wateja wake.
Tayari Mawakala wengi wameanza
kutumia mfumo huu ambao tayari umeeunganishwa na Benki za CRDB, NMB na Benki ya
Posta ili kumwezesha Wakala kupata Ankara ya malipo, kufanya malipo na kisha
kwenda moja kwa moja katika eneo la kuchukulia mzigo ndani ya Bandari.
Mpaka sasa Wakala anaweza kutumia Benki
ya CRDB na NMB kufanya malipo kwa kutumia CRDB Sim Banking, CRDB Internet Banking,
CRDB fahari Huduma, NMB Internet Banking, NMB Mobile Banking na pia anaweza
kutumia matawi ya CRDB, NMB na Benki ya Posta.
Ili kuweza kutumia mfumo huu wakala
anapaswa kusajiliwa na Mamlaka na baada ya kusajiliwa anaweza kuingia katika mfumo
kupitia tovuti rasmi ambayo ni www.tpapayments.com.
Mteja wa kawaida pia anaweza kuingia
katika tovuti hii na kuweza kuona Ankara ya malipo ya huduma za Bandari kwa
kila mzigo au gari aliloagiza. Pamoja na mambo mengine mfumo huu unatarajiwa
kuweka uwazi na kupunguza kwa kiwango kikubwa malalamiko ya wateja ya kukosa taarifa sahihi za gharama za mizigo yao.
No comments:
Post a Comment