Habari za Punde

Dk Shein: Wananchi jitokezeni kwa wingi kuadhimisha miaka 52 ya Mapinduzi

STATE HOUSE ZANZIBAR
OFFICE OF THE PRESS SECRETARY
PRESS RELEASE
    Zanzibar                                                  03 Januari, 2016
---
TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI
Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Ali Mohamed Shein ametoa wito kwa wananchi wa Unguja na Pemba kujitokeza kwa wingi kusherehekea maadhimisho ya miaka 52 ya Mapinduzi yanayoanza leo.

Dk. Shein amesema wananchi wana kila sababu za kushiriki maadhimisho hayo kwa kuwa Mapinduzi ya tarehe 12 Januari, 1964 ndiyo yaliyoleta Uhuru kwa wananchi wa Unguja na Pemba kutoka kwa wakoloni.

Akizungumza na waandishi wa habari mara baada ya kushiriki zoezi la kufanya usafi katika soko la matunda la Mombasa mjini Unguja leo, Dk. Shein alisema wananchi wanaelewa vyema historia ya Mapinduzi ya Zanzibar na kwamba wanajua wajibu wao katika kuyalinda na kuyadumisha.

Dk Shein alisisitiza kuwa “Kila mtu ana haki na wajibu wa kuyaenzi na kuyaendeleza Mapinduzi ya mwaka 1964” kwa kuwa ni dhahiri hakuna mwananchi asiethamini uhuru wake.


Rais wa Zanzibar aliwaeleza waandishi wa habari na wananchi waliohudhuria zoezi hilo kuwa Mapinduzi ya mwaka 1964 yameleta maendeleo kwa kila mwananchi na kwamba hakuna mwananchi asiyefaidika na matunda ya Mapinduzi.

Dk. Shein alisema Mapinduzi ya mwaka 1964 yalifanyika kwa malengo maalum ya kuwakomboa wananchi Zanzibar kwa kuwa mazingira yaliyokuwepo wakati huo kitendo cha kufanya Mapinduzi kilikuwa hakiwezi kuepukika.

Alibainisha kuwa wapo wanaoyakumbuka kwa furaha na wengine wamenuna lakini Mapinduzi yalikuwa ni lazima na ndivyo ilivyofanyika na sasa Zanzibar iko huru.

Aliwataka wananchi kushiriki katika ratiba mbalimbali za maadhimisho hayo yakiwemo mashindano ya mpira wa miguu ya Kombe la Mapinduzi yanayoanza leo katika uwanja wa Amaan Zanzibar.

Postal Address: 2422 Tel.+255 776 613 015, Fax: 024 2231822 

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.