Na Mwandishi Wetu Pemba.
Viongozi wa CCM Zanzibar wamewataka wananchi na wanaCCM kumpigia kura Dk.
Ali Mohamed Shein ili aendelee kuiongoza Zanzibar miaka mitano ijayo kwani
ahadi zake zinatekelezeka na tayari ameshafanya mambo mengi ya kimaendeleo
Unguja na Pemba.
Hayo waliyaeleza leo huko katika mkutano
wa Kampeni ya uchaguzi wa CCM uliofanyika Makombeni, Mkoa wa Kusini Pemba uliohudhuriwa
na maelfu ya wanaCCM na wananchi ambapo mgeni rasmi alikuwa mgombea nafasi ya
Urais wa Zanzibar kwa tiketi ya CCM, Dk. Ali Mohamed Shein.
Viongozi hao wa CCM walipata fursa ya
kusalimiana na wananchi pamoja na WanaCCM waliohudhuria katika mkutano huo waliwaeleza
haja ya kumchagua tena Dk. Shein kutokana na uadilifu wake na utekelezaji wa
ahadi zake.
Nae Omar Yussuf Mzee, ambaye ni Waziri wa
Fedha wa Serikali ya Mapinduzi ya
Zanzibar, alisema kuwa ipo haja ya kushindana kwa Sera, kwani Dk. Shein
anapofanya na anapoahidi jambo anakuwa ameshafanya hesabu.
Waziri Yussuf alishangazwa na CUF kusema
kuwa wakipata madaraka watatoa mshara wa Shilingi laki nne na kuuliza fedha
hizo watazipata wapi kwani tayari Dk. Shein ameshaeleza kuwa yeye atatoa kima
cha chini kwa mwaka wa kwanza kitakuwa laki tatu kwani anajua fedha zilizopo.
Alisema kuwa tayari CCM imeshashinda na
kuwataka wanaCCM kudumisha amani kwani vyama vya upinzani wanataka kuivunja ili
uchaguzi usifanyike na kusema kuwa meli itakapokuwa tayari itawachukuwa bure wanachama
wa CCM kwenda Unguja kushuhudia Dk. Shein anavyoapishwa.
Waziri wa Maji,Ardhi na Nishati Ramadhan
Abdalla Shaaban alisema kuwa mgombea nafasi ya urais kupitia chama cha CUF
anawadharau wananchi kwa sababu amekuwa akiwadanganya kwa kiasi kikubwa hasa
kwa suala la mafuta.
Alisema kuwa suala la mafuta limeanza
kushughulikiwa kwa muda mrefu kwani Dk. Shein baada ya kuingia madarakani
ameanza kulishughulikia suala hilo kwani kupata mafuta inachukua muda mrefu
ambapo kwa teknolojia ya sasa hufika hadi miaka mitano.
Alisisitiza kuwa tayari Dk. Shein
ameshatekeleza Sera na tayari Sheria iko tayari na lililobaki ni kujadiliwa na
kusema kuwa huwezi kuchimba mafuta bila ya kuwa na sheria.
Alisema kuwa katika katiba iliyopendekezwa
tayari suala la mafuta lilikuwa limeshatolewa lakini hata hivyo tayari sheria
ya kutoa ruhusa imeshatolewa baada ya juhudi za Dk. Shein na Rais Jakaya Mrisho
Kikwete.
Nae Naibu Katibu Mkuu wa CCM Zanzibar
Vuai Ali Vuai, alitoa pongezi kwa wanaCCM wa Pemba kwa kuendelea kukiunga mkono
Chama Cha Mapinduzi na kusema kuwa CCM inaendesha kampeni kwa kistaarabu bila
ya kumtukana mtu wala kugombana na mtu na kuvitaka vyama vya upinzani navyo
kufanya hivyo.
Bi Zainab Omar Mohammed ambaye ni Waziri
wa Wizara ya Uwezeshaji, Ustawi wa Jamii, Vijana , Wanawake na Watoto alieleza
kuwa Serikali ina mpango wa kuanzisha Benki ya Wanawake.
Alisema kuwa wanawake na vijana wamekuwa wakipewa mikopo
bila ya riba yoyote na kueleza kuwa CCM haitaki kukopiwa Sera zake huku
akieleza haja ya kumpongeza rais kwa kuanzisha Mfuko wa Uwezeshaji.
Alisema kuwa Wilaya zote za Pemba
walipewa mikopo, wakulima wa mwani nao waliangaliwa ambapo Rais aliwagaiya
mwenyewe wakulima wa zao hilo wa Pemba na Unguja na hivi sasa wanawake hawabebi
tena mwani kwenye vichwa.
Alieleza kuwa vijana wamepewa green house
ambazo zote hizo amezitoa Dk. Shein na kuwasifu wanaCCM kwa kutoyumba huku
akisisitiza kuwa udhalilishaji sasa basi kwani hivi sasa Serikali imo katika
kampeni ya kupambana na hali hiyo na atakaefanya hivyo sheria itafuata mkondo
wake kwa kufungwa miaka 30.
Alisema kuwa kuna nyumba tatu za wazee
ikiwemo ya Sebleni, Welezi na Limbani ambapo wazee wanalelewa na kupata milo
mitatu ya uhakika pamoja na fedha za kujikimu huku watoto yatima nao
wakiendelea kutunzwa.
Nae Mjumbe wa Kamati Kuu, Khadija Aboud
aliipongeza Wadi ya Makombeni kwa kuhakikisha kila uchaguzi wadi hiyo inakuwa
ya CCM na kuwataka wananchi na wanaCCM kuwachagua viongozi wa CCM
Alisema kuwa Dk. Shein ndie Rais anaefaa
kutokana na kuleta maendeleo makubwa Zanzibar ndani ya miaka mitano iliyopita
na anafaa kupewa miaka mitano mengine
huku akiwataka vijana kuichagua CCM.
Nae Haji Mkema, Mjumbe wa Halmashauri Kuu
ya Taifa ya CCM aliwataka wananchi na wanaCCM kumpa kura zote Dk. Shein
kutokana na kutekeleza sekta za maendeleo ikiwemo maji, umeme, barabara, afya
sambamba na kudumisha amani na utulivu.
Alisema kuwa hulka na tabia yake ikiwa ni
pamoja na kuwa na huruma ambapo tayari hivi karibuni ameshaiondosha michango ya
skuli za msingi na Sekondari hapo baadae huku akiondosha malipo kwa wazazi pamoja
na wazee.
Alimsifu Dk. Shein kwa kuimarisha uwanja
wa Gombani, uwanja wa Amani na uwanja wa Maotsetung hivi karibuni utaanza matengenezo
na hivi karibuni Fumba kutatengenezwa uwanja mwengine mpya wa michezo.
Skuli za Sekondari zimeimarika ikiwa ni
pamoja na kuleta waalimu kutoka sehemu mbali mbali wakiwemo kutoka Nigeria, kuwepo
kwa vyuo vikuu na kuanzishwa kipya huko Dole pamoja na kuimarisha vyuo vya
amali ambapo hivi karibuni vyuo hivyo vitaengezwa katika maeneo ya Mtambwe na
Makunduchi.
Mapema Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa
Kaskazini Pemba Mberwa Hamad Mberwa, alisema kuwa ushindi wa CCM wa mwaka huu
utakuwa mkubwa tena wa kishindo sambamba na kupata mafanikio mara tatu kuliko
yale ya mwaka 2010.
No comments:
Post a Comment