Habari za Punde

RAIA WAAMILIFU WALILIA HUDUMA BORA KWA WAKULIMA

Na Krantz Mwantepele,

“Huku tupo tu tunahangaika na kilimo, tunalima kila mwaka,

lakini ukweli ni kwamba kilimo chetu wala hakina faida basi

tu bora siku ziende”


Lilikuwa ni jibu toka Alex Jonh maarufu kwa jina la

“Mafuriko” mmoja wa wanaharakati na waraghbishi wa kijiji

cha Lugunga, kilichopo wilaya ya Mbogwe, mkoani Geita

baada ya kuulizwa swali kuhusu maendeleo ya kijiji chao na

mmoja wa waandishi wa habari za mitandao Ali Masoud

maarufu kwa jina la Kipanya.


Kijiji hiki kina wakazi wanakadiriwa kuwa na wakazi 3,685

wengi wao wakiwa ni wakulima wadogo wadogo. Kilimo

kinaajiri karibu 75% ya wakazi wa vijijini. Lakini ni ukweli

pia, ni kilimo ambacho bado kinategemea jembe la mkono na

mvua na hivyo kuathiri sekta hiyo kwa kiasi kikubwa.


Tukiacha hiyo pia upatikanaji wa pembejeo kwa mifumo

iliyomo kwenye sera ya kilimo, bado ni changamoto kubwa.

Waraghbishi wengi ni wakulima, ingawa wapo pia walimu,

viongozi wa dini, wenyeviti wa vijiji, na watendaji wa kata

lakini ukweli unabaki  kwamba wengi wao wanategemea

kilimo. Changamoto wanazokutana nazo wakulima ndiyo

sababu inayopelekea kilimo kutokuwa cha faida hali

inayowakatisha tamaa na kusema bora liende.

Mraghbishi Alex John maarufu kwa jina Mafuriko akiongea na mwandishi wa habari wa gazeti la Mwananchi Herieth Makwetta alipotembelea kijijini hapo .

Akielezea masikitiko yake kuhusu hali yetu, mraghbishi Alex
John ama Mafuriko anasema:

“Ndugu zangu sisi huku tumesahaulika kabisa, kilimo chetu

tunacholima ni kilimo cha bora liende maana hatuna kabisa

elimu yoyote hapa kijijini. Kila mtu analima na kupanda

anavyojua maana tumeshazoea maisha ya hivi.”

Katika ufafanuzi wake Mafuriko ameendelea kusema kuwa

kijiji chao kina ardhi yenye rutuba na inayokubali mazao

mengi yakiwemo mahindi, maharage, mpunga na karanga

lakini licha ya kuwa na ardhi nzuri kama hiyo bado kilimo

hakina faida kwao.

Mchora Katuni Ali Masoud (mwenye miwani)
akizungumza na waraghbishi na wananchi wa kijiji
cha Lugunga


Lakini ni sababu gani inayowafanya wakose faida katika

kilimo chao licha ya kuwa na ardhi nzuri inayokubali zaidi ya

mazao ya aina tatu. Hapo ndipo waraghbishi walipoanza

kuelezea changamoto wanazokabiliana nazo.

Akifafanua ukubwa wa tatizo linalowakabili wakulima wa

kijiji hapo raia mwamilifu na mraghbishi Gabriel Jonathan

anasema:

“Unajua ndugu mwaandishi hapa kijijini tatizo ni moja,

asilimia kubwa ni wakulima na wakulima wengi hawana

elimu. Unaona, wengi wao wameishia darasa la saba na

wengine hawajasoma kabisa, hivyo hata kilimo chao

wanalima ili mradi msimu upite hata akilima heka mbili

akatoa gunia tano kwake anaona sawa.”

Ni kweli kilimo ni suala la kitaalamu na hivyo kuna uhitaji

mkubwa wa ufahamu kwa mkulima, na hapo ndipo serikali

inapomwajiri Afisa Kilimo. Ambaye kimsingi ndio mwenye

jukumu hilo katika kuhakikisha anawatembelea wakulima na

kuwasaidia kitaalamu ili waweze kuzalisha mazao mengi na

yenye ubora.

Hali hii iliibua hamu ya kutaka kujua iwapo kijijini hapo yupo

Afisa wa Kilimo ama Bwana Shamba kama anavyojulikana na

wengi, katika hali ya kutokuridhishwa na kiwango cha

huduma anachotoa mtaalamu huyo wa mashamba,

mraghbishi Mafuriko alisema,

“Bwana Shamba yupo tena yupo sana lakini hana ushirikiano

kabisa na wakulima wa Lugunga, kwanza hakai hapa kijijini.

Pili wengine hawamjui kabisa yaani kwa wiki anaweza kuja

mara mbili au msimuone mwezi mzima ila mshahara

analipwa”

Akiongezea kuhusu upatikanaji wa Afisa huyo Yohana Julius

alisema:

“Tunasikia anaishi Masumbwe na anapoishi hatujui ni mtaa

gani na wala mimi simjui licha ya kwamba nakaa hapa

katikati (Center) hata nikikutana naye bila kuambiwa simjui

je mwananchi anayeishi Mahameni itakuwaje”

Mahameni ni kitongoji kilichopo pembeni ya kijiji cha

Lugunga ambapo pia bwana Shamba wa kijiji hicho

anatakiwa kufika katika kutimiza wajibu wake.

Mraghbishi Gabriel (wa kwanza kushoto) akiwa na wananchi
wenzake wa kijiji cha Lugunga, wakisikiliza maswali toka kwa
mwandishi


Umbali wa kutoka Masumbwe hadi Lugunga ni kilometa 17

hali inayodhihirisha kuwepo umbali mrefu kati ya anapoishi

Afisa kilimo huyo Dickson Silvester na kituo chake cha kazi.

Kukaa tu na kulaumu hakusaidii sana hivyo ni jukumu la

waraghbishi kujua nini wanachotakiwa kufanya,  

“Mimi naona hapa tuandamane mpaka ofisi ya Mkurugenzi,

yeye ni mwajiri wake na inawezekana akawa hana hata

taarifa ya nini kinafanyika huku, alisikika mmoja wa

wananchi aliyetambulika kwa jina moja la Hassan.

Katika hatua nyingine wananchi hao wakapaza sauti kwa

kumtaka afisa kilimo huyo kurudi kuishi kijijini na kuongeza

kuwa kama alikubali kuja kufanya kazi na kupokea mshahara

basi akubali kuishi katika kijiji hicho cha Lugunga kama

wanavyoishi wananchi alioenda kuwatumikia.

Safari ya kujua ukweli wa kwanini afisa kilimo huyo haishi

katika kituo chake cha kazi ilizidi kusonga mbele na ndipo

mwandishi wa makala hii alipomtafuta kwa njia ya simu na

kufanya naye mahojiano yaliyodumu kwa dakika kumi na

tano.

Katika mahojiano hayo afisa kilimo huyo Dickosn Silvester

alikiri kuwa yeye ndiye afisa kilimo wa kijiji cha Lugunga na

kukanusha taarifa za kuwa haishi katika kituo chake cha kazi.

“Mimi ni afisa kilimo wa Lugunga kweli na ninaishi hapo

hapo Lugunga Center aliyekwambia siishi hapo ni nani?

Mana huo ni uzushi”, alisikika akisema Dickson kwa njia ya

simu wakati akiongea na mwandishi wa makala hii.

Baada ya kupata majibu ambayo hayakuniridhisha kutoka

kwa afisa kilimo huyo nilirudi Lugunga kwa njia ya simu na

kumtafuta mwenyekiti wa kitongoji cha Lugunga Kati

(Center) bwana Mashiba Dioniz ili kupata ukweli yalipo

makazi ya afisa kilimo huyo.

“Mimi ndiye mwenyekiti wa kitongoji cha hapa Senta,

kwakweli mwandishi huyo afisa kilimo hana makazi hapa

mimi nazijua kaya zangu zote, Ila huwa namuona mara moja

kwa wiki basi ila kusema anaishi hapa ni uongo kabisa.’

Alisema Bwana Mashiba mwenyekiti wa Lugunga.

Lakini waraghbishi hawa si tu wanajaribu kufuatilia

upatikanaji wa huduma za ugani katika kijiji chao, ila

wameendelea kutoa elimu kwa wanakajiji wengine wa kijiji

hapo. Mfano mmoja ni migogoro baina ya wakulima

wenyewe. Na kwa kuwa waraghbishi hawa hawaitishi

mikutano ya vijiji mara nyingi wamekuwa wakitumia maeneo

ya migogoro kama sehemu yao ya kutolea elimu.

Akifafanua hilo Felix Daudi, mraghbishi mwingine katika

kijiji hicho anasema,


“Kuna kesi tunakutana nazo ambazo tunazitumia pia kutoa

elimu. Moja ya kesi hizo ni zile na mtu kuacha mifugo yake

bila uangalizi na mwishowe inaingia kwenye mashamba ya

watu na kuanza kula mazao. Utakuta mtu hajui wapi

akapeleke tatizo lake ama akishaikamata mifugo hiyo afanye

nayo ni nini,”

Hivyo ni vizuri watendaji wa serikali wakashirikiana na

waraghbishi na muda mwingine kuwapatia ujuzi mdogo

mdogo. Hii itasaidia kufanikisha shabaha ya Maendeleo

kwani pande zote watakuwa wanategemeana. Na si katika

hali hii ambayo watu wanashutumiana.  Hivyo ni jukumu letu

sote kucheza nafasi zetu katika kusukuma gurudumu la

maendeleo.

                 Moja ya mashamba ya mpunga yaliyopo katika kijiji cha Lugunga

                      CHANZO ; MWANAHARAKATI MZALENDO BLOG 

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.